I
UTANGULIZI:
1.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja
kwamba Bunge lako Tukufu liweze kujadili na kupitisha makadirio ya mapato na
matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2012/2013. Pamoja na hotuba hii,
nimewasilisha vitabu vinne vya Bajeti vinavyoelezea takwimu mbalimbali za
Bajeti. Kitabu cha Kwanza kinaelezea makisio ya mapato.
Kitabu cha Pili kinaelezea makisio ya matumizi ya kawaida
kwa Wizara, Idara zinazojitegemea; Taasisi na Wakala wa Serikali; cha Tatu
kinahusu makisio ya matumizi ya kawaida kwa Mikoa na Mamlaka za Serikali za
Mitaa na cha Nne kinaelezea makadirio ya matumizi ya maendeleo kwa
Wizara, Idara zinazojitegemea, Taasisi na Wakala za Serikali; Mikoa na
Mamlaka za Serikali za Mitaa. Aidha, upo Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2012 ambao ni sehemu ya Bajeti hii.
Mamlaka za Serikali za Mitaa. Aidha, upo Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2012 ambao ni sehemu ya Bajeti hii.
2.
Mheshimiwa Spika, awali
ya yote, naomba nitumie fursa hii kumshukuru kwa dhati Mheshimiwa Dkt. Jakaya
Mrisho
Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa imani kubwa aliyonayo kwangu kwa kuniteua kuwa Waziri wa Fedha. Naahidi kutekeleza majukumu niliyokabidhiwa kwa umakini na uaminifu mkubwa.
Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa imani kubwa aliyonayo kwangu kwa kuniteua kuwa Waziri wa Fedha. Naahidi kutekeleza majukumu niliyokabidhiwa kwa umakini na uaminifu mkubwa.
3.
Mheshimiwa Spika, napenda kuwapongeza
wafuatao kwa kuteuliwa na Mheshimiwa Rais kuwa mawaziri kama ifuatavyo: Mhe.
Prof. Sospeter Mwijarubi Muhongo (Mb); Mhe. Mhandisi Christopher Kajoro Chiza
(Mb); Mhe. Dkt. Harrison George Mwakyembe (Mb); Mhe. Dkt. Fenella Ephraim
Mukangara (Mb); Mhe. Balozi Khamis Sued Kagasheki (Mb); Mhe. Dkt. Abdallah
Omari Kigoda (Mb). Aidha, napenda kuwapongeza wafuatao kwa kuteuliwa kuwa naibu
mawaziri katika Wizara mbalimbali, Mhe. Janet Zebedayo Mbene (Mb); Mhe. Saada
Mkuya Salum (Mb); Mhe. Dkt. Seif Suleiman Rashid (Mb.); Mhe. George Boniface
Simbachawene (Mb.); Mhe. January Yusuf Makamba (Mb.); Mhe. Dkt. Charles
John Tizeba (Mb.); Mhe. Amos Gabriel Makalla (Mb.); Mhe. Angela Jasmine Kairuki
(Mb.); Mhe. Stephen Julius Maselle (Mb.); na Mhe. Mhandisi Dkt. Binilith Satano
Mahenge (Mb). Kadhalika, nampongeza Mhe. James Mbatia (Mb) kwa kuteuliwa na
Mhe. Rais kuwa Mbunge.
4.
Mheshimiwa Spika, nawapongeza pia, Mhe.
Alhaji Adam Kimbisa (Mb.); Mhe. Shy Rose Banji (Mb.); Mhe. Abdulah Alli Hassan
Mwinyi (Mb); Mhe. Charles Makongoro Nyerere (Mb); Mhe. Dkt Twaha Issa Taslima
(Mb); Mhe. Nderkindo Perpetua Kessy (Mb); Mhe. Bernard Musomi Murunyana (Mb);
Mhe. Anjela Charles Kizigha (Mb.); Mhe. Maryam Ussi Yahaya (Mb.), ambao
wamechaguliwa kutuwakilisha kwenye Bunge la Afrika Mashariki. Ni matumaini
yangu watatuwakilisha vyema kwa maslahi na manufaa ya Taifa letu.
5.
Mheshimiwa Spika, maandalizi ya Bajeti
hii yamehusisha wadau na Taasisi mbalimbali. Napenda kuwashukuru walioshiriki
kwa namna moja au nyingine kufanikisha matayarisho yake. Kwa namna ya pekee, ninaishukuru
Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi chini ya uenyekiti wa Mhe. Mtemi Andrew John
Chenge, Mbunge wa Bariadi Magharibi, pamoja na kamati nyingine za kisekta kwa
ushauri mzuri waliotoa wakati wakichambua mapendekezo ya Bajeti hii. Aidha,
ninawashukuru Waheshimiwa Wabunge wote kwa ushauri na mapendekezo yao ambayo
yamezingatiwa katika Bajeti hii.
6.
Mheshimiwa Spika, napenda kumshukuru
Mhe. Stephen Masatu Wasira (Mb), Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mahusiano na
Uratibu kwa ushirikiano alionipatia wakati wa maandalizi ya Bajeti. Aidha,
nawashukuru Naibu Mawaziri wa Fedha, Mhe. Janet Zebedayo Mbene (Mb) na Mhe.
Saada Mkuya Salum (Mb). Namshukuru Katibu Mkuu Ndugu Ramadhani M. Khijjah;
Naibu Katibu Wakuu, Ndugu Laston T. Msongole; Dkt. Servacius B. Likwelile; na
Ndugu Elizabeth Nyambibo kwa mchango wao mkubwa katika matayarisho ya Bajeti.
Vilevile, nawashukuru Prof. Benno Ndulu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania;
Dkt. Phillip Mpango, Katibu
Mtendaji Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango; Ndugu Harry Kitilya, Kamishna Mkuu wa
Mamlaka ya Mapato Tanzania; na Dkt. Albina Chuwa, Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya
Takwimu ya Taifa. Nawashukuru wote kwa mchango wao katika maandalizi ya bajeti
hii. Naishukuru pia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kutayarisha kwa
wakati Muswada wa Sheria ya Fedha ya mwaka 2012 na nyaraka mbalimbali za sheria
ambazo ni sehemu ya Bajeti hii.
7.
Mheshimiwa Spika, napenda kuwashukuru
Wakuu wa Idara, Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Fedha na wafanyakazi
wote wa Wizara ya Fedha kwa ushirikiano wao. Aidha, namshukuru Mpigachapa Mkuu
wa Serikali kwa kuchapisha Hotuba hii kwa wakati. Nawashukuru pia wataalamu na
wale wote waliotoa mapendekezo kuhusu sera, mikakati na masuala mbalimbali ya
kodi ambayo yamezingatiwa katika kuandaa Bajeti hii.
8.
Mheshimiwa Spika, Tanzania imekuwa
mwenyeji wa Mikutano ya Bodi ya Magavana wa Benki ya Maendeleo ya Afrika kwa
Mwaka 2012 iliyofanyika kuanzia tarehe 28 Mei hadi tarehe 2 Juni 2012 na
kufunguliwa rasmi na Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania. Mikutano hii ilifanyika kwa ufanisi mkubwa katika Kituo
cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha na kuhudhuriwa na washiriki 2,350 kutoka
ndani na nje ya Tanzania. Hii imekuwa ni nafasi ya kipekee kwa Tanzania
kutangaza fursa mbalimbali za kiuchumi zilizopo nchini. Aidha, washiriki wa
ndani kutoka sekta binafsi walipata nafasi ya kufahamu fursa za mikopo zilizopo
katika Benki ya Maendeleo ya Afrika. Napenda kutoa wito kwa sekta binafsi
kutumia fursa hizo kikamilifu.
9.
Mheshimiwa Spika, Bajeti ya mwaka
2012/13 imelenga kukabiliana na changamoto zinazokabili uchumi ikiwa ni pamoja
na; kuongeza fursa za kukuza uchumi, kushughulikia uhaba wa chakula nchini,
kupambana na mfumuko wa bei, kuendelea kuimarisha ukusanyaji wa mapato na
kusimamia matumizi, kushughulikia suala la ukosefu wa ajira hasa kwa vijana,
kuwekeza katika miundombinu ya nishati ya umeme hususan ujenzi wa bomba la gesi
kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam, barabara, bandari na reli ya kati ili
kupunguza gharama za kufanya biashara na kuongeza tija katika uzalishaji;
pamoja na kulipa madeni ya ndani na nje.
MWAKA 2011/12
10.
Mheshimiwa Spika, baada ya utangulizi
huo, naomba sasa kutoa taarifa kuhusu utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2011/12. Mfumo
wa Bajeti ya mwaka 2011/12 uliendeleza juhudi za Serikali za kufikia malengo ya
Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025. Aidha, bajeti ilizingatia utekelezaji wa
vipaumbele vya Mpango wa kwanza wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/12 –
2015/16); Awamu ya Pili ya Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini
(MKUKUTA II); Malengo ya Maendeleo ya Milenia 2015; Mkakati wa Pamoja wa
Misaada Tanzania (MPAMITA); Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010; Mkakati wa
Taifa wa Madeni; pamoja na kuimarisha usimamizi wa kodi na matumizi ya fedha za
Umma.
11.
Mheshimiwa Spika,
misingi na shabaha za bajeti ya mwaka 2011/12, pamoja na mambo mengine,
ililenga kukamilisha malengo ya Serikali ya kukabiliana na changamoto za
kupunguza makali ya maisha kwa wananchi; kuendelea kuboresha mfumo wa makusanyo
ya mapato ya ndani; kuboresha mazingira ya uwekezaji wa ndani na nje;
kuendeleza sekta binafsi ili kupanua wigo wa kodi; kukamilisha maandalizi ya
Mradi wa Vitambulisho vya Taifa; na kutenga rasilimali na kutekeleza miradi
katika maeneo ya kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi.
12.
Mheshimiwa Spika,
maeneo mengine yaliyozingatiwa katika misingi na shabaha ya bajeti hiyo
yalikuwa ni: kutekeleza mipango na mikakati maalum ya kuharakisha ukuaji wa uchumi;
kutafuta mikopo ya masharti nafuu na ya kibiashara; kuharakisha utekelezaji wa
Sheria ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na ya Binafsi ili kupanua fursa za
utekelezaji wa miradi ya maendeleo; Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012;
kuhakikisha kwamba maduhuli ya Serikali yanakusanywa ipasavyo na kuwasilishwa
katika Mfuko Mkuu wa Serikali; pamoja na kulinda na kudumisha mafanikio
yaliyopatikana katika Sekta za huduma za jamii, hususan elimu na afya ambazo
zimekuwa na upanuzi mkubwa wa huduma.
Hatua za Utekelezaji
wa Bajeti ya mwaka 2011/12
Kupunguza Makali ya
Maisha
13.
Mheshimiwa Spika,
katika utekelezaji wa Bajeti ya mwaka
2011/12, Serikali iliendelea kuchukua hatua mbalimbali kukabiliana na
changamoto zinazowakabili wananchi kwa lengo la kupunguza makali ya maisha
kunakotokana na kupanda kwa bei za bidhaa na huduma. Hatua zilizochukuliwa ni
pamoja na: kurekebisha namna ya kukokotoa gharama za mafuta na kutangaza bei
elekezi kila mwezi na kuanzisha utaratibu wa uagizaji mafuta kwa pamoja (bulk
procurement). Hatua hizi zimesaidia kupunguza kasi ya upandaji wa bei ya mafuta
hapa nchini.
14.
Mheshimiwa Spika,
Serikali imetumia shilingi bilioni 296
kutekeleza mpango wa dharura wa kukabiliana na tatizo la upungufu wa nishati ya
umeme kwa kutumia mitambo ya kukodi. Utekelezaji wa jitihada hizi umeongeza
megawati 324 kwenye Gridi ya Taifa. Kadhalika, Serikali ilitumia Dola za
Marekani milioni 183 kugharamia ujenzi wa mitambo ya kufua umeme wa megawati
100 kwa mkoa wa Dar es Salaam mradi ambao umekamilika na uko kwenye hatua za
majaribio na Megawati 60 kwa mkoa wa Mwanza ambao bado ujenzi unaendelea.
15.
Mheshimiwa Spika,
Serikali imetumia shilingi bilioni 27
kugharamia ununuzi na usambazaji wa tani 120,000 za mahindi katika masoko kwa
lengo la kukabiliana na uhaba wa chakula kwa baadhi ya maeneo. Aidha, Serikali
ilitoa vibali vya kuagiza sukari bila kutoza ushuru wa forodha kiasi cha tani
200,000 ili kukabiliana na uhaba na kupanda kwa bei ya sukari. Kadhalika,
Serikali ilipandisha kiwango cha riba inayotozwa na Benki Kuu kwa Taasisi za
Fedha kutoka asilimia 7.58 hadi asilimia 12.58. Vilevile, Serikali ilipandisha
kiwango cha amana ambacho benki za biashara zinapaswa kuhifadhi Benki Kuu
kutoka asilimia 20 hadi asilimia 30. Hatua hizi zimesaidia kupunguza kasi ya
kupanda kwa bei.
Kuwezesha
Wananchi Kiuchumi na Kuongeza Ajira
16.
Mheshimiwa Spika,
katika kukabiliana na tatizo la ajira, Serikali imechukua hatua mbalimbali za
kuongeza fursa za ajira. Hatua hizo ni pamoja na: kuboresha mazingira ya kisera
na kisheria kuwezesha sekta binafsi kukua; kupanua huduma za fedha ikiwa ni
pamoja na kuongeza mitaji katika Benki ya Rasilimali, Benki ya Wanawake, Benki
ya Posta na Twiga Bancorp, na kufanikisha uanzishwaji wa kampuni ya kutoa
mikopo ya muda mrefu ya ujenzi wa nyumba na makazi. Hatua nyingine
zilizochukuliwa na kuchangia ongezeko la ajira ni pamoja na kujenga miundombinu
ya barabara, umeme, kilimo, mawasiliano na kuwezesha wananchi kupitia programu
mbalimbali za uwezeshaji. Aidha, kuna Taasisi mbalimbali ambazo zimechangia
kutoa ajira kama vile, TASAF, SELF, VETA, Shirika la Viwanda Vidogovidogo (SIDO),
Taasisi ndogondogo za Fedha, VICOBA, Benki za Kijamii na Mifuko ya Udhamini ya
mikopo inayosimamiwa na Benki Kuu. Katika mwaka 2011/12, Serikali iliajiri
Walimu wa Shule za Sekondari na Msingi 25,000, Maafisa Ugani wa Kilimo na
Mifugo 4,499 na Watumishi wa Kada ya Afya 6,916.
Uboreshaji wa Mazingira Wezeshi kwa Sekta Binafsi
17.
Mheshimiwa Spika, Serikali ilianza
utekelezaji wa Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Uwekezaji mwaka 2011 kufuatia
kuidhinishwa kwake mwaka 2010. Kupitia Mpango huu, taratibu na kanuni za
mawasilisho na malipo ya kodi na ushuru yanafanyika kwa njia ya mtandao.
Utaratibu huu umeongeza ufanisi kwa kuondoa usumbufu na upotevu wa muda katika
ulipaji wa kodi. Hadi sasa, zaidi ya asilimia 75 ya walipa kodi wakubwa na
walipa kodi wengine 2,795 wanafanya mawasilisho yao kwa njia ya mtandao.
Aidha, Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania ilianzisha mfumo
unaounganisha usimamizi wa kodi (Asycuda, ITAX) na benki za biashara ili
kurahisisha ulipaji wa kodi. Mfumo huu umeunganisha jumla ya benki 25.
Kadhalika, Mamlaka inatumia huduma za M-Pesa (Vodacom) na “NMB mobile”
kwa ajili ya kulipia kodi ya majengo na kodi ya mapato.
18.
Mheshimiwa Spika, Serikali iliendelea
na jitihada za kupunguza urasimu katika utoaji wa mizigo bandarini kwa
kuanzisha utaratibu wa kuwasilisha nyaraka kwa njia ya mtandao kabla ya mizigo
kuwasili. Utaratibu huu umelenga kupunguza tatizo la mrundikano na upotevu wa
nyaraka na kupelekea kupungua kwa muda na gharama za uagizaji na usafirishaji
mizigo nje ya nchi. Serikali imepunguza vizuizi vya usafirishaji mizigo
ndani ya nchi kutoka 50 vilivyokuwepo kufikia 15, isipokuwa vituo vya mizani na
forodha. Lengo la hatua hii ni kupunguza gharama za kufanya biashara na
usumbufu wanaopata wafanyabiashara.
Sera za Mapato
19.
Mheshimiwa Spika,
katika mwaka 2011/12, Serikali iliendelea kuboresha mfumo wa ukusanyaji wa
mapato ya ndani yanayotokana na kodi na yasiyo ya kodi kwa kuchukua hatua za
kiutawala, kisera pamoja na marekebisho ya viwango vya kodi na sheria.
20.
Mheshimiwa Spika,
Serikali ilifanya marekebisho katika Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani,
SURA 148 ili kuboresha uzalishaji katika sekta za Kilimo, Mifugo, Viwanda,
Biashara na Utalii. Marekebisho hayo ni pamoja na kusamehe Kodi ya Ongezeko la
Thamani kwenye vipuri vya zana za kilimo; chakula cha kukuzia kuku; nyuzi za
kutengenezea nyavu za kuvulia samaki; pamoja na kuanzisha utaratibu wa
kuwarejeshea kodi wageni kwa bidhaa walizonunua nchini wakati wanaondoka.
21.
Mheshimiwa Spika, Serikali ilifuta msamaha wa Kodi ya
Ongezeko la Thamani kwenye kuuza na kupangisha majengo ya nyumba za kuishi za
Shirika la Nyumba la Taifa - NHC; kuondoa unafuu wa Kodi ya Ongezeko la Thamani
kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali isipokuwa kwenye vifaa vya misaada kwa vituo
vya kulelea watoto yatima na shule.
22.
Mheshimiwa Spika, Serikali
pia ilifanya marekebisho ya Sheria ya Kodi ya Mapato, SURA 332 kwa kufuta kodi
ya Zuio kwa usafirishaji wa samaki nje ya nchi ili kuongeza utoaji wa huduma za
usafirishaji wa mazao ya samaki kutokea hapa nchini badala ya kupitia nchi za
jirani. Aidha, marekebisho yalifanyika katika Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, SURA
147 kwa kupunguza ushuru wa bidhaa kwenye mafuta mazito ya kuendeshea mitambo
ili kupunguza gharama za uzalishaji.
23.
Mheshimiwa Spika,
Sheria
ya Ushuru wa Mafuta ya Petroli, SURA 220 ilifanyiwa marekebisho kwa kutoa
msamaha wa ushuru unaotozwa kwenye mafuta yanayotumika katika kuendesha meli,
na vifaa vingine vinavyotumika katika utafiti wa mafuta na gesi ili kupunguza
gharama. Aidha, marekebisho yalifanyika kwenye Sheria ya Forodha ya
Jumuiya ya Afrika Mashariki, ya mwaka 2004 kufuatia kuridhia kwa Mawaziri
wa Fedha wa Nchi Wanachama kufanya marekebisho mbalimbali katika kukuza Sekta
za Viwanda, Usafirishaji, Mifugo, Biashara na Utalii. Vilevile, marekebisho
yalilenga katika kuboresha afya ya jamii na kuimarisha ulinzi na usalama wa
raia na mali zao.
24.
Mheshimiwa Spika,
hatua nyingine zilizochukuliwa ni pamoja na kuhamasisha na kuhakikisha
mashine za kielectroniki – EFD zinatumika ipasavyo; kuimarisha mfumo wa
kusimamia vitalu vya kodi; kuongeza vituo vya kutoa huduma kwa wateja na vya
kukusanyia mapato; kuimarisha mifumo ya malipo ya kodi; na kuboresha mfumo wa
uthaminishaji kwa kuimarisha ukaguzi wa hesabu za walipa kodi.
Mwenendo wa Ukusanyaji
Mapato
25.
Mheshimiwa Spika, katika
mwaka wa fedha 2011/12, Serikali ilipanga kukusanya mapato ya jumla ya shilingi
bilioni 13,525.9 kutoka katika vyanzo mbalimbali na kutumia kiasi hicho kwa
matumizi ya kawaida na maendeleo. Vyanzo vya mapato vilikuwa kama ifuatavyo:
mapato ya ndani yalikadiriwa kufikia kiasi cha shilingi bilioni 6,775.9; mapato
kutoka Serikali za mitaa yalikadiriwa kufikia kiasi cha shilingi bilioni 350.5;
misaada na mikopo ya kibajeti ilikadiriwa kufikia kiasi cha shilingi bilioni
869.4; misaada na mikopo ya miradi ya maendeleo na ya kisekta ilikadiriwa
kufikia kiasi cha shilingi bilioni 3,054.1; mikopo ya ndani na nje yenye
masharti ya kibiashara ilikadiriwa kufikia kiasi cha shilingi bilioni 1,664.9;
na mikopo ya kulipia dhamana na hatifungani zinazoiva zilikadiriwa kufikia
kiasi cha shilingi bilioni 810.9.
26.
Mheshimiwa Spika,
kwa upande wa mapato ya ndani ikijumuisha mapato ya Halmashauri, hadi Aprili
2012 makusanyo yamefikia jumla shilingi bilioni 5,684.5. Kiasi hiki ni sawa na
asilimia 80 ya makadirio ya kukusanya shilingi bilioni 7,126.4 kwa mwaka
2011/12.
27.
Mheshimiwa Spika,
makusanyo ya kodi yalifikia shilingi bilioni 5,227.5 ambayo ni sawa na asilimia
84 ya makadirio ya kukusanya shilingi bilioni 6,228.8. Kulingana na mwenendo wa
makusanyo ya mapato ya kodi kwa kipindi cha miezi kumi ya mwaka 2011/12, hadi
kufikia mwishoni mwa mwaka wa fedha 2011/12 Serikali inatarajia kukusanya jumla
ya shilingi bilioni 6,307.8 na hivyo kuweza kufikia lengo tulilojiwekea.
28.
Mheshimiwa Spika,
mapato yasiyotokana na kodi yamefikia shilingi bilioni 451.6 ikiwa ni asilimia
83 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 547.1 kwa mwaka. Kutokana na mwenendo
huo, Serikali inatarajia hadi Juni 2012 kufikia lengo.
29.
Mheshimiwa
Spika, mapato ya Serikali za Mitaa yalifikia kiasi
cha shilingi bilioni 143, sawa na asilimia 40.8 ya lengo la kukusanya shilingi
bilioni 350.5 kwa mwaka. Hadi Juni 2012, Serikali inatarajia kukusanya jumla ya
shilingi bilioni 200 kutokana na chanzo hiki ikiwa ni asilimia 57 ya lengo la
mwaka. Kutokufikia malengo ya ukusanyaji wa mapato haya kumechangiwa na
kuchelewa kuanza kutekeleza utozaji wa ada za leseni.
Misaada na Mikopo ya Masharti Nafuu Kutoka Nje
30.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka
2011/12, Serikali ilikadiria kupata kiasi cha shilingi bilioni 869.4 kama
misaada na mikopo ya kibajeti ambapo hadi sasa Serikali imepokea shilingi
bilioni 916.3, ikiwa zaidi kwa shilingi bilioni 46.9. Ongezeko hili limetokana
na baadhi ya wafadhili kutoa fedha zaidi ya kiwango walichoahidi. Kwa upande wa
misaada na mikopo ya miradi ya maendeleo ikijumuisha mifuko ya kisekta, hadi
kufikia Aprili 2012 ilifikia shilingi bilioni 1,450.4 sawa na asilimia 47 ya
makadirio ya bajeti ya mwaka ya shilingi bilioni 3,054.1. Upungufu huu
umesababishwa na kasi ndogo ya utekelezaji wa baadhi ya miradi na kuchelewa
kupokea taarifa ya fedha hizi kutoka kwa washirika wa maendeleo na Wizara na
Taasisi zinazotekeleza miradi husika.
Mikopo ya Ndani
31.
Mheshimiwa Spika, katika
kipindi cha Julai 2011 hadi Aprili 2012, Serikali imekopa kiasi cha shilingi
bilioni 526 kwa ajili ya kulipia dhamana za Serikali zilizoiva ikiwa ni
asilimia 64 ya lengo la mwaka la shilingi bilioni 819.1. Aidha, Serikali
ilipanga kukopa shilingi bilioni 393.4 sawa na asilimia moja ya Pato la Taifa
kwa ajili ya kugharamia matumizi ya maendeleo. Hadi kufikia Aprili 2012,
Serikali ilikuwa imekopa shilingi bilioni 232.6 sawa na asilimia 59 ya
makadirio ya mwaka.
Mikopo ya Nje yenye
Masharti ya Kibiashara
32.
Mheshimiwa Spika, mwaka
2011/12 Serikali ilikadiria kukopa kiasi cha Dola za Marekani milioni 822, sawa
na shilingi bilioni 1,271.6 kama mikopo ya kibiashara. Katika kipindi cha Julai
2011 hadi Aprili 2012, Serikali ilisaini Mkataba wa mkopo wa kiasi cha Dola za Marekani
milioni 310 na Benki ya Standard ya Afrika Kusini. Hadi kufikia Aprili 2012,
jumla ya Dola za Marekani milioni 229 ambazo zilitumika kulipia madeni
ya barabara ya mwaka 2010/11. Aidha, Serikali ilisaini Mkataba wa mkopo wa Euro
milioni 61 na Benki ya HSBC. Mkopo huu umeelekezwa kugharamia ujenzi wa mtambo
wa kufua umeme wa megawati 60 Nyakato Mwanza. Serikali pia imesaini mkataba wa
mkopo wa Dola za Marekani milioni 350 kutoka Benki ya Credit Suisse ya
Uingereza ambapo Dola za Marekani milioni 200 zimepokelewa mwanzoni mwa Mwezi
Juni 2012. Kiasi kilichobaki cha Dola za Marekani milioni 150 kitapatikana
na kutumika mwaka 2012/13.
33.
Mheshimiwa Spika, Serikali
imepata Mshauri Mwelekezi ambaye ataishauri Serikali katika zoezi la kujiandaa
kufanyiwa tathmini ya uwezo wa kukopa na kulipa madeni (Sovereign Credit
Rating). Maandalizi haya yataiwezesha nchi kufanyiwa
tathmini yanatarajiwa kukamilika mwanzoni mwa mwaka 2013. Kukamilika kwa zoezi
hilo kutawapatia wakopeshaji imani na hivyo kuiwezesha Serikali kupata mikopo
yenye masharti nafuu ya kibiashara kwa wakati.
Sera
za Matumizi
34.
Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2011/12, Serikali iliendelea kutekeleza sera za matumizi kulingana na
upatikanaji wa mapato ya ndani, misaada pamoja na mikopo ya ndani na nje.
Aidha, Serikali iliendelea kuboresha usimamizi na udhibiti wa matumizi ya fedha
za umma, ikijumuisha udhibiti wa ulipaji wa mishahara, matumizi katika miradi
ya maendeleo, ruzuku ya pembejeo, ununuzi wa umma na kuendelea kudhibiti
malimbikizo ya madeni. Serikali imeandaa mkakati wa kulipa na kudhibiti madeni
yatokanayo na malimbikizo ya madai ya watumishi; wakandarasi; wazabuni; na
madeni mengineyo. Madeni hayo yatalipwa baada ya kuhakikiwa na Mkaguzi Mkuu wa
Ndani.
Programu ya Maboresho
ya Usimamizi wa Fedha za Umma
35.
Mheshimiwa Spika, katika jitihada za
kuimarisha usimamizi wa fedha za umma, Serikali iliendelea kutekeleza programu
ya maboresho ya usimamizi wa fedha za umma katika Serikali Kuu na Serikali za
mitaa. Katika utekelezaji wa programu hiyo Serikali imeweka mtandao wa IFMS
katika Halmashauri 133. Aidha, Serikali imetoa mafunzo ya ulipaji kwa mfumo wa
malipo ya kibenki - TISS kwa watumishi wa kada ya Uhasibu katika
mikoa 20, Hazina ndogo zote, Ofisi ya Bunge, TAMISEMI na Ofisi ya Mrajisi wa
vyama vya Ushirika. Vilevile, Serikali imetoa mafunzo kwa Wahasibu wa
Wizara, Idara, Mikoa na Balozi zetu 32 katika kuandaa Hesabu za Serikali kwa
viwango vya Kimataifa (IPSAS – Accruals basis).
36.
Mheshimiwa Spika, kutokana na
maboresho hayo, usimamizi wa fedha katika Wizara, Idara, Taasisi, Mikoa na
Mamlaka ya Serikali za Mitaa unaendelea kuimarika. Hali hii inajidhiirisha
katika taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya mwaka
2010/11 ambapo Hati safi za ukaguzi kwa Wizara, Idara na Sekretarieti za Mikoa
zimeongezeka kutoka asilimia 71 hadi asilimia 85. Wakati Hati zenye shaka
zimepungua kutoka asilimia 26 mwaka wa fedha 2009/10 hadi asilimia 15 kwa mwaka
wa fedha 2010/11 na hapakuwepo na Hati zisizoridhisha ikilinganishwa na mwaka
2009/10 ambapo Hati hizo zilitolewa kwa Taasisi mbili.
37.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Balozi
zetu Hati safi zimeongezeka kutoka asilimia 71 mwaka 2009/10 na kufikia
asilimia 85 mwaka 2010/11 na hapakuwepo na Hati zisizoridhisha katika mwaka
2010/11. Aidha, kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa Hati safi
zimeongezeka kutoka asilimia 49 mwaka wa fedha 2009/10 hadi asilimia 54 mwaka
2010/11 na Hati zenye shaka zimepungua kutoka asilimia 64 mwaka 2009/10 na
kufikia asilimia 56 mwaka 2010/11.
38.
Mheshimiwa Spika,
katika mwaka 2011/12, Serikali imefungua akaunti sita kwa kila Halmashauri kwa
ajili ya uendeshaji wa majukumu yao. Akaunti hizo ni za Mapato; Amana; Matumizi
ya kawaida; Mishahara; Maendeleo; na Mfuko wa Barabara. Lengo la hatua hii ni
kupunguza gharama za uendeshaji, urasimu wa matumizi, ugumu wa kutoa taarifa za
matumizi, ulimbikizaji wa fedha kwenye akaunti bila kutumika kwa muda mrefu na
kudhibiti fedha zisitumike katika shughuli ambazo hazikuidhinishwa.
Mwenendo wa Matumizi
39.
Mheshimiwa Spika,
kwa upande wa matumizi, Serikali ilikadiria kutumia kiasi cha shilingi bilioni
13,525.9 katika mwaka wa fedha wa 2011/12. Mgawanyo wa matumizi ya Serikali
katika kipindi hiki ulikuwa kama ifuatavyo; kiasi cha shilingi bilioni 8,600.3
zilitengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi bilioni 4,925.6
zilikadiriwa kutumika kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.
Matumizi ya kawaida
40.
Mheshimiwa Spika, katika
kipindi cha Julai 2011 hadi Aprili 2012 matumizi ya kawaida
yamefikia shilingi bilioni 7,349.8 sawa na asilimia 85.5 ya makadirio ya mwaka
kama ilivyo katika ridhaa ya matumizi. Kati ya kiasi hicho, malipo ya mishahara
ya watumishi wa Serikali, Sekretarieti za Mikoa, Mamlaka ya Serikali za Mitaa,
Taasisi na Mashirika ya Umma yalikuwa shilingi bilioni 2,760.5 sawa na asilimia
84.4 ya lengo la mwaka la shilingi bilioni 3,270.3. Malipo
ya riba kwa mikopo ya ndani na nje yalikuwa shilingi bilioni 316.1 sawa na
asilimia 102.4 ya makadirio ya shilingi bilioni 308.7 kwa mwaka. Malipo ya
mikopo ya nje yalikuwa shilingi bilioni 57.3 sawa na asilimia 85.7 ya makadirio
kwa mwaka. Serikali ilitumia shilingi bilioni 526 kwa ajili ya kulipia dhamana
za Serikali za muda mfupi na Hatifungani za Serikali zilizoiva. Serikali
imeendelea kutoa kipaumbele katika kulipa madeni kwa wakati ili kuepuka
malimbikizo ya riba.
41.
Mheshimiwa
Spika, matumizi mengineyo katika Wizara, Idara,
Taasisi za Serikali, Mikoa na Halmashauri yalifikia shilingi bilioni 2,384.9
ikiwa ni asilimia 72.8 ya makadirio ya shilingi bilioni 3,275.1 kwa mwaka. Kati
ya matumizi mengineyo, kiasi cha shilingi bilioni 284.1 zilitumika kwa ajili ya
mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu ikiwa ni asilimia 89 ya bajeti ya mwaka ya
shilingi bilioni 317.4, na hivyo kunufaisha jumla ya wanafunzi 93,176.
Kadhalika, Serikali ililipa kiasi cha shilingi bilioni 44.0 za madai ya walimu
wa shule za msingi na sekondari yaliyohakikiwa na Mkaguzi Mkuu wa Ndani.
Matumizi ya Maendeleo
42.
Mheshimiwa Spika,
kwa upande wa Matumizi ya Maendeleo kiasi cha shilingi bilioni 2,657.2
ziligharamia miradi ya maendeleo ikilinganishwa na makadirio ya mwaka ya
kutumia shilingi bilioni 4,924.6. Fedha za ndani zilikuwa shilingi bilioni
1,201.6 ikilinganishwa na makadirio ya mwaka ya shilingi bilioni 1,871.5 sawa
na asilimia 64.2. Upungufu huu umetokana na kuchelewa kupatikana kwa wakati kwa
mikopo ya nje yenye masharti ya kibiashara. Jumla ya shilingi bilioni 663.8
ziligharamia miradi ya miundombinu, kati ya hizo shilingi bilioni 296
zilitumika kwenye miradi ya umeme na shilingi bilioni 367.8 kwenye miradi ya
barabara. Matumizi ya maendeleo yaliyogharamiwa kwa fedha za nje yalikuwa
shilingi bilioni 1,450.4 ikilinganishwa na makadirio ya shilingi bilioni
3,054.1 sawa na asilimia 47.
Vitambulisho vya Taifa na Anwani za Makazi
43.
Mheshimiwa Spika, Serikali
imeendelea
na azma yake ya kutekeleza mradi wa Vitambulisho vya Taifa ambavyo vitasaidia,
pamoja na mambo mengine, kurahisisha upatikanaji wa huduma mbalimbali ikiwa ni
pamoja na huduma za kifedha. Mradi huu unaenda sambamba na uanzishwaji wa
anwani za makazi. Vitambulisho hivyo vitaanza kutolewa katika robo ya kwanza ya
mwaka 2012/13 kwa Zanzibar na Mkoa wa Dar es Salaam.
Sensa ya Watu na Makazi na Utafiti Kuhusu Hali
ya Umaskini
44.
Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu
wa Sensa ya Watu na Makazi Serikali imeendelea kugharamia maandalizi ya Sensa
ya Watu na Makazi, ambapo utekelezaji umefikia asilimia 95. Hadi sasa Serikali
imetumia shilingi bilioni 23.6 kugharamia maandalizi ya zoezi la Sensa. Sensa
hiyo imepangwa kufanyika tarehe 26 Agosti 2012. Aidha, Serikali iliendelea
kugharamia utafiti wa mapato na matumizi katika kaya. Utafiti huu ulianza mwezi
Oktoba 2011, na unatarajiwa kukamilika mwezi Septemba 2012 na matokeo
yanatarajiwa kutoka mwezi Julai 2013. Utafiti huu utatoa picha halisi ya hali
ya umaskini, hususan wa kipato tangu mwaka 2007 hadi mwaka 2012. Hii itasaidia
kutambua mwenendo wa umaskini wa kipato na sababu zilizopelekea mwenendo huo.
Utekelezaji
wa Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini (MKUKUTA II)
45.
Mheshimiwa Spika,
katika kipindi cha mwaka 2011/12, serikali iliendelea
kutekeleza MKUKUTA awamu ya pili unaojielekeza katika maeneo ya kukuza uchumi
na kupunguza umaskini wa kipato, kuboresha maisha na ustawi wa jamii, na
utawala bora na uwajibikaji sambamba na Melengo ya Maendeleo ya Milenia. Ili
kufikia matokeo tarajiwa katika kila eneo, sekta kadhaa huchangia katika
utekelezaji kupitia sera, mikakati na mipango ya kisekta. Kwa
mantiki hiyo, utekelezaji wa MKUKUTA II unahitaji ushirikiano wa sekta
mbalimbali za uchumi katika hatua ya upangaji na utekelezaji.
46.
Mheshimiwa Spika,
MKUKUTA ni mkakati unaoziweka pamoja juhudi za Serikali na wadau
mbalimbali katika kupambana na umaskini. Aidha, umaskini ni suala pana
linalojumuisha umaskini wa kipato na usio wa kipato. Ni kweli kuwa umaskini wa
kipato umekuwa ukipungua kwa kasi ndogo. Hata hivyo, Serikali inachukua hatua
mbalimbali za kupunguza umaskini kwa kujenga mazingira bora ili wananchi
washiriki kikamilifu katika shughuli za uchumi, ikiwa ni pamoja na kuwekeza
katika elimu, afya, miundombinu na sekta ya fedha.
47.
Mheshimiwa Spika,
pamoja na changamoto zilizojitokeza, hususan mtikisiko wa uchumi duniani,
uchumi uliendelea kukua kwa kiwango cha kuridhisha. Kiwango cha ukuaji wa
uchumi kwa mwaka 2011, kilikuwa asilimia 6.4 ikilinganishwa na asilimia 7.0
mwaka 2010. Aidha, pato la wastani la Mtanzania limeongezeka kutoka shilingi
770,464 kwa mwaka 2010 hadi shilingi 869,436 kwa mwaka 2011. Kwa wastani,
ongezeko hili limeongeza uwezo wa wananchi kupata huduma bora ikiwa ni pamoja
na nyumba bora, simu za mkononi, pikipiki na usafiri wa baiskeli.
48.
Mheshimiwa Spika,
Serikali iliendelea kutekeleza programu mbalimbali za huduma ya jamii kwa lengo
la kuboresha maisha na ustawi wa jamii. Matokeo ya utekelezaji wa programu hizo
zinaonesha mabadiliko chanya. Katika sekta ya elimu, viwango vya uandikishaji
na kumaliza katika ngazi zote za elimu vinaridhisha. Mfano, kiwango cha
uandikishwaji katika elimu ya msingi, kilikuwa asilimia 94 na katika elimu ya
sekondari ni asilimia 35 kwa mwaka 2011. Huduma za afya kwa mtoto na mama
zinaendelea kuimarika kutokana na utekelezaji wa mpango wa afya ya mtoto na
mama. Aidha, hali ya upatikanaji wa huduma ya maji safi
na salama imeendelea kuimarika kutokana na utekelezaji wa programu ya sekta ya
maji iliyoanza mwaka 2007.
49.
Mheshimiwa Spika,
katika kudumisha utawala bora na uwajibikaji, Serikali iliendelea kuchukua
hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na: kuimarisha sekta ya sheria kwa kuongeza
idadi ya mahakimu wa Mahakama za mwanzo; kuimarisha mfumo wa sheria na haki za
binadamu; kuhamasisha umma kuhusu haki za binadamu na wajibu wa jamii; na
kushiriki katika mpango wa nchi za Afrika kujitathmini zenyewe katika masuala
ya utawala bora. Aidha, Serikali imeendelea kuimarisha mifumo ya usimamizi wa
fedha za umma, kwa kuimarisha ofisi za ukaguzi katika wizara, mikoa na Mamlaka
za Serikali za Mitaa.
Sekta ya Fedha
50.
Mheshimiwa Spika, Serikali imefanya mageuzi mbalimbali
katika sekta ya fedha ili kuhakikisha kwamba inachangia kikamilifu katika
shughuli za kiuchumi na kukuza Pato la Taifa. Mageuzi haya yameleta mafanikio
makubwa.Hadi kufika mwezi Aprili mwaka 2012 idadi ya benki imeongezeka na
kufikia 49 kutoka benki 43 Aprili mwaka 2011. Kadi za simu za mkononi
zinazotumika kutoa huduma za kifedha zimefikia 21,184,808 mwaka 2011 kutoka
10,663,623 mwaka 2010. Aidha, idadi ya Taasisi ndogo ndogo za kifedha
zimefikia 150 mwaka 2011.
51.
Mheshimiwa Spika,
Serikali
iliendelea kutoa Mikopo ya kilimo kupitia dirisha la Kilimo lililopo katika
Benki ya Rasilimali Tanzania. Hadi kufikia Machi, 2012 jumla ya mikopo 81 yenye
thamani ya shilingi bilioni 22.9 ilitolewa, kati ya mikopo hiyo, 42 ni ya
SACCOS, 32 ni kwa ajili ya makampuni na 7 kwa Taasisi ndogondogo za fedha
(MFIs). Mikopo iliyotolewa kwa MFIs na SACCOS ilitumika kukopesha miradi mingi
ya wakulima wadogo wadogo vijijini. Aidha, Serikali imetoa shilingi bilioni 30
kwa ajili ya mtaji wa Benki ya Kilimo.
52.
Mheshimiwa Spika, Serikali iliendelea
na utekelezaji wa programu ya mageuzi na maboresho ya Ushirika nchini ili
kuimarisha vyama vikuu vya ushirika na kuviwezesha kutoa huduma za kifedha kwa
wananchi wengi zaidi hususan waliopo vijijini. Mwaka 2011, idadi ya Vyama vya
Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS) iliongezeka na kufikia 5,346 kutoka vyama
5,314 mwaka 2010. Vile vile, idadi ya wanachama iliongezeka kwa asilimia 5.7 na
kufikia wanachama 970,655 kutoka wanachama 917,889 mwaka 2010. Aidha, Hisa,
Akiba na Amana za wanachama ziliongezeka kutoka shilingi bilioni 236.8 mwaka
2010 hadi shilingi bilioni 399.0 mwaka 2011, sawa na ongezeko la asilimia 68.5.
Mikopo iliyotolewa kwa wanachama iliongezeka kutoka shilingi bilioni 539.2
mwaka 2010 hadi shilingi bilioni 627.2 mwaka 2011, sawa na ongezeko la asilimia
16.3.
53.
Mheshimiwa Spika,
hadi
kufikia Machi 2012, mikopo kwa sekta binafsi iliongezeka kwa asilimia 21.9
ikilinganishwa na asilimia 23.3 Machi 2011. Ongezeko hili linaenda sambamba na
kuongezeka kwa rasilimali za fedha za ndani kwenye benki pamoja na kupungua kwa
ukuaji wa rasilimali za fedha za kigeni kwenye benki. Sehemu kubwa ya mikopo
hii ilielekezwa katika shughuli binafsi asilimia 21.9; biashara asilimia 19.9;
uzalishaji bidhaa viwandani asilimia 11.9; kilimo asilimia 11.8; na usafiri na
mawasiliano asilimia 7.9.
54.
Mheshimiwa Spika,
ili kuongeza upatikanaji wa mikopo, Serikali imepata Mshauri Mwelekezi kwa
ajili ya kuanzisha taasisi ya kuratibu taarifa za wakopaji (Credit Rerefence
Bureau) na mfumo wa kuhifadhi taarifa za wakopaji (Credit Reference Databank).
Mshauri mwelekezi ameanza zoezi la kuweka mitambo na kutoa mafunzo kwa
watumiaji. Aidha, Serikali imeboresha mazingira ya upatikanaji wa mikopo ya
muda mrefu na kati kwa ajili ya nyumba, Kilimo na uwekezaji ambapo kanuni
za taasisi za fedha za maendeleo ziliandaliwa na kuchapishwa katika
Gazeti la Serikali la Machi 2012.
55.
Mheshimiwa Spika,
katika
mwaka 2011/12, Serikali imeendelea kufanya maboresho katika sekta ya Hifadhi ya
Jamii kwa kufanya tathmini ya uwekezaji wa mifuko, uhai wa mifuko, pamoja na
kuandaa mwongozo za uwekezaji wa mifuko hiyo. Aidha, Serikali imefanya
marekebisho ya Sheria za Mifuko yote pamoja na Mamlaka ya Usimamiaji wa
Shughuli za Mifuko (SSRA) ili kuboresha usimamizi wa mifuko hiyo.
Ubia Kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi
56.
Mheshimiwa Spika, Bunge lako tukufu
lilipitisha sheria mpya ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi ya mwaka
2010 ili kutoa fursa kwa sekta binafsi kushiriki katika ujenzi wa miundombinu
na kuiendesha kwa lengo la kutoa huduma bora za kijamii na kiuchumi kwa
wananchi. Katika mwaka 2011/12, Serikali imefanya maandalizi ya utekelezaji wa
Sera ya Ubia ikiwa ni pamoja na kuanzisha madawati ya PPP kwa kila Wizara na
kuandaa miongozo itakayotumika kuchambua na kuidhinisha miradi ya Ubia kwa
mujibu wa sheria. Aidha, Serikali imeanza hatua za awali kubaini miradi
inayoweza kutekelezwa kwa utaratibu wa Ubia kwa mujibu wa sheria.
57.
Mheshimiwa Spika, dhana ya Ubia kati ya
Sekta ya Umma na Sekta Binafsi inatekelezwa kwa kutumia sheria mbili – Sheria
ya Ubia ya mwaka 2010 na Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2004
iliyorekebishwa mwaka 2011. Sababu za kurekebisha Sheria ya Ununuzi wa Umma
pamoja na mambo mengine ni kuingiza vifungu vinavyowezesha Taasisi za Serikali
kupata Wabia makini wa uwekezaji katika miradi ya Umma kwa njia zilizo wazi.
Aidha, katika mwaka 2012/13, Serikali itakamilisha Kanuni za Sheria ya Ununuzi
wa Umma ambazo zinazingatia mazingira ya kipekee ya Sheria ya Ubia ambayo
inawezesha kupata Wabia walio tayari kuwekeza katika miradi husika. Serikali
itahakikisha kanuni na taratibu zote za kuidhinisha na kusimamia miradi ya ubia
zinazingatiwa.
58.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha
2012/13, Serikali itatoa mafunzo ya uelewa wa dhana ya Ubia kati ya Sekta ya
Umma na Sekta binafsi kwa watumishi wa Wizara, Idara Zinazojitegemea, Taasisi
za Serikali, na Halmashauri zote. Aidha, Serikali itachagua miradi michache ya
kuanza nayo ili kupata uzoefu wa uendeshaji wa miradi hiyo. Maeneo
tunayotarajia kuanza nayo ni barabara, reli, bandari, viwanja vya ndege, maji
pamoja na ujenzi wa ofisi.
59.
Mheshimiwa Spika, Napenda kutumia fursa
hii kuziomba Wizara, Idara zinazojitegemea, Mashirika ya Umma, na Mamlaka ya
Serikali za Mitaa kuhamasisha Sekta Binafsi kushiriki katika utekelezaji wa
miradi mbalimbali kwa kuzingatia taratibu na kanuni zilizowekwa kwa mujibu wa
Sheria.
Usimamizi wa Deni la Taifa
60.
Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza
azma yake ya kuboresha miundombinu ya kimkakati, Serikali imeendelea kukopa
kutoka nje na ndani ya nchi ili kugharamia miradi mbali mbali ya maendeleo.
Hadi mwishoni mwa Machi 2012, deni la taifa lilikuwa shilingi bilioni 20,276.6
ikilinganishwa na deni la shilingi bilioni 17,578.9 Machi 2011 ikiwa ni sawa na
ongezeko la asilimia 15.4. Kati ya hizo, shilingi bilioni 15.306.9 zilikuwa ni
deni la nje na shilingi bilioni 4,969.7 ni deni la ndani. Kati ya kiasi
cha deni la nje, shilingi bilioni 12,342.5 zilikuwa ni deni la umma na kiasi
kilichobaki cha shilingi bilioni 2,964.4 ni deni la sekta binafsi. Aidha, hadi
kufikia Machi 2012, deni la ndani la Serikali lilifikia shilingi bilioni 4,969.7
ikilinganishwa na shilingi bilioni 4,496.5 mwezi Machi, 2011, sawa na ongezeko
la asilimia 10.5. Sababu kubwa ya kuongezeka kwa deni la taifa ni mikopo mipya
kwa ajili ya kugharimia miradi ya maendeleo na utumiaji wa dhamana za muda
mfupi za Serikali kwa ajili ya kudhibiti mfumuko wa bei katika uchumi na
kushuka kwa thamani ya shilingi kuliongeza deni la nje.
61.
Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha
kuwa Deni la Taifa linasimamiwa vizuri, mwezi Februari, 2012, Serikali ilifanya
tathmini ya uhimilivu wa deni (Debt Sustainability Analysis) likijumuisha
dhamana zinazotolewa na Serikali kwa Wizara, Mashirika na Taasisi za Umma
ambapo matokeo ya tathmini hiyo yanaonesha kuwa Deni la Taifa linahimilika.
Usimamizi wa Mashirika ya Umma
62.
Mheshimiwa Spika, katika
kuhakikisha Taasisi, Wakala na Mashirika ya umma yanatekeleza majukumu yao,
Serikali imetoa Waraka Na.1 wa mwaka 2012 unaoelekeza Wizara mama na
Bodi za Wakurugenzi kuingia katika mikataba ya utendaji, Waraka huo umeanza
kutumika Januari, 2012. Aidha, ukaguzi wa kiutendaji (Management Audit) katika
Taasisi za Serikali umefanyika kwa baadhi ya Taasisi na Mashirika ya umma kwa
kuangalia uzingatiaji wa kanuni, Sheria na miongozo mbalimbali inayotolewa na
Serikali ikiwa ni pamoja na uwajibikaji na utawala bora, matumizi ya fedha
na taratibu za ajira. Zoezi hili ni endelevu na linalenga kuboresha
uendeshaji wa Mashirika na Taasisi za Serikali. Kadhalika, Serikali imefanya
uhakiki wa mashirika 170 yaliyobinafsishwa. Kati ya hayo, mashirika 41 yalikutwa
yanajiendesha kwa faida, mashirika 66 yanajiendesha kwa hasara na mashirika 63
yalikuwa muflisi. Kwa yale ambayo yanaendeshwa kwa hasara yatawekwa chini ya
mfilisi kwa lengo la kuyachambua na kupendekeza hatua za kuchuliwa. Aidha, kwa
yale yaliyokuwa muflisi hatua za kuyafilisi zinaendelea.
III. BAJETI YA MWAKA
2012/13
63.
Mheshimiwa Spika, Bajeti
ya mwaka 2012/13 itazingatia vipaumbele vilivyoainishwa kwenye Mpango wa
Maendeleo wa mwaka 2012/13; Awamu ya Pili ya Mkakati wa Kukuza Uchumi na
Kupunguza Umasikini (MKUKUTA II); Malengo ya Maendeleo ya Milenia 2015; Ilani
ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010 na program za maboresho katika sekta ya umma.
Lengo likiwa ni kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025.
64.
Mheshimiwa Spika, pamoja
na miongozo hiyo, Bajeti hii inazingatia pia changamoto zilizojitokeza wakati
wa utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2011/12. Changamoto hizo ni pamoja na
upatikanaji wa umeme wa uhakika; kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la
Dunia; uhaba wa chakula katika baadhi ya maeneo; kupanda kwa bei za bidhaa na
huduma; kutopatikana kwa wakati fedha za kugharamia miradi ya maendeleo
kulikosababishwa na masharti magumu na urasimu kwa mikopo ya kibiashara; na
kuongezeka kwa malimbikizo ya madeni ya ndani, hususan ya wazabuni, wakandarasi
na watumishi. Mambo mengine yaliyozingatiwa ni pamoja na mwenendo
wa uchumi wa dunia na makubaliano ya kikanda na kimataifa. Serikali imepanga
hatua mbalimbali za kuchukua kukabiliana na changamoto hizo kama nitakavyoeleza
hapo baadae.
Shabaha na Malengo ya Bajeti ya mwaka 2012/13
65.
Mheshimiwa Spika, Bajeti ya mwaka
2012/13, imejielekeza katika kufikia Shabaha na malengo yafuatayo:
i.
Kukuza
Pato halisi la Taifa kwa asilimia 6.8 mwaka 2012
ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 6.4 mwaka 2011;
ii.
Kuimarisha
miundombinu ya uchumi, ikijumuisha umeme, barabara, reli na bandari;
iii.
Kuongeza
upatikanaji wa huduma za kifedha;
iv.
Kuongezeka
kwa mapato ya ndani yatakayofikia uwiano na Pato la Taifa wa asilimia 18
kwa mwaka 2012/13 kulinganisha na mwelekeo wa asilimia 16.9 mwaka 2011/12;
v.
Kuendelea
kudhibiti mfumuko wa bei ili urudi kwenye viwango vya tarakimu moja;
vi.
Kuwa
na kiwango tengemavu cha ubadilishaji wa fedha kitakachotokana na mwenendo wa
soko la fedha;
vii.
Kukua
kwa mikopo kwa sekta binafsi kwa kiwango cha asilimia 20 ya Pato la Taifa
mwishoni mwa Juni 2013 sambamba na jitihada za kudhibiti mfumuko wa bei;
viii.
Kuwa
na akiba ya fedha za kigeni kwa kiwango cha kukidhi mahitaji ya uagizaji wa
bidhaa na huduma kutoka nje kwa kipindi kisichopungua miezi minne na nusu;
ix.
Kuimarisha
utaratibu wa ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP) ili kupanua fursa za
kuchangia utekelezaji wa miradi ya maendeleo;
x.
Kuboresha
mazingira ya wafanya biashara wadogo na wakati;
xi.
Kulinda
na kuendeleza mafanikio yaliyopatikana katika Sekta za huduma za jamii;
xii.
Kuimarisha
utawala bora na uwajibikaji; na
xiii.
Kujenga
uwezo wa nchi kukabiliana na misukosuko ya kiuchumi na kifedha pamoja na
kushiriki kwa ufanisi katika ushirikiano kikanda na kimataifa.
Misingi ya Bajeti ya Serikali kwa Kipindi cha mwaka
2012/13
66.
Mheshimiwa Spika; ili kufikia malengo
yaliyoainishwa hapo juu, misingi ya Bajeti ya Serikali kwa
kipindi cha mwaka 2012/13 ni hii ifuatayo:
i.
Kuendelea
kuimarika kwa utengamavu wa viashiria vya uchumi jumla na maendeleo ya jamii;
ii.
Kuwepo
kwa nishati ya umeme wa uhakika na kuhamasisha matumizi ya gesi asilia;
iii.
Kuimarika
kwa utekelezaji wa Sera za Fedha na Bajeti;
iv.
Kuendelea
kuimarika kwa mahusiano na Washirika wa Maendeleo;
v.
Kuendelea
kutekeleza sera ya ugatuaji wa madaraka kwa wananchi;
vi.
Kuendelea
kutekeleza maboresho katika sekta ya umma ikiwa ni pamoja na kuendelea
kuimarika kwa usimamizi wa fedha za umma;na
vii.
Kuendelea
kuboresha mazingira ya biashara pamoja na kuongezeka kwa tija na fursa za
uwekezaji.
Sera za Mapato
67.
Mheshimiwa Spika,
Serikali itaendelea na azma yake ya kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani
kwa kuchukua hatua mbalimbali katika maeneo ya mapato yatokanayo na kodi na
yasiyotokana na kodi; na kupanua wigo wa makusanyo. Aidha, Serikali itaendelea
kuimarisha taratibu za kukusanya mapato pamoja na kupunguza misamaha ya kodi
ili kuweza kugharamia kwa kiwango kikubwa matumizi ya kawaida kwa kutumia
mapato ya ndani. Sera za mapato zitakazozingatiwa
kwenye Bajeti ya mwaka 2012/13 ni pamoja na;
i.
kuboresha
mifumo ya ukusanyaji na usimamiaji wa mapato yasiyo ya kodi
kwa kupitia upya mfumo wa utoaji stakabadhi na leseni, pamoja na kuboresha
viwango vya kubakiza maduhuli kwa Wizara, Idara na Taasisi za Serikali;
ii.
kupanua wigo wa kodi kwa kuendelea
kurasimisha sekta isiyo rasmi ili iingie kwenye mfumo wa kodi;
iii.
kuendelea kufanya mapitio ya sheria za
Wakala/Taasisi za Umma zinazokusanya maduhuli ili ziweze kuchangia zaidi kwenye
Mfuko Mkuu wa Serikali;
iv.
kuendelea kufanya mapitio ya sheria mbalimbali
zinazotoa misamaha ya kodi kwa lengo la kudhibiti na kupunguza misamaha
hiyo;
v.
Kupitia upya mfumo wa ukusanyaji wa kodi ya majengo
katika majiji, manispaa, miji, wilaya na miji midogo ili kuuboresha zaidi;
vi.
kufanya mapitio ya vyanzo vya mapato na mfumo wa
ukusanyaji katika Serikali za Mitaa ili kuongeza mapato; na
vii.
Kujenga uwezo wa Wizara ya Fedha, Wizara ya Nishati na
Madini, Shirika la Maendeleo la Petroli Tanzania, Mamlaka ya Mapato Tanzania,
Wakala wa Ukaguzi wa Madini ili kusimamia ukusanyaji wa mapato katika maeneo ya
madini, gesi na petroli.
Hatua za Kuboresha
Uzalishaji na Huduma
68.
Mheshimiwa Spika, Serikali
imepokea mapendekezo kutoka kwa wadau mbalimbali wakiwemo waheshimiwa wabunge
kuhusu haja ya kuboresha mazingira ya uzalishaji katika sekta za Uvuvi,
Viwanda, Kilimo, Mifugo na Utalii. Hatua ambazo Serikali imepanga kuchukuwa ni
pamoja na:
i.
Kupitia upya vivutio kwa sekta ya viwanda vya ndani
vinavyotumia malighafi za ndani vikiwemo viwanda vya nguo na mafuta ya kula;
ii.
Kutafuta utaratibu mzuri wa kubainisha vipuri vya
mashine na mitambo inayosamehewa kodi ili kuondoa usumbufu wanaoupata
waagizaji;
iii.
Kupitia upya viwango vya kodi katika sekta ya Kilimo
na Uvuvi kwa lengo la kuviwianisha na kupunguzwa;
iv.
Kupitia upya maudhui na viwango vya Tozo ya Kuendeleza
Stadi (Skills Development Levy) na Leseni ya Magari (Motor Vehicle Licence).
Kwa kufanya hivyo, Serikali inalenga katika kupanua wigo wa kodi, kuwapunguzia
mzigo waajiri na kupanua ajira hapa nchini. Aidha, mapitio ya Leseni za Magari
yatazingatia kurejea madhumuni ya kuanzishwa kwa leseni hiyo; na
v.
Kufanya mapitio ya Sheria ya VAT kwa lengo la
kuibadili kwa kuzingatia uzoefu wa kimataifa “Best Practice”.
69.
Mheshimiwa Spika,
Mamlaka za Serikali za Mitaa zinahimizwa kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani
kwa kuzingatia fursa zilizopo. Aidha, OWM – TAMISEMI kwa kushirikiana na
Shirika la Misaada na Utaalamu la Ujerumani – GIZ watakamilisha na kusambaza
kwenye Halmashauri mfumo wa kompyuta wa utunzaji kumbukumbu za mali na majengo
(Integrated Property Rating Information Management System - IPRIMS) ili
kuboresha ukusanyaji wa mapato hususan kodi ya majengo. Natoa rai kwa
Waheshimiwa Wabunge wote pamoja na viongozi wengine wa ngazi mbalimbali kuweka
msukumo utakaowezesha Halmashauri kukusanya kikamilifu kodi ya majengo pamoja
na mapato mengine ili kuziongezea uwezo wa kuhudumia wananchi na kuwaletea
maendeleo endelevu.
70.
Mheshimiwa Spika,
kwa kuzingatia sera za mapato zilizoainishwa hapo juu,
Serikali inalenga kukusanya mapato ya ndani (bila kujumuisha Halmashauri)
shilingi bilioni 8,714.7 sawa na asilimia 18 ya Pato la Taifa. Kati ya kiwango
hicho, mapato ya kodi shilingi bilioni 7,080.1 na mapato yasiyo ya kodi shilingi
bilioni 644.6. Mapato yanayotokana na vyanzo vya Halmashauri shilingi bilioni
362.2 sawa na asilimia 0.7 ya Pato la Taifa.
Mikopo ya Ndani
71.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea
na utaratibu wake wa kukopa katika soko la ndani la fedha kwa ajili ya
kugharamia miradi ya maendeleo na kulipia hatifungani za Serikali na dhamana za
Serikali za muda mfupi zinazoiva. Katika mwaka 2012/13, Serikali inakusudia
kukopa kiasi cha shilingi bilioni 1,632 kutoka soko la fedha la ndani. Kati ya
kiasi hicho, shilingi bilioni 483.9 sawa na asilimia moja ya Pato la Taifa ni
kwa ajili ya kugharimia miradi ya maendeleo na kiasi cha shilingi bilioni
1,148.1 ni kwa ajili ya kulipia hatifungani za Serikali na dhamana za Serikali
za muda mfupi zinazoiva. Kiwango hiki kimezingatia viashiria vya kiuchumi
pamoja na kuhakikisha kuwa Taasisi za Fedha zinaendelea kutoa mikopo kwa Sekta
binafsi ili kuchochea ukuaji wa uchumi.
Misaada na Mikopo Mipya yenye Masharti Nafuu
72.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea
kushirikiana na Washirika wa Maendeleo ili kuhakikisha Misaada na mikopo
inapatikana kwa wakati na kuchangia katika utekelezaji wa bajeti ya Serikali.
Katika bajeti ya mwaka 2012/13 serikali inatarajia kupata kiasi cha shilingi
bilioni 3,156.7 kutokana na misaada na mikopo yenye masharti nafuu. Kati ya
fedha hizo, Misaada na mikopo ya kibajeti ni shilingi bilioni 842, sawa na Dola
za Marekani milioni 495. Misaada na mikopo kwa ajili ya miradi ya maendeleo
ikijumuisha mifuko ya kisekta inatarajiwa kuwa shilingi bilioni 2,314.2.
73.
Mheshimiwa Spika, pamoja na misukosuko
ya kiuchumi na majanga ya kiasili iliyozikumba nchi Wahisani, bado zimeendelea
kutoa misaada na mikopo kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu. Napenda kuwatambua
washirika wetu wa maendeleo ambao ni: Uingereza, Norway, Canada, Marekani,
Uholanzi, Ubelgiji, China, Finland, Ufaransa, Ujerumani, Ireland, Japani, Korea
ya Kusini, Denmark, Hispania, Sweden, Uswisi, India, Italia, Benki ya Dunia,
Benki ya Maendeleo ya Afrika, Umoja wa Ulaya, Global Funds, Shirika la Fedha la
Kimataifa (IMF), BADEA, Kuwait Fund, Nordic Fund, Opec Fund, Saudi Fund, na
Mashirika ya Umoja wa Mataifa. Tunawashukuru Sana.
Mikopo ya nje yenye Masharti ya Kibiashara
74.
Mheshimiwa Spika,
sera ya Serikali ni kutafuta mikopo nafuu kutoka mashirika na nchi wahisani kwa
ajili ya kugharamia Bajeti yake ya maendeleo. Hata hivyo, kwa kuzingaita
mahitaji makubwa ya kuendeleza miradi ya miundombinu kwa mwaka 2012/13,
Serikali inatarajia kupata kutoka nje mikopo yenye masharti ya kibiashara kiasi
cha shilingi bilioni 1,254.1 sawa na Dola za Marekani milioni 749. Fedha hizi
zitatumika kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo kama ilivyoainishwa kwenye
Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2012/13 ikijumuisha mchango wa Serikali
(counterpart fund) katika ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es
Salaam, mradi wa maji wa Ruvu chini na ujenzi wa barabara. Uamuzi wa kuendelea
kukopa kwa masharti nafuu na ya kibiashara unazingatia uhimilivu wa Deni la
Taifa uliopo.
Sera
za Matumizi
75.
Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2012/13, sera za matumizi zitazingatia yafuatayo:
i.
Matumizi yataendelea kuzingatia mapato halisi
yanayopatikana;
ii.
Nakisi ya bajeti haitazidi asilimia 5.5 ya Pato la
Taifa, ikijumuisha ruzuku;
iii.
Mafungu yataendea kuzingatia viwango vya matumizi
vitakavyoidhinishwa na Bunge;
iv.
Maafisa Masuuli wataendelea kuzingatia Sheria ya Fedha
na ya Ununuzi wa Umma; na
v.
Serikali inaendelea kukusanya madeni yote kwa lengo la
kuyahakiki na kuyapangia utaratibu wa kuyalipa.
Matumizi
ya Kawaida
76.
Mheshimiwa Spika,
Sera za matumizi ya kawaida kwa mwaka 2012/13
zinalenga pamoja na mambo mengine katika kugharamia mishahara; madeni ya mikopo
ya ndani na nje; uboreshaji wa huduma za kiuchumi na maendeleo ya jamii; mikopo
ya wanafunzi wa elimu ya juu; mitihani ya shule za msingi na sekondari; ununuzi
na usambazaji wa dawa; mahitaji ya Tume ya Kuratibu Mabadiliko ya Katiba;
matengenezo ya mali ya Serikali; ununuzi wa chakula cha hifadhi; mahitaji ya
kawaida kwenye miradi iliyokamilika; pamoja na kuendelea kulipa madai mbalimbali
ya watumishi na wazabuni.
77.
Mheshimiwa Spika,
ili kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa mikopo ya
muda mrefu, kilimo kisichokuwa na tija na ukosefu wa ajira, Serikali imetenga
fedha katika maeneo yafuatayo: Shilingi bilioni 30 kwa ajili ya Benki ya
Rasilimali; shilingi bilioni 40 kwa Benki ya Maendeleo ya Kilimo na hivyo
kufikisha mtaji wa shilingi bilioni 100. Aidha, shilingi bilioni 7.5 zimetengwa
kwa ajili ya kurejesha mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa kwa mujibu wa sheria,
ambapo katika awamu ya kwanza vijana 5,000 wanatarajiwa kujiunga. Vilevile,
Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 70.7 katika maeneo mapya ikiwa ni
Mikoa, Wilaya na Halmashauri kugharamia matumizi ya kawaida na maendeleo.
Matumizi ya Maendeleo
78.
Mheshimiwa Spika, katika
hotuba ya Hali ya Uchumi kwa mwaka 2011 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa
mwaka 2012/13, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu Mhe. Stephen
Masatu Wasira, aliainisha miradi ya kitaifa ya kimkakati pamoja na miradi katika
maeneo muhimu ya ukuaji wa uchumi. Bajeti hii itazingatia vipaumbele hivyo:
a)
Miundombinu
i.
umeme - mkazo utawekwa
katika upatikanaji wa umeme wa kuhakika kwa kuongeza uzalishaji, usafirishaji
na usambazaji ambapo jumla shilingi bilioni 498.9 zimetengwa kwa ajili
hiyo. Aidha, Serikali itatekeleza mradi wa ujenzi wa Bomba la gesi kutoka
Mtwara hadi Dar es Salaam kwa mkopo kutoka Benki ya Exim ya China wenye thamani
ya Dola za Marekani milioni 1,225.3 utakaosimamiwa na TPDC.
ii.
usafirishaji na uchukuzi – uimarishaji
wa reli ya kati ikijumuisha ukarabati wa injini na mabehewa ya treni. Kwa
upande wa barabara, miradi inayopewa kipaumbele ni pamoja na barabara zenye
kufungua fursa za kiuchumi. Katika usafiri wa anga na majini, miradi
itakayotekelezwa ni pamoja na ujenzi na ukarabati wa viwanja vya ndege na
uendelezaji wa gati ya Ziwa Tanganyika. Jumla ya shilingi bilioni 1,382.9
zimetengwa katika eneo hili.
iii
maji safi na salama - kuongeza upatikanaji wa
maji safi na salama mijini na vijijini.
Kiasi cha shilingi bilioni 568.8 kimetengwa.
iv
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA)
– kuimarisha mawasiliano kwa kutumia
TEHAMA ili kuboresha upatikanaji wa huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na
upatikanaji wa taarifa za masoko ya ndani na nje ya nchi; ukusanyaji wa
mapato; huduma za afya; elimu; huduma za kifedha; n.k. Jumla ya shilingi
bilioni 4 zimetengwa katika eneo hili.
b)
Kilimo, Uvuvi na Ufugaji
79.
Mheshimiwa Spika,
kwa kushirikiana na sekta binafsi, Serikali itawekeza katika
kilimo cha mpunga na miwa katika mabonde makuu ya Wami, Ruvu, Kilombero na
Malagarasi pamoja na kuongeza tija na thamani, kubadilisha mfumo wa kilimo na
kukuza kilimo cha misitu. Hii ni pamoja na kuendeleza shughuli za ufugaji
na uvuvi ili ziwe na tija kwa kuboresha mazingira ya uwekezaji; kwa kufanya
hivyo kutapunguza umaskini wa kipato.
80.
Mheshimiwa Spika, katika kuongeza
uzalishaji wa mazao ya chakula pamoja na kuhakikisha usalama wa chakula,
Serikali itaimarisha utekelezaji wa dhana ya Kilimo Kwanza kwa
kuhakikisha kwamba nguzo zake zote zinaendelea kuzingatiwa; kuhakikisha kwamba
walengwa wanapata pembejeo kwa wakati; Maafisa ugani kutakiwa kuwa na mashamba
yao ya mfano (mashamba darasa) ili kuwaelimisha wakulima kilimo cha kisasa; kuongeza
msukumo kwenye kilimo cha umwagiliaji ili wakulima waweze kufanya shughuli zao
za kilimo katika misimu yote badala ya kutegemea mvua;Kuimarisha masoko ya
mazao kupitia Bodi ya Mazao Mchanganyiko ambayo imeshaanza shughuli zake; na
Mikoa kutakiwa kuendelea kutenga ardhi na vijiji kutakiwa kupima na
kurasimisha ardhi kwa ajili ya wawekezaji wa ndani na wa nje. Kiasi
cha shilingi bilioni 192.2 kimetengwa katika eneo hili.
c)
Maendeleo ya Viwanda
81.
Mheshimiwa Spika, Serikali
inakusudia kuendeleza viwanda vinavyotumia malighafi zinazopatikana nchini;
viwanda vinavyoongeza thamani ya madini; viwanda vikubwa vya saruji; na viwanda
vya eletroniki na TEHAMA pamoja na kuboresha mazingira ya biashara na kutenga
maeneo maalum ya uwekezaji mijini na vijijini na kukuza ubia kati ya sekta ya
umma na sekta binafsi. Hatua hii inaenda sambamba na kuboresha na kuimarisha
viwanda vidogo vidogo nchini. Jumla ya shilingi bilioni 128.4 zimetengwa katika
eneo hili.
d)
Maendeleo ya Rasilimali Watu na Huduma
za Jamii
82.
Mheshimiwa Spika,
katika mwaka wa fedha 2012/13, Serikali imepanga kuboresha viwango vya elimu
katika ngazi zote hususan katika maeneo ya utafiti, ufundi stadi, afya; sayansi
na ujuzi maalum kuhusu madini, gesi, urani, chuma na mafuta; hatua hii
inajumuisha ukarabati wa maabara na upatikanaji wa vifaa vya maabara. Shilingi
bilioni 84.1 zimetengwa katika eneo hili.
e)
Utalii
83.
Mheshimiwa Spika, Serikali
itaendelea kuboresha huduma zitolewazo katika eneo hili ikiwa ni pamoja na
kutangaza utalii na kuboresha mazingira ya kitalii na kutoa mafunzo ya utalii,
kuainisha maeneo mapya ya utalii na kuboresha vyuo vya utalii.
Huduma za Fedha
84.
Mheshimiwa Spika,
Serikali itaendelea kuimarisha huduma za kifedha
hususan mifumo ya kuweka akiba na kukopa kama vile SACCOS, VICOBA na benki za
kijamii ili kuwawezesha wananchi kupata mitaji kwa ajili ya biashara na
uzalishaji. Kiasi cha shilingi bilioni 2.6 zimetengwa kwa ajili ya kuimarisha
mtaji wa Benki ya Wanawake, Mradi wa SELF na Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi
Kiuchumi. Aidha, Wizara ya Fedha itaendelea kusimamia maendeleo ya Taasisi za
fedha zinazojihusisha na utoaji wa mikopo kwa wajasiriamali. Ili kufanikisha
hili kitengo kilichopo cha maendeleo ya sekta ya fedha kitahuishwa na kuwa
idara kamili.
Usimamizi wa Fedha za
Umma
85.
Mheshimiwa Spika,
Serikali itaendelea kutekeleza awamu ya nne ya Programu ya Maboresho ya
Usimamizi wa Fedha za Umma na kuhakikisha kwamba Sheria ya Fedha za Umma na
Sheria ya Ununuzi wa Umma zinafuatwa kikamilifu ili kuongeza uwajibikaji katika
matumizi ya fedha za Umma. Maeneo yanayozingatiwa kwenye programu hiyo ni
pamoja na: kuendelea kuboresha Mtandao wa malipo (IFMS) ili kuimarisha udhibiti
wa matumizi ya fedha za Umma kwa Serikali Kuu na Mamlaka za Serikali za Mitaa;
utoaji wa mafunzo ya ulipaji kwa mfumo wa malipo wa kibenki kwa watumishi wa
Ofisi za Bunge, Sekretarieti za Mikoa, Idara ya Ushirika, Ofisi ya Waziri Mkuu
-TAMISEMI na Ofisi za Hazina ndogo Mikoa yote. Aidha, Serikali itaendelea kutoa
mafunzo ya kuandaa hesabu kwa kutumia viwango vya uhasibu vya kimataifa ili
kuongeza uwazi katika matumizi ya fedha za Umma; kuijengea uwezo Idara
ya Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali katika kuhakikisha kanuni na
taratibu za matumizi ya fedha za umma zinazingatiwa ipasavyo; na kujenga uwezo
wa Serikali Kuu, Mikoa na Halmashauri katika eneo la uandaaji wa mipango na
bajeti, ukusanyaji wa mapato, usimamizi wa raslimali, uboreshaji wa mawasiliano
na utoaji wa taarifa za utekelezaji wa bajeti.
86.
Mheshimiwa Spika,
Serikali itaendelea kuboresha utaratibu wa kupeleka fedha kwenye Halmashauri na
kutoa taarifa mapema kuhusu matumizi ya fedha zilizopelekwa. Aidha, fedha zote
zitakazovuka mwaka bila kutumika zitatolewa taarifa kwenye vikao vya Kamati za
Kudumu na Baraza la Madiwani ili kuongeza uwazi na uwajibikaji kwa umma.
87.
Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2012/13, Serikali itaendelea na zoezi la uhakiki wa watumishi kwenye Wizara,
Idara, Sekretarieti za Mikoa na Halmashauri zote ili kuondoa watumishi
wasiostahili kwenye orodha ya malipo ya mishahara ya watumishi wa Serikali.
Aidha, mamlaka za ajira na maafisa masuuli wanaelekezwa kusitisha malipo kwa
watumishi walioacha au kuachishwa kazi, kustaafu, kufariki au likizo bila
malipo ili kuzuia upotevu wa fedha za umma.
88.
Mheshimiwa Spika, Serikali
itaendelea kutilia mkazo wa ukaguzi wa mapato na matumizi ya fedha za umma
katika Wizara, Taasisi, Wakala, Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa ili
kuthibitisha endapo fedha zinazopangwa kukusanywa zinapatikana na pia fedha
zinazotumwa kutoka Hazina zinafika na kutekeleza shughuli zilizoidhinishwa.
Serikali itaboresha mifumo ya udhibiti na usimamizi wa fedha za umma
zinazokusanywa au kupelekwa kwenye Mikoa na Halmashauri nchini.
Usimamizi wa Mashirika ya Umma
89.
Mheshimiwa Spika, katika kukabliana na
changamoto za usimamizi wa Mashirika ya Umma, Serikali inaendelea
kuimarisha Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa kufanya mapitio ya Sheria za Msajili
wa Hazina ambazo ni “Treasury Registrar Ordinance” ya mwaka 1958 na “Treasury
Registrar Powers and Functions” SURA 370 ya mwaka 2000 kama ilivyorekebishwa
mwaka 2010 ili kuwa na Sheria moja. Lengo la hatua hiyo ni kuimarisha
ofisi kwa kuipa nguvu zaidi za kisheria kuweza kusimamia ipasavyo utendaji wa
Mashirika ya Umma pamoja na Taasisi ili kuongeza tija.
Kukabiliana na Mfumuko wa Bei
90.
Mheshimiwa Spika, uchumi wetu
unakabiliana na changamoto nyingi ikiwemo mfumuko wa bei ambao kwa wastani
umeshuka kutoka asilimia 19.8 mwezi Desemba 2011 hadi asilimia 18.7 mwezi
Aprili 2012. Kichocheo kikubwa cha mfumuko wa bei ni kupanda kwa bei za umeme,
mafuta na vyakula hususan mchele na sukari. Kwa mfano kwa mwezi Aprili 2012,
chakula kimechangia asilimia 24.7 wakati umeme na mafuta vimechangia kwa
asilimia 24.9. Mfumuko wa bei ambao haujumuishi chakula na nishati bado uko
kwenye tarakimu moja ambayo ni asilimia 8.8. Hivyo, jitihada za Serikali
zitaelekezwa katika kukabiliana na kupanda kwa bei ya bidhaa hizo.
91.
Mheshimiwa Spika, hatua za haraka
ambazo Serikali itachukua ni pamoja na kutoa vibali vya uagizaji wa sukari na
mchele kutoka nje na kuendelea kuimarisha Hifadhi ya Chakula ya Taifa. Aidha,
Serikali itawekeza katika kilimo cha mpunga na miwa katika mabonde makuu ya
Kilombero, Wami, Kagera na Malagarasi pamoja na miradi ya kilimo cha
umwagiliaji. Hatua nyingine ni pamoja na kuendelea kuimarisha
miundombinu ya usafirishaji na masoko; kuimarisha mfumo wa masoko kwenye maeneo
yanayozalisha chakula kwa wingi hususan mikoa ya nyanda za juu kusini na
mipakani. Kwa upande wa nishati ya umeme, Serikali itaendeleza vyanzo mbadala
vya umeme kama vile umeme wa gesi, nguvu za jua, upepo, miwa ili kupunguza
matumizi ya mafuta kama chanzo cha nishati.
Kupanua fursa za Ajira
92.
Mheshimiwa Spika, ili kuongeza ajira hasa kwa vijana,
Serikali itaendelea kupanua huduma za fedha ikiwa ni pamoja na kuanzisha Benki
ya Kilimo na kuongeza mitaji kwa Benki za Rasilimali, Wanawake, Posta na Twiga
Bancorp. Hatua nyingine zitakazochukuliwa na kuchangia ongezeko la ajira ni
pamoja na kujenga miundombinu ya barabara, umeme, kilimo na mawasiliano. Aidha,
sekta binafsi itahamasishwa kutumia fursa zinazotolewa na Benki na Maendeleo ya
Afrika kupitia Dirisha la kuendeleza sekta binafsi. Kadhalika, Serikali
itaajiri watumishi 71,756 katika sekta za Elimu, Afya, Kilimo na kada nyingine.
IV.
MABORESHO YA MFUMO WA KODI, ADA, TOZO NA HATUA NYINGINE ZA MAPATO:
93.
Mheshimiwa Spika, katika miaka ya hivi
karibuni, Serikali imefanya maboresho katika mfumo wa kodi kwa nia ya kupanua
wigo wa kodi na kuongeza mapato ya ndani. Maboresho yaliyofanywa ni
pamoja na marekebisho ya sheria za kodi, kanuni na taratibu za usimamiaji wa
kodi. Aidha hatua hizi zimechangia katika kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya
kodi na yasiyo ya kodi. Hata hivyo kuna changamoto katika kuhuisha mapato ya
ndani ili kupunguza utegemezi wa bajeti hatua kwa hatua. Kwa
kuzingatia hali hiyo Serikali itaendelea kuchukua hatua zenye kuboresha sera za kodi na usimamiaji wa mapato.
kuzingatia hali hiyo Serikali itaendelea kuchukua hatua zenye kuboresha sera za kodi na usimamiaji wa mapato.
94.
Mheshimiwa Spika, ili kuendeleza mafanikio
yaliyopatikana kwenye mfumo wa kodi, napendekeza kufanya maboresho katika
sheria mbalimbali za kodi kama ifuatavyo:-
a)
Sheria
ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, SURA 148;
b) Sheria
ya Kodi ya Mapato, SURA 332;
c) Sheria
ya Ushuru wa Bidhaa, SURA 147;
d)
Sheria
ya Ushuru wa Mauzo Nje, SURA 196;
e)
Sheria
ya Kodi ya Michezo ya Kubahatisha (Gaming Act), SURA, 41;
f)
Sheria
ya Usajili na Uhamishaji wa Magari, SURA, 124;
g)
Sheria
ya Ushuru wa Viwanja vya Ndege, SURA, 365;
h)
Misamaha
ya Kodi ya magari kupitia sheria za kodi na matangazo ya Serikali
(GNs);
i)
Marekebisho
mengine katika baadhi ya sheria za kodi na sheria za Usimamizi wa Fedha; na
j)
Marekebisho
ya Ada na Tozo Mbalimbali za Wizara, Mikoa na Idara zinazojitegemea.
k)
Sheria
ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, ya mwaka 2004;
A. Sheria ya
Kodi ya Ongezeko la Thamani, SURA 148
95.
Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya
marekebisho katika Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, SURA 148 kama
ifuatavyo: -
(i)
Kuanzisha
kiwango kipya (VAT Rate) cha asilimia 10 cha Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa baadhi
ya watu, taasisi na mashirika yanayopata unafuu wa kodi
hiyo
(special relief). Kwa mantiki hiyo, wale
waliokuwa hawalipi kodi hiyo kuanzia sasa watalipa asilimia 10. Hatua hii
itazihusu Kampuni binafsi, watu binafsi na Kampuni zitakazopewa vyeti vya Kituo
cha Uwekezaji Tanzania isipokuwa zile zenye vyeti hivyo kwa sasa. Aidha,
itahusu pia Mashirika yasiyo ya Kiserikali isipokuwa yale yaliyopewa
msamaha wa kodi pale yanapotoa huduma ya chakula, dawa baridi na vifaa kama
vile sabuni ambavyo vinatolewa msaada kwenye vituo mahsusi vya kulelea watoto
yatima na shule;
(ii)
Kurekebisha
kifungu cha 19 cha Jedwali la Pili la Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani ili
kuongeza Mashine za Elektroniki za kutoa stakabadhi za kodi (Electronic Fiscal
Devices - “EFDs”) katika orodha ya vifaa vinavyopata msamaha wa kodi hiyo.
Lengo ni kuwawezesha walipa kodi kupata vifaa hivi kwa gharama nafuu na
kuhamasisha matumizi yake kwa kuwa ni muhimu katika kutoa stakabadhi za mauzo
ya bidhaa na huduma;
(iii)
Kusamehe
Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa Vifaa vitakavyotumika kwa ajili ya gesi
iliyoshindiliwa na gesi ya mabomba (Compressed Natural Gas and Piped Natural
Gas). Msamaha wa kodi unatolewa ili kuhamasisha matumizi ya gesi katika magari,
kupikia, nyumbani, taasisi na viwandani. Aidha, Shirika la Maendeleo ya Petroli
(TPDC) litawajibika kuhakiki vifaa hivyo ili kuhakikisha kwamba vitatumika
kujenga miundo mbinu ya gesi.
96.
Mheshimiwa Spika, Mitambo na vifaa vya kujenga miundombinu ya
gesi asili vinavyoombewa msamaha wa kodi ni kama ifuatavyo:-
i.
CNG vehicles conversion
kits – vifaa vinavyoongezewa kwenye magari yaweze kutembea kwa kutumia nishati
ya gesi asili;
ii.
High pressure vessels
(CNG and LPG cylinders) – mitungi maalumu ya kutunzia gesi asili
iliyoshindiliwa na gesi ya LPG;
iii.
Natural Gas
Compression plants equipments – vifaa kwa ajili ya mitambo ya kushindilia gesi
asili;
iv.
Natural gas pipes
(Transportation and Distribution pipes) – mabomba maalum ya kusafirishia na
kusambazia gesi asili;
v.
CNG storage cascades –
mitungi maalum ya pamoja ya kusafirishia na kuhifadhia gesi asili
iliyoshindiliwa;
vi.
CNG transportation
trailers - magari na matela ya kusafirishia gesi asili iliyoshindiliwa;
vii.
Natural gas metering
equipments – mita za kupimia kiasi cha gesi asili;
viii.
Pipeline fittings and
valves – vifaa vya kuunganishia mabomba na kuruhusu/kuzuia gesi kupita;
ix.
CNG Refueling/filling
equipment – vifaa vya kujazia gesi asili kwenye magari;
x.
PNG/CNG accessories –
vifaa vidogo vidogo vinavyotumika katika ujenzi wa mabomba ya gesi asili na
katika mitambo ya kushindilia gesi asili;
xi.
Gas Receiving Unit –
vifaa vya kupokelea gesi ya mabomba;
xii.
Condensate Stabilizer
– vifaa vya mifumo ya kuimarisha uhifadhi wa condensate;
xiii.
Flare Gas System –
vifaa kwa ajili ya mifumo ya kuunguza gesi kwa ajili ya usalama;
xiv.
Air & Nitrogen
System – vifaa vya mifumo ya hewa na ya Nitrogen;
xv.
Condensate Tanks and
Loading Facility – matanki ya kuhifadhia condensate na vifaa vya
kupakilia;
xvi.
System piping on
piperack – mifumo ya kubeba mabomba ya gesi asili;
xvii.
Instrumentation –
vifaa vya umeme na udhibiti kwenye mifumo ya gesi asili.
xviii.
Majiko
yaliyotengenezwa mahsusi kwa ajili ya matumizi ya gesi pekee.
Hatua hizi katika Kodi ya Ongezeko la
Thamani kwa pamoja zitaongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni
22,565.1
B.
Sheria ya Kodi ya Mapato, SURA 332
97.
Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya
marekebisho ya Sheria ya Kodi ya Mapato, SURA 332 kama ifuatavyo: -
i.
Kuweka kiwango cha chini
cha mapato ghafi ya wafanyabiashara wadogo cha shilingi 3,000,000 kisichotozwa
kodi na kurekebisha matabaka (bands) ya walipa kodi. Lengo la hatua hii ni
kulinda mapato halisi ya Serikali na kuhakikisha kwamba wenye mapato ya chini
ya kiwango cha kutozwa kodi cha shilingi 3,000,000 hawatozwi kodi chini ya
mfumo wa kukadiria kodi Walipa kodi wadogo “Presumptive Scheme” kama ilivyo
kwenye mapato yatokanayo na ajira. Hivi sasa Wafanyabiashara wenye kipato hicho
wanatozwa Sh. 35,000.
Viwango vya sasa na
vinavyopendekezwa ni kama ifuatavyo: -
Viwango vya sasa
Thamani ya Mauzo
|
Kodi kwa wasiokuwa na kumbukumbu za mauzo
|
Kodi kwa wenye kumbukumbu za mauzo
|
||
(i)
|
Kwa
mauzo yasiyozidi Shs. 3,000,000/=
|
Shs. 35,000/=
|
1.1%
ya mauzo
|
|
(ii)
|
Kwa
mauzo yanayozidi Shs. 3,000,000/= na yasiyozidi Shs. 7,000,000/=
|
Shs. 95,000/=
|
Shs.
33,000/= + 1.3% ya mauzo yanayozidi Shs. 3,000,000/=
|
|
(iii)
|
Kwa
mauzo yanayozidi Shs. 7,000,000/= na yasiyozidi Shs. 14,000,000/=
|
Shs. 291,000/=
|
Shs.
85,000/= + 2.5% ya mauzo yanayozidi 7,000,000/=
|
|
(iv)
|
Kwa
mauzo yanayozidi Shs. 14,000,000/= na yasiyozidi Shs. 20,000,000/=
|
Shs. 520,000/=
|
Shs.
260,000/= + 3.3% ya mauzo yanayozidi Shs. 14,000,000/=
|
|
Viwango vinavyopendekezwa
|
||||
Thamani ya Mauzo
|
Kodi kwa wasiokuwa na kumbukumbu za mauzo
|
Kodi kwa wenye kumbukumbu za mauzo
|
||
(i)
|
Kwa
mauzo yasiyozidi Shs. 3,000,000/=
|
Asilimia sifuri (0%)
|
Asilimia
sifuri (0%)
|
|
(ii)
|
Kwa
mauzo yanayozidi Shs 3,000,000/= na yasiyozidi Shs 7,500,000/=
|
Shs. 100,000/=
|
2%
ya mauzo yanayozidi
Shs
3,000,000/=
|
|
(iii)
|
Kwa
mauzo yanayozidi Shs 7,500,000/= na yasiyozidi Shs 11,500,000/=
|
Shs. 212,000/=
|
Shs.
90,000/= plus 2.5% ya mauzo yanayozidi Shs 7,500,000/=
|
|
(iv)
|
Kwa
mauzo yanayozidi Shs 11,500,000/= na yasiyozidi Shs 16,000,000/=
|
Shs. 364,000/=
|
Shs.
190,000/= + 3.0% ya mauzo yanayozidi Shs 11,500,000/=
|
|
(v)
|
Kwa
mauzo yanayozidi Shs 16,000,000/= na yasiyozidi Shs 20,000,000/=
|
Shs. 575,000/=
|
Shs.
325,000/= + 3.5% ya mauzo yanayozidi Shs 16,000,000/=
|
|
ii.
Kutoza Kodi ya Zuio ya
asilimia 10 kwenye mapato yatokanayo na riba inayotolewa na mabenki kwa wafanyabiashara
ambao si wakaazi (non-residents). Lengo ni kuweka usawa kwa walipa kodi wote.
iii.
Kufanya marekebisho ya
kifungu cha 54 (2) cha sheria ya kodi ya mapato ili kufuta msamaha wa kodi ya
mapato kwa makampuni yenye hisa zipatazo asilimia 25 au zaidi. Lengo la
marekebisho haya ni kuleta usawa kwa walipa kodi wanapopata gawio.
iv.
Kuanzisha kodi itokanayo
na uuzaji wa raslimali ya uwekezaji (capital gains tax) kwenye uuzaji wa
hisa za kampuni za ndani unaofanywa na Kampuni mama ya nje ya nchi.
v.
Kuongeza kima cha chini
cha kutozwa kodi (threshold) kwenye mapato ya ajira kutoka shilingi 135,000
hadi 170,000. Hatua hii itaongeza kipato kwa mfanyakazi.
vi.
Kutoa msamaha wa Kodi ya
Mapato kwa soko la Hisa la Dar es Salaam (Dar es salaam Stock Exchange). Lengo
ni kulifanya soko hilo kukua.
vii.
Kusamehe Kodi ya Mapato
(kwa wenye leseni) yatokanayo na michezo ya kubahatisha iliyokwishalipiwa
kodi chini ya sheria ya kodi ya michezo ya kubahatisha, SURA 41. Lengo la hatua
hii ni kuepusha wenye leseni za biashara ya michezo ya kubahatisha kulipa kodi
mara mbili.
viii.
Kusamehe Kodi ya Zuio
kwenye riba ya mikopo inayotozwa na mabenki ya nje kwa wawekezaji wanaowekeza
kwenye sekta na shughuli muhimu katika mkakati wa kukuza uchumi (Strategic
Investors). Lengo la hatua hii ni kutoa unafuu kwa wawekezaji hao
wanapopata mikopo kutoka kwenye mabenki ya nje ya nchi na hivyo kuhamasisha
uwekezaji hapa nchini.
Hatua hizi za Kodi ya Mapato zitaongeza
mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 105,672.3
C.
Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, SURA 147
98.
Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya
marekebisho katika Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, SURA 147 kama ifuatavyo:-
i.
Kufuta Ushuru wa bidhaa uliokuwa unatozwa
kwenye mafuta mazito ya kuendeshea mitambo. Hivi sasa mafuta hayo yanatozwa
ushuru wa bidhaa wa shilingi 40 kwa lita. Lengo la hatua hii ni kupunguza
gharama za uzalishaji katika viwanda hapa nchini. Aidha, hatua hii itaongeza
uzalishaji na kuleta ushindani sawa kwa wenye viwanda katika nchi za Jumuiya ya
Afrika Mashariki (EAC) kwa kuwa nchi nyingine hivi sasa hazitozi ushuru kwenye
bidhaa hiyo.
ii.
Mheshimiwa Spika,
kumekuwa na kilio cha muda mrefu cha wasanii kudurufiwa kazi zao za sanaa na
kukosa maslahi kwa kazi wanazofanya. Ili kutatua tatizo hili, Serikali kupitia
Mamlaka ya Mapato itaanza kurasimisha biashara ya bidhaa za muziki na filamu
kwa nia ya kuhakikisha kwamba uasili wake unatambulika na hivyo kuzuia vitendo
vya kudurufu kazi za sanaa (piracy of artists work) hali ambayo inadumaza
ukuaji wa sanaa na vipaji hapa nchini. Aidha, Mamlaka ya Mapato itaweka stampu
kwenye bidhaa hizo ili uuzaji wa kazi hizo uwe rasmi na kuwawezesha wasanii
kupata kipato stahili kutokana na kazi zao. Vilevile hatua hii itaiingizia
serikali mapato.
Kwa kuwa yanahitajika maandalizi ya kutosha
ikiwa ni pamoja na kurekebisha sheria na kanuni mbalimbali, utekelezaji wa
hatua hii utaanza rasmi tarehe 1 Januari, 2013.
iii.
Kufuta msamaha wa Ushuru
wa Bidhaa kwa magari kwa wote waliokuwa wananufaika na msamaha huo isipokuwa
kwa miradi inayotekelezwa kwa misaada ya wafadhili yenye msamaha wa kodi kwenye
mkataba, mashirika ya dini, Balozi, Ofisi za Balozi, Wanabalozi na Wawakilishi
wa mashirika ya kimataifa (Diplomats and Diplomatic Missions). Aidha haitahusu
Kampuni za Madini zenye mikataba yenye kutoa misamaha.
iv.
Ili kulinda viwanda vya
hapa nchini vinavyotengeneza maji ya matunda (juisi) dhidi ya ushindani usio
haki wa bidhaa hiyo kutoka nje, maji ya matunda kutoka nje yatatozwa ushuru wa
bidhaa wa shilingi 83 kwa lita ambapo yanayozalishwa hapa nchini yatatozwa
ushuru wa bidhaa wa shilingi 8 tu kwa lita.;
v.
Kurejea msamaha wa ushuru
wa mafuta ya petroli (fuel levy) uliotolewa mwaka 2011/12 kwenye mafuta
yanayotumika kuendesha meli, na vifaa vingine vinavyotumika katika utafiti wa
mafuta na gesi ili usomeke kama Ushuru wa Bidhaa (Excise Duty) kwenye mafuta ya
Petroli.
vi.
Napendekeza kufanya marekebisho kwenye Ushuru wa
bidhaa unaotozwa kwenye pombe, vinywaji baridi, sigara, na mvinyo kama
ifuatavyo: -
a.
Vinywaji
baridi kutoka shilingi 69 kwa lita hadi shilingi 83 kwa lita ikiwa ni nyongeza
ya shilingi 14;
b.
Mvinyo
uliotengenezwa kwa Zabibu inayozalishwa hapa nchini kwa kiwango kinachozidi
asilimia 75 kutoka shilingi 420 kwa lita hadi shilingi 145 kwa lita, ikiwa ni
punguzo la shilingi 275;
c.
Mvinyo
uliotengenezwa kwa zabibu inayozalishwa nje ya nchi kwa kiwango kinachozidi asilimia
25, kutoka shilingi 1,345 kwa lita hadi shilingi 1,614 kwa lita, ikiwa ni
nyongeza ya shilingi 269;
d.
Vinywaji vikali, kutoka shilingi 1,993 kwa lita hadi
shilingi 2,392 kwa lita, ikiwa ni nyongeza ya shilingi 399.
e.
Bia
inayotengenezwa na nafaka ya hapa nchini na ambayo haijaoteshwa, kutoka
shilingi 248 kwa lita hadi shilingi 310 kwa lita, ikiwa ni nyongeza ya shilingi
62;
f.
Bia
nyingine zote, kutoka shilingi 420 kwa lita hadi shilingi 525 kwa lita, ikiwa
ni nyongeza ya shilingi 105 sawa na shilingi 52.5 kwa chupa yenye ujazo wa nusu
lita;
Marekebisho ya viwango vya Ushuru wa
bidhaa kwenye sigara ni kama ifuatavyo: -
a)
Sigara zisizo na kichungi na zinazotengenezwa
kutokana na tumbaku inayozalishwa hapa nchini kwa kiwango cha angalau asilimia
75, kutoka shilingi 6,820 hadi shilingi 8,210 kwa sigara elfu moja. Hii
ni sawa na nyongeza ya shilingi 1,390
kwa sigara elfu moja au shilingi 1.4 kwa sigara moja;
b)
Sigara zenye kichungi na zinazotengenezwa kutokana na
tumbaku inayozalishwa hapa nchini kwa kiwango cha angalau asilimia 75, kutoka
shilingi 16,114 hadi shilingi 19,410 kwa sigara elfu moja, ikiwa ni nyongeza ya
shilingi 3,296 au shilingi 3.3 kwa sigara moja;
c)
Sigara nyingine zenye sifa tofauti na (a) na (b)
kutoka shilingi 29,264 hadi shilingi 35,117 kwa sigara elfu moja, ikiwa ni nyongeza ya
shilingi 5,853 sawa na shilingi 5.8 kwa sigara moja;
d)
Tumbaku ambayo iko tayari kutengeneza sigara (cut
filler) kutoka shilingi 14,780 hadi shilingi 17,736 kwa kilo, ikiwa ni
nyongeza ya shilingi 2,956 kwa kilo; na,
e)
Ushuru wa “Cigar” unabaki kuwa asilimia 30.
vii.
Kutoza Ushuru wa bidhaa kwenye Gesi asilia
inayotumika viwandani kwa kiwango cha Shilingi 0.35 kwa kila futi ya
ujazo (Shs 0.35 per cubic feet);
viii.
Kuongeza Ushuru wa bidhaa kwenye muda wa
maongezi (airtime) kwenye simu za mkononi kutoka asilimia 10 kwenda asilimia
12. Lengo la hatua hii ni kuwianisha ushuru wa bidhaa unaotozwa kwa huduma hii
katika Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa wakati huu ambapo tupo kwenye
soko la pamoja.
Hatua hizi katika Ushuru wa Bidhaa kwa pamoja
zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni
144,054.9
D.
Sheria ya Ushuru wa Mauzo Nje, Sura 196;
99.
Mheshimiwa Spika, napendekeza
kuongeza kiwango cha Ushuru wa mauzo nje (export levy) kwenye bidhaa za ngozi
ghafi zinazosafirishwa kwenda nje ya nchi kutoka asilimia 40 za sasa au
Shilingi 400 kwa kilo moja hadi asilimia 90 au Shilingi 900 kwa kilo moja
kutegemea kiwango kipi ni kikubwa. Lengo la hatua hii ni kuhamasisha
usindikaji wa ngozi hapa nchini na kuongeza thamani ya bidhaa za ngozi. Aidha
hatua hii itachangia katika kukuza ajira viwandani na kuongeza mapato ya
Serikali.
Hatua hii inatarajiwa
kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni
26,431.8
E.
Sheria ya Kodi ya Michezo ya Kubahatisha
(Gaming Act), SURA, 41;
100. Mheshimiwa
Spika, napendekeza kufanya marekebisho katika
Sheria ya Kodi ya Michezo ya Kubahatisha (Gaming Act), SURA 41; kama
ifuatavyo:-
i.
Kuongeza
tozo la Gaming Tax kwa casino kutoka asilimia 13 ya mapato ghafi ya mchezo wa
kubahatisha (Gross Gaming Revenue) hadi asilimia 15;
ii.
Kutoza
tozo kwenye michezo ya Utabiri wa matokeo ya michezo (Sports Betting) kwa
asilimia 6 ya “total stakes”;
iii.
Kutoza
tozo la Gaming Tax kwa kiwango cha asilimia 43 kwenye michezo ya “SMS
Lotteries”;
iv.
Kutoza
tozo la Gaming Tax kwa kiwango cha asilimia 15 kwa michezo ya Internet Casino.
v.
Kuweka
kipengele katika Sheria ya Kodi ya Michezo ya kubahatisha kinachotamka kwamba
“gaming tax shall be conclusive tax”.
Hatua hii inatarajiwa kuongeza mapato ya
serikali kwa kiasi cha shilingi milioni
6,360.
F.
Sheria ya Usajili na Uhamishaji wa Magari, SURA, 124;
101.
Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya
marekebisho katika Sheria ya Usajili na Uhamishaji wa Magari, SURA, 124 kwa
kuanzisha utaratibu wa kumiliki usajili wa namba za magari zenye utambulisho wa
taarifa za mtu binafsi kwenye gari lake kwa ada ya shilingi 5,000,000 kwa miaka
mitatu.
Hatua hii inatarajiwa kuongeza mapato ya
Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 50
G.
Sheria ya Ushuru wa Viwanja vya Ndege,
SURA, 365;
102. Mheshimiwa
Spika, napendekeza kufanya marekebisho katika
Sheria ya Ushuru wa Viwanja vya Ndege, SURA, 365 kwa kuongeza tozo ya huduma za
viwanja vya ndege (Airport Service Charges) kutoka kiwango cha sasa cha Dola za
Kimarekani 30 hadi Dola 40 kwa safari za nje na kutoka Shilingi za Tanzania
5,000 hadi Shilingi 10,000 kwa safari za ndani.
Hatua hii inatarajiwa kuongeza mapato ya
Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 11,597.7
H.
Misamaha ya kodi ya magari kupitia sheria
za kodi na matangazo ya Serikali (GNs)
103. Mheshimiwa
Spika, napendekeza kufanya
marekebisho kwenye sheria husika za kodi na matangazo ya Serikali yanayotoa
msamaha wa kodi kwenye magari kwa walengwa mbalimbali ili kuweka ukomo wa umri
wa miaka nane (8) kwa magari hayo badala ya miaka 10. Aidha, magari yenye umri
wa zaidi ya miaka nane (8) yatatozwa Ushuru wa bidhaa wa asilimia 20. Lengo la
hatua hii ni kupunguza wimbi la uagizaji wa magari chakavu na kulinda
mazingira.
I.
Marekebisho mengine katika baadhi ya Sheria za Kodi na sheria za Usimamizi wa
Fedha
104. Mheshimiwa
Spika, napendekeza kufanya
marekebisho mengine madogo madogo yasiyo ya kisera katika Sheria mbalimbali za
kodi ili ziwe sanjari na azma ya kurahisisha utekelezaji wake.
105.
Mheshimiwa Spika, napendekeza
kufanya marekebisho katika sheria ya Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki,
SURA 231 ili kwanza, kuweka kinga dhidi ya mali zinazomilikiwa na Benki
ya Maendeleo ya Afrika Mashariki ikiwemo nyumba, akiba, fedha na akaunti za
benki dhidi ya mashauri ya kisheria, maamuzi ya kimahakama na utaifishaji. Pili,
kuipa hadhi ya mdai benki hii kama ilivyo kwa Taasisi ya Fedha ya Kimataifa
(IMF), Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Afrika ili kuiwezesha kupewa
upendeleo endapo yatatokea matatizo yoyote katika soko la fedha. Tatu,
kumpa mamlaka Waziri wa Fedha kutekeleza maamuzi ya Baraza la uongozi
(Governing Board) la EADB kwa kurekebisha Jedwali la Sheria hii kupitia Tangazo
la Serikali na baadaye kuwasilisha taarifa Bungeni. Nne, kutoa
tafsiri ya mali za benki ili kutoa ufafanuzi kwamba mali za benki ni pamoja na
nyumba za benki, akiba za fedha zilizokasimiwa kwa EADB kwa ajili ya utendaji
wake.
J.
Marekebisho ya Ada na Tozo Mbalimbali za
Wizara, Mikoa na Idara zinazojitegemea
106. Mheshimiwa
Spika, napendekeza kufanya
marekebisho ya viwango vya ada na tozo mbali mbali zinazotozwa na Wizara, Mikoa
na Idara zinazojitegemea ili kuvihuisha kulingana na hali halisi ya ukuaji wa
uchumi.
K.
Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, ya mwaka 2004
107. Mheshimiwa Spika,
Mawaziri wa Fedha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki walifanya Kikao cha maandalizi
ya Bajeti (Pre-Budget Consultations of EAC Ministers for Finance) mnamo tarehe
18 Mei 2012 jijini Kampala, Uganda. Kikao hicho kilipendekeza marekebisho ya
viwango vya Ushuru wa Pamoja wa Forodha (EAC-Common External Tariff “CET”) na
Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC-Customs Management Act,
2004) kwa mwaka wa fedha wa 2012/13. Mapendekezo hayo yanalenga katika
kuboresha Sekta za Viwanda, Usafirishaji, Afya, Nishati, Mifugo, Mawasiliano na
Habari.
108.
Mheshimiwa Spika, maeneo yanayopendekezwa
kufanyiwa marekebisho kwenye viwango vya Ushuru wa Pamoja wa Forodha ni: -
i.
Kutoza
ushuru wa asilimia sifuri (0%) badala ya asilimia 35 kwenye ngano
inayotambuliwa katika HS Code 1001.90.20 na HS Code 1001.90.90 kwa kipindi cha
mwaka mmoja. Lengo la hatua hii ni kupunguza gharama za uingizaji wa bidhaa hii
nchini kwa vile uzalishaji wa ndani bado ni wa chini kuweza kutosheleza
mahitaji.
ii.
Kuongeza
Ushuru wa Forodha kwenye galvanized wire kutoka asilimia sifuri (0%) hadi
asilimia 10 inayotambuliwa katika HS Code 7217.20.00. Hatua hii inalenga katika
kuwianisha viwango vya utozaji wa Ushuru wa Forodha kwa vile bidhaa hii
inatengenezwa kutokana na hot rolled steel wire rods zinazotambuliwa katika HS
Code 7213.20.00 ambayo inatozwa ushuru wa asilimia 10.
iii.
Kutenganishwa
kwa bidhaa zinazotambulika katika HS Code 2106.90.91 ili kutenganisha
virutubisho vya chakula na madini (food supplements and mineral premix)
vinavyotumika katika kutengeneza chakula cha watoto wachanga na kuzitoza Ushuru
wa Forodha wa asilimia sifuri (0%). Hatua hii inalenga katika kuwezesha watoto
wachanga na wagonjwa kuweza kupata vyakula vyenye virutubisho kwa bei nafuu na
kuimarisha afya zao.
iv.
Kupunguza
Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 25 hadi asilimia sifuri kwenye ving’amuzi
(set top boxes) vinavyotambuliwa katika HS Code 8528.71.00 ili kuwezesha
mabadiliko ya kutoka katika teknolojia ya analogi na kwenda katika teknolojia
ya digitali. Hatua hii inatekeleza makubaliano ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki kwamba ifikapo Desemba 2015 ziwe zimetoka kwenye mfumo wa
utangazaji wa analogi kwenda digitali.
v.
Kupunguza
Ushuru wa Forodha kwenye umeme (HS Code 2716.00.00) kutoka asilimia 10 hadi
asilimia sifuri (0%). Hatua hii inalenga katika kupunguza gharama ya umeme
unaonunuliwa kutoka nje ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na hivyo kupunguza
gharama za uzalishaji katika nchi hizo.
vi.
Kupunguza
Ushuru wa Forodha kwenye glasi za ndani (inner glass) za chupa za chai
(thermos) zinozotambuliwa katika HS Code 7020.00.90 kutoka asilimia 25 hadi
asilimia sifuri ili kutoa unafuu na kuchochea ukuaji wa viwanda vya kuunganisha
chupa za chai katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuwa bidhaa hiyo
haipatikani katika Jumuiya.
vii.
Kutenganisha
programu (software) inayotambulika katika HS Code 8523.80.00 ili kutoza Ushuru
wa Forodha wa asilimia sifuri (0%). Lengo ni kuhamasisha ukuaji wa Sekta ya
Mawasiliano na hivyo kuongeza mchango wake katika Pato la Taifa.
viii.
Kutoa
msamaha wa Ushuru wa Forodha (duty remission) kwenye malighafi ya kutengeneza
sabuni (Palm Sterini, RBD) inayotambuliwa katika HS Code 1511.90.40 kwa kipindi
cha mwaka moja. Hatua hii inalenga katika kuvipa unafuu viwanda vidogo vya
kutengeneza sabuni hapa nchini na kuviwezesha kumudu ushindani katika bidhaa
hiyo inapoingizwa kutoka nje.
ix.
Kutoa
msamaha wa Ushuru wa Forodha (duty remission) kwa malighafi ya kutengeneza
sabuni inayojulikana kama LABSA inayotambuliwa katika HS Code 3402.11.00; HS
Code 3402.12.00 na HS Code 3402.19.00 kwa kipindi cha mwaka mmoja. Hatua hii
inalenga katika kuimarisha uzalishaji na kukuza viwanda vidogo vya sabuni
nchini.
x.
Kupunguza
Ushuru wa Forodha kwenye bidhaa inayojulikana kama cathodes inayotambuliwa
katika HS Code 7403.11.00 kutoka asilimia 10 hadi sifuri (0%). Hivi sasa bidhaa
hii inatozwa ushuru wa asilimia 10 ambapo shaba iliyotengenezwa kwa ukamilifu
(refined alloys/refined copper) hutozwa ushuru wa asilimia (0%), ambapo ni
kinyume na matakwa ya sheria ya ushuru wa forodha ya jumuiya ya Afrika
Mashariki ya mwaka 2004. Lengo la hatua hii ni kuwianisha ushuru wa malighafi
inayotumika kuzalisha bidhaa hii ili iendane na kanuni/taratibu za kutoza
ushuru zinazozingatia viwango vya usindikaji.
xi.
Kuendelea
kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 badala ya asilimia 35 kwenye saruji
inayotambuliwa katika HS Code 2523.90.00 kwa kipindi cha mwaka mmoja.
xii.
Kutoa
msamaha wa Ushuru wa Forodha (duty remission) kwa wazalishaji wanaotumia mafuta
ya kutengeneza vilainishi (castor oil and its fraction) inayotambuliwa katika
HS Code 1515.30.00 Hatua hii imezingatia kwamba bidhaa hii ni mali ghafi
inayotumika katika kutengeneza vilainishi;
xiii.
Kutoa
msamaha wa Ushuru wa Forodha kwenye vyuma vinavyowekwa kwenye kingo za barabara
vijulikanavyo kama road guard rails kwa kutenganisha HS Code 7308.90.90. Lengo
ni kutoa unafuu katika ujenzi wa miundombinu ya barabara. Aidha, hatua hii
inazingatia kwamba bidhaa hii haizalishwi kwa kiwango cha kukidhi mahitaji ya
soko la Jumuiya ya Afrika Mashariki;
109.
Mheshimiwa Spika, Mawaziri wa Fedha
wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki walifanya marekebisho kwenye
Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC-Customs Management Act,
2004) kama ifuatavyo:-
i.
Kufanya
marekebisho katika Kifungu 30(b) cha Sehemu B ya Jedwali la Tano la Sheria ya
Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ili kutoa msamaha wa Ushuru wa Forodha
kwenye mitambo (machinery) na vipuri vyake vinavyotumika kwenye uchimbaji wa
madini. Msamaha huu hautahusisha vipuri vya magari vitakavyoagizwa na
makampuni yanayojihusisha na uchimbaji wa madini.
ii.
Kufanya
marekebisho katika aya ya 22 (a) ya Jedwali la Tano la Sheria ya Forodha ya
Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuongeza “refrigerated trailers” katika bidhaa
zinazopata msamaha wa Ushuru wa Forodha. Hatua hii inalenga katika kutoa
msamaha wa Ushuru wa Forodha kwenye magari ya trela yenye majokofu ili
kuimarisha biashara ya usambazaji bidhaa kama vile nyama, maziwa n.k.
iii.
Kutoa
msamaha wa Ushuru wa Forodha kwenye malighafi zinazotumika katika kutengeneza
vifaa vya kufanyia uchunguzi wa magonjwa (medical diagnostic kits) kwa kuwa
vifaa hivyo hutozwa asilimia sifuri (0%) vinapoagizwa kutoka nje. Aidha, lengo
pia ni kuhamasisha uzalishaji wa bidhaa hiyo katika Nchi za Jumuiya ya Afrika
Mashariki.
iv.
Kufanya
marekebisho katika Jedwali la Tano, B kwenye aya ya 15 ili kuongeza vifaa
vinavyotumika katika ufugaji na kurina asali na kuvipa msamaha wa ushuru wa
forodha vinapoagizwa nje na wafugaji wa nyuki. Lengo ni kuhamasisha na
kuchochea ukuaji wa sekta ya ufugaji wa nyuki.
v.
Kuendelea
kutoa msamaha wa Ushuru wa Forodha kwenye migahawa ya Majeshi ya Ulinzi kwa
kipindi cha mwaka mmoja.
vi.
Kufanya
marekebisho katika Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka
2004 ili kutoa msamaha wa Ushuru wa Forodha (duty remission) kwa wazalishaji wa
vyakula vinavyotengenezwa mahsusi kwa lishe ya watoto wenye utapia mlo na watu
wanaoishi na virusi vya ukimwi. Hatua hii inalenga katika kuwawezesha kupata
vyakula hivyo kwa gharama nafuu na kuboresha afya zao.
110.
Mheshimiwa Spika, Marekebisho mengine
ninayotarajia kufanya kwenye Ushuru wa Forodha ni kama ifuatavyo: -
i.
Kufuta
msamaha wa Ushuru wa Forodha kwa magari yenye ujazo wa cc 3000. Hatua hii
haitahusu miradi inayotekelezwa kwa misaada ya wafadhili yenye msamaha wa kodi
kwenye mikataba, mabalozi na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa (Diplomats
and Diplomatic missions).
ii.
Kupunguza
msamaha wa kodi uliokuwa unatolewa kwenye bidhaa zinazotambulika kama “deemed
capital goods” kutoka asilimia 100 hadi asilimia 90. Kwa mantiki
hiyo, mwekezaji atatakiwa kulipa asilimia 10 ya kodi zote zinazotozwa kwenye
bidhaa husika.
Hatua hizi kwa pamoja zinatarajiwa kupunguza
mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni
12,805
Mheshimiwa Spika, hatua
zote za mapato kwa ujumla zimezingatia azma ya Serikali ya kukuza uchumi na
kuongeza mapato ili hatimaye kupunguza utegemezi wa bajeti kutoka kwa wahisani.
Aidha, ili kutekeleza azma hiyo, hatua za mapato zinalenga katika kupunguza
misamaha ya kodi hatua kwa hatua ili kufikia kiwango cha asilimia 1 ya Pato la
Taifa kama ilivyo katika nchi nyingine Wanachama wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki.
L.
Tarehe ya Kuanza Kutekeleza Hatua Mpya za
Kodi
111. Mheshimiwa
Spika, hatua hizi za kodi
zinazopendekezwa zitaanza kutekelezwa tarehe 1 Julai, 2012, isipokuwa pale
ilipoelezwa vinginevyo.
V. SURA YA BAJETI KWA MWAKA
2012/13
112.
Mheshimiwa Spika, kwa
kuzingatia sera za uchumi pamoja
na misingi na sera za bajeti,
Serikali inatarajia kukusanya shilingi bilioni 15,119.6. Kati ya mapato hayo,
Serikali
inalenga kukusanya mapato ya kodi na yasiyo ya kodi ya jumla ya shilingi
bilioni 8,714.8 sawa na asilimia 18 ya Pato la Taifa.
Aidha, mapato kutokana na vyanzo vya Halmashauri ni shilingi bilioni 362.2 sawa
na asilimia 0.7 ya Pato la Taifa.
113.
Mheshimiwa Spika, Washirika
wa Maendeleo wanatarajiwa kuendelea kutusaidia mwakani kwa kutupatia misaada na
mikopo ya jumla ya shilingi bilioni 3,156.7. Kati ya fedha hizo, shilingi
bilioni 842.5 ni misaada
na mikopo ya kibajeti na shilingi bilioni 2,314.2 ni mikopo na misaada kwa
ajili ya miradi
ya maendeleo, ikijumuisha Basket Funds na fedha za Millenium Challenge Account
(MCA - T).
114.
Mheshimiwa Spika, Serikali
inategemea kukopa kiasi cha shilingi bilioni 2,886.1 kutoka vyanzo vya ndani na
nje kuziba pengo la mapato. Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 1,148.1 ni kwa
ajili ya kulipia hatifungani na dhamana za Serikali za muda mfupi zinazoiva,
shilingi bilioni 483.9 ambayo ni asilimia moja ya Pato la Taifa na shilingi
bilioni 1,254.1 ni mikopo yenye masharti ya kibiashara.
115.
Mheshimiwa Spika, Kwa
upande wa matumizi, Serikali imepanga kutumia jumla ya shilingi bilioni
15,119.6 katika mwaka 2012/13 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na ya maendeleo.
Jumla ya shilingi bilioni 10,591.8 zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida
ikijumuisha shilingi bilioni 3,781.1 kwa ajili ya mishahara ya watumishi wa
Serikali, Taasisi na Wakala za Serikali na shilingi bilioni 2,745.1 kwa ajili
ya Mfuko Mkuu wa Serikali. Aidha, jumla ya shilingi bilioni 4,527.8 zimetengwa
kwa ajili ya matumizi ya maendeleo, ambapo kiasi cha shilingi bilioni 2,213.6
kitagharamiwa kwa fedha za ndani na shilingi bilioni 2,314.2 kitagharamiwa kwa
fedha za nje (misaada na mikopo ya miradi ya maendeleo ikijumuisha miradi ya
MCA (T) na basket fund).
116.
Mheshimiwa Spika, kwa
kuzingatia mfumo wa bajeti kama ulivyoelezwa hapo juu, sura ya bajeti kwa mwaka
2012/13 inakuwa kama ifuatavyo:-
Mapato
|
Shilingi Milioni
|
|||
A.
|
Mapato ya Ndani
|
8,714,671
|
||
(i)
Mapato ya Kodi (TRA)
|
8,070,088
|
|||
(ii)
Mapato yasiyo ya Kodi
|
644,583
|
|||
B.
|
Mapato ya Halmashauri
|
362,206
|
||
C.
|
Mikopo na Misaada ya Kibajeti
|
842,487
|
||
D.
|
Mikopo na Misaada ya Miradi ya Maendeleo ikijumuisha MCA (T)
|
2,314,231
|
||
E.
|
Mikopo ya Ndani
|
1,631,957
|
||
F.
|
Mikopo yenye Masharti ya Kibiashara
|
1,254,092
|
||
JUMLA YA MAPATO YOTE
|
15,119,644
|
|||
Matumizi
|
||||
G.
|
Matumizi ya Kawaida
|
10,591,805
|
||
(i)
Deni la Taifa
|
2,745,056
|
|||
(ii)
Mishahara
|
3,781,100
|
|||
(iii)
Matumizi Mengineyo
|
4,065,649
|
|||
Wizara
3,311,399
|
||||
Mikoa
49,701
|
||||
Halmashauri 704,549
|
||||
H.
|
Matumizi ya Maendeleo
|
4,527,839
|
||
(i)
Fedha za Ndani
|
2,213,608
|
|||
(ii)
Fedha za Nje
|
2,314,231
|
|||
JUMLA YA MATUMIZI YOTE
|
15,119,644
|
|||
117.
Mheshimiwa
Spika, mambo yaliyozingatiwa wakati wa mgao wa fedha kwa bajeti ya
mwaka 2012/13 ni pamoja na yafuatayo:-
i.
Kuweka
mafungu yote katika kiwango cha mgao wa fedha kinacholingana na matarajio ya
matumizi ya mafungu husika kwa mwaka 2011/12;
ii.
Kuyatengea
fedha matumizi yasiyoepukika kama vile posho za kisheria, “ration allowance”,
nk.
iii.
Maeneo
mapya ya utawala;
iv.
Fedha
zinazotolewa kwa wizara zenye utaratibu wa kubakiza (retention);
v.
Maeneo
ya vipaumbele (strategic na non-strategic).
118.
Mheshimiwa
Spika, bajeti ninayoiwasilisha ina uwiano wa asilimia 70 kwa matumizi
ya kawaida na asilimia 30 kwa matumizi ya maendeleo. Viwango hivyo
vya uwiano vimezingatia ukweli kwamba makisio ya matumizi ya maendeleo kwa fedha
za ndani ya Shilingi 1,871.5 bilioni na makisio ya matumizi ya maendeleo kwa
fedha za nje ya Shilingi 3,054.1 bilioni yenye jumla ya Shilingi 4,925.6 kwa
mwaka 2011/12 hayatafikiwa. Hivyo, inatarajiwa kwamba hali halisi ya
matumizi ya maendeleo itakuwa Shilingi 2,983 bilioni ambayo ni karibu ya
asilimia 22. Kwa kipindi kilichoishia Aprili, 2012 matumizi ya maendeleo kwa
fedha za ndani yalifikia 1,201.6 bilioni na matumizi ya maendeleo kwa fedha za
nje ni shilingi 1,450.4 bilioni. Sababu za kutofikiwa kwa malengo hayo ya
matumizi nimezieleza hapo awali ikiwa ni pamoja na kutopatikana kwa fedha za
mikopo ya kibiashara na kuchelewa kwa fedha za misaada na mikopo ya
miradi ya maendeleo kutoka kwa wahisani. Aidha, uwiano huo umezingatia
maeneo niliyoyataja hapo juu ambayo ni matumizi muhimu.
VI.
HITIMISHO
119.
Mheshimiwa Spika,
Serikali kupitia bajeti hii imejipanga kutekeleza Mpango wa Maendeleo wa mwaka
2012/13 ambao unaelekeza uwekezaji wa rasilimali za Taifa kwenye
maeneo machache ya kipaumbele kwa lengo la kuongeza
kasi ya kukua kwa uchumi na kupunguza umaskini. Serikali itaendelea kuhamasisha
sekta binafsi kwa kuwekeza zaidi katika maeneo ya kipaumbele. Aidha, kila
mwananchi anapaswa kushiriki kikamilifu katika kutumia fursa zinazojitokeza kwa
kutoa huduma na kuzalisha mali ili kujiongezea kipato.
120.
Mheshimiwa Spika, kufanikiwa kwa Bajeti
ya Mwaka 2012/13 kunahitaji nidhamu ya hali ya juu kwa kila Wizara, Idara,
Mikoa, Taasisi na Mamlaka za Serikali za Mitaa katika ukusanyaji wa mapato na
matumizi ya fedha za umma. Matumizi yasiyokuwa na
tija na ambayo si muhimu ni vyema yakaepukwa. Sekta binafsi ina uwezo mkubwa wa
kuchangia katika uchumi. Hivyo, ni muhimu kila Wizara, Idara, Mikoa na Mamlaka
za Serikali za Mitaa kutoa fursa kwa sekta binafsi ili waweze kuchangia
kikamilifu katika kukuza uchumi wa Taifa letu.
121.
Mheshimiwa Spika, Mkutano wa
Bunge la Bajeti mwaka huu unafanyika miezi michache kabla
ya zoezi muhimu la Sensa ya Watu na Makazi itakayofanyika tarehe 26 Agosti
2012. Kauli mbiu ya sensa ya mwaka huu ni ‘‘Sensa kwa Maendeleo Jiandae
Kuhesabiwa’’. Napenda kutoa wito kwa Waheshimiwa Wabunge na viongozi
wengine katika ngazi zote kuhamasisha wananchi kushiriki katika zoezi hili
ambalo matokeo yake yatawezesha kupata takwimu muhimu zitakazowezesha Serikali
kupanga mipango kwa ajili ya maendeleo ya wananchi kwa usahihi.
122.
Mheshimiwa Spika, napenda
kutumia nafasi hii kuwashukuru wapiga kura wangu wote wa Jimbo la Kalenga kwa
kunichagua kuwa Mbunge wao na kwa ushirikiano wanaonipatia. Napenda kuwaahidi
kuwa nitaendelea kushirikiana nanyi kuliletea maendeleo Jimbo letu la Kalenga.
Mwisho namshukuru mke wangu mpendwa pamoja na familia kwa kuwa msaada kwangu
katika kutekeleza majukumu haya mapya.
123.
Mheshimiwa Spika,
naomba kutoa
hoja.
No comments:
Post a Comment