Tuesday, 12 June 2012

MAELFU WAMWAGA BOB MAKANI



 


RAIS Jakaya Kikwete ameongoza mamia ya waombolezaji kutoa heshima za mwisho kwa mwasisi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Bob Makani (76), aliyefariki dunia Jumamosi iliyopita.
Akizungumza katika shughuli hiyo, iliyofanyika kwenye Viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam, Rais Kikwete alisema mchango wa hayati Makani hasa katika nyanja za kisiasa na kiuchumi utakumbukwa daima na Watanzania.

“Aliitumia vizuri nafasi yake kama mwanasiasa, hali kadhalika, alipokuwa mfanyakazi wa umma katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), alikuwa mchapakazi,” alisema Rais Kikwete.
Katika hotuba yake fupi, Rais alieleza jinsi alivyozipata taarifa za msiba huo mkubwa na jinsi alivyoguswa kwa kumpoteza mwanasiasa mkongwe.... “Binadamu anaweza kupata urefu au ufupi, unene au wembamba, lakini kifo ni cha kila mtu.”

Mbowe: mfumo ulimsaliti Makani
Akimzungumzia hayati Makani, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema alikuwa ni mwanasiasa mahiri na mkweli, lakini mfumo wa kisiasa Tanzania haukumpa fursa ya kupata nafasi ya uongozi kitaifa.

Alisema, Makani aligombea ubunge zaidi ya mara mbili lakini hakuwahi kushinda kwa kile ambacho Mbowe alidai kuwa ni tatizo la mfumo.

“Bob alikuwa akishinda katika kila chaguzi, lakini mfumo haukumkubali,” alidai.
Mwenyekiti huyo alishauri kuwa Katiba Mpya haina budi kuwaangalia watu muhimu wenye kazi zilizotukuka ili wawepo bungeni kwa ajili ya kutoa mawazo, ushauri na hekima zao pamoja na kuwaenzi.

“Wapo wanasiasa wengi, wengine ni waongo na wasiotekeleza ahadi zao lakini wanaingia bungeni, lakini pia wapo wanasiasa werevu na wa kweli, ila tu wanakosa fursa za kuongoza,” alisema Mbowe.
Katika hotuba yake, Mbowe alikumbuka nyakati muhimu za marehemu Makani alizowahi kuzishuhudia ikiwemo kutoa hotuba fupi kuliko zote katika moja ya kampeni zake za kugombea ubunge huko Shinyanga.

“Katika kampeni hiyo, Makani alitoa hotuba fupi pengine kuliko zote. Alinyoosha mikono yake na kusema, ‘Nawapenda’ kisha akamaliza” alisema Mbowe

Mtei amlilia
Mwasisi wa Chadema, Edwin Mtei aliyeanzisha chama hicho pamoja na Makani alisema taifa limepoteza nguzo imara wakati huu likiwa katika mchakato wa mabadiliko muhimu ya nchi.
Hotuba hiyo ya Mtei iliyosomwa kwa niaba yake na Mzee wa Chadema, Victor Kimesera ilieleza historia ya wawili hao wakiwa wanafunzi katika Shule ya Sekondari Tabora na baadaye wafanyakazi wa BoT.
“Mimi na Makani tumekutana mwaka 1951 na tangu wakati huo tumekuwa pamoja tukishirikiana katika mambo mengi,” alisema Mtei.

Slaa: ni pengo lisilozibika
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alimtaja marehemu Makani kuwa mtu jasiri ambaye alianzisha chama cha upinzani hasa enzi zile ambazo upinzani ulionekana kama uhaini... “Alikuwa ni mtu ambaye haogopi, alisema hadharani kile alichokiona kinafaa.”

Dk Slaa alisema japokuwa Makani alikuwa mgonjwa na umri wake kuwa mkubwa, lakini bado aliendelea kufanya kazi za chama bila makosa.

“Unaweza kumuamsha Makani usiku wa manane na akafanya kazi za chama. Kwetu sisi hili ni pigo kwani tumempoteza mshauri na jemedari wa jeshi la kuleta mabadiliko.”

Wengine waliotoa hotuba katika hafla hiyo ni mwakilishi wa vyama vya upinzani, Profesa Ibrahim Lipumba (CUF) ambaye alimtaja marehemu kama mchezaji wa mpira hodari na mwerevu.

“Nilisoma na Makani shule moja, ingawa aliniacha kwa miaka mingi. Alikuwa ni mchezaji hodari na mwerevu,” alisema Profesa Lipumba.

Alimtaja hayati Makani kuwa ni Mtanzania mzalendo aliyejitoa kwa kiasi kikubwa kuifikisha nchi ilipo hasa katika mchakato wa kuleta Katiba Mpya.

Naibu Gavana wa BoT, Dk Natu Mwamba alisema taasisi hiyo haitamsahau kamwe Makani kutokana na uchapaji kazi wake na kuishi vizuri na wafanyakazi wengine.

Alisema aliteuliwa kuwa Naibu Gavana wa BoT mwaka 1966 na alikuwa ni mmoja wa maofisa waliofanya kazi kubwa katika kushughulikia tatizo la kuungua kwa Benki Kuu miaka ya 1970.
Mwili wa Makani ambaye alizaliwa mwaka 1936, ulisafirishwa jana jioni kwa ndege kwenda Shinyanga kwa mazishi.

Makani ilianza kupata matatizo ya kiafya katika miaka ya karibuni na wakati wa uzinduzi wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2010 katika Viwanja vya Jangwani, Dar es Salaam, aliishiwa nguvu na kudondoka. Alisimama baadaye na kuwasalimia wananchi.

Pia Januari 17, mwaka huu katika msiba wa aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Regia Mtema alianguka tena muda mfupi baada ya kuaga mwili wa marehemu.

Wasifu
Marehemu Makani alizaliwa mwaka 1936 huko Kolandoto, Shinyaga.
Alianza darasa la kwanza akiwa na umri wa miaka sita, mwaka 1942 katika Shule ya Ibadakuli, hukohuko Shinyanga.

Alijiunga na Shule ya Sekondari ya Tabora ambako alifaulu vizuri na kuchaguliwa kujiunga na Chuo Kikuu cha Makerere, Uganda.

Alipata shahada ya pili ya sheria katika Chuo Kikuu cha Liverpool, Uingereza.
Mwaka 1965 alirejea nchini na kuajiriwa katika utumishi wa umma akiwa Mwanasheria wa Serikali.
Hakudumu katika nafasi hiyo kwani alipandishwa cheo na kuteuliwa kuwa Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania wakati huo, Edwin Mtei, akiwa ni Gavana.

Mwaka 1991-92 wakati vuguvugu la mfumo wa vyama vingi likianza, Makani akishirikiana na Mtei walianzisha Chadema.Namba ya kadi ya uanachama ya Makani ilikuwa ni tatu.
Mwaka 1991 alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa kwanza wa Chadema na mwaka 1995 aliteuliwa kuwa Mwenyekiti nafasi aliyoishika hadi 2005 alipostaafu.

Baada ya kustaafu, Makani alibaki kuwa mshauri na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya chama hicho.
Vyeo vingine alivyowahi kushika ni pamoja na Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mkurugenzi wa Kiwanda cha Bia Tanzania (TBL) na Mkurugenzi wa Kampuni ya Uwakili ya “Makani and Adovacate Company.’

Makani alifariki dunia katika Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam Jumamosi iliyopita, baada ya kuugua maradhi ya moyo yaliyomsumbua tangu mwaka 2009.

No comments:

GEITA DOCUMENTARY

Contributors