Kama ilivyo ada, katika maadhimisho hayo
yatakayofanyika kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam, Rais Jakaya
Kikwete anatarajia kukagua gwaride la vikosi mbalimbali vya ulinzi na
usalama ambavyo pia vitatoa heshima kwa kiongozi huyo kwa mwendo wa pole
na haraka. Baadaye kikosi cha anga kitatoa heshima zake na kufuatiwa na
burudani mbalimbali ikiwamo ngoma na michezo ya halaiki. Sherehe hizo
pia zitahudhuriwa na wageni mbalimbali waalikwa wa ndani na nje ya nchi,
wakiwamo mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini.
Katika sherehe hizo, Rais Kikwete hutoa msamaha
kwa wafungwa na mwaka jana aliwasamehe wafungwa 3,814 waliokuwa na umri
zaidi ya miaka 70, wenye ulemavu wa mwili na akili, magonjwa kama
Ukimwi, kifua kikuu na saratani ambao wako kwenye hatua ya mwisho ya
ugonjwa,
Wengine ni wafungwa wa kike walioingia na mimba
gerezani na walioingia na watoto wanaonyonya na wanaotumikia kifungo
kisichozidi miaka mitano ambao hadi siku ya msamaha, walikuwa
wametumikia robo ya vifungo vyao.
Katika maadhimisho hayo mwaka jana,
yaliyohudhuriwa na viongozi 14 wa kutoka Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za
Kusini mwa Afrika (SADC), Rais Kikwete aliwataka Watanzania kujivunia
na kuyaenzi mafanikio ya kisiasa, kiuchumi na kijamii yaliyopatika tangu
nchi ilipopata uhuru.