Umoja wa mataifa unasema kuwa maelfu ya Wapalestina wanakimbia kutoka kwenye kambi moja ya wakimbizi iliyo karibu na mji wa bandari wa Latakia nchini Syria. Kambi hiyo imekuwa ikishambuliwa kwa makombora na jeshi la Syria kwa siku ya tatu mfululizo.
Watu wasiopungua 30 wameripotiwa kuuwawa tangu jumamosi ambapo vikosi vya serikali vilianza kutekeleza harakati hizo za kijeshi kutoka ardhini na baharini. Msemaji wa Umoja wa Mataifa Christopher Gunness, ameiambia BBC kwamba takriban nusu ya wakimbizi kwenye kambi hiyo yenye watu elfu kumi wanaukimbia mji huo.