Friday 13 April 2012


BABA MZAZI WA LULU ATAKA JAMII ISIMHUKUMU MWANAWE


BABA mzazi wa msanii wa filamu, Elizabeth Michael 'Lulu,' ameitaka jamii kutomhukumu mwanawe kutokana na kifo cha msanii mwenzake marehemu Steven Kanumba, badala yake iache vyombo vya sheria vifanye kazi yake.

Mzazi huyo, Michael Edward Kimemeta anayeishi mjini Moshi, amewaomba Watanzania kuiachia Mahakama iamue kama mtoto wao anahusika katika kifo hicho ama la.

Kimemeta, ameeleza kuwa binti yake ana umri wa miaka 16 tofauti na inavyoelezwa kuwa ana miaka 18.

MAONYESHO YA SABA YA VYUO VIKUU KUANZA APRIL 18


Maonyesho ya saba ya vyuo vikuu yatafanyika kuanzia tarehe 18 hadi 20 mwezi Aprili mwaka 2012 katika ukumbi wa Diamond Jubilee Upanga Dar es Salaam.
Mgeni rasmi atakuwa Makamu wa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dr. Gharib Bilali.
Maonesho yatakuwa yanafunguliwa saa tatu kamili asubuhi na kufungwa saa kumi na mbili jioni kila siku.
       'HAKUNA KIINGILIO NA WOTE MNAKARIBISHWA'

Thursday 12 April 2012

Wizi wa kazi za wasanii waibua mjadala Bungeni


SUALA la wizi wa kazi za wasanii nchini, limeibua mjadala mkali bungeni huku Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto akipendekeza mtu atakayekamatwa akiuza CD na DvD feki za kazi za wasanii atozwe faini isiyopungua sh50 milioni.

Mbunge huyo ambaye pia ni Naibu Msemaji wa Kambi rasmi ya upinzani Bungeni, alipendekeza kuwa mtu yeyote atakayekutwa na kazi feki za wasanii naye aadhibiwe vikali ili kujenga Utamaduni wa Watanzania kuacha kununua kazi za wizi wasaniii.

Wabunge hao walichachamaa Bungeni mjini Dodoma jana wakati wakichangia hotuba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Cyril Chami kuhusu muswada wa sheria ya marekebisho ya sheria mbalimbali za biashara wa mwaka 2011.

Mutharika kuzikwa April 23


IKULU ya Malawi imethibitisha jana kuwa mazishi ya Rais wake wa tatu, Bingu wa Mutharika yatafanyika Aprili 23, mwaka huu katika shamba lake lililopo Ndata, Wilaya ya Thyolo, kusini mwa Mji wa Blantyre.

Uamuzi huo unakwenda sambamba na ule wa kuongezwa kwa siku za maombolezo kutoka 10 hadi 30, ili kuyapa maombolezo hayo uzito unaolingana na msiba wa “mkuu wa nchi aliyefariki dunia akiwa madarakani.”


Awali, kabla ya Rais Banda kuapishwa, Ofisi ya Rais na Baraza la Mawaziri (OPC) ya Malawi, ilitoa taarifa kwamba kungekuwa na siku 10 tu za maombolezo ambazo zilitarajiwa kumalizika Jumapili wiki hii.

Lakini kutokana na kuongezeka kwa siku 20 zaidi, maombolezo hayo yanatarajiwa kukoma ifikapo Mei 6, mwaka huu na katika kipindi chote hicho, bendera zitaendelea kupepea nusu mlingoti huku televisheni na redio zikipiga muziki wa maombolezo.

Wednesday 11 April 2012

quote of the day


Jenerali Mwita Kyaro afariki dunia

MKUU wa Majeshi Mstaafu Jenerali Ernest Mwita Kyaro, amefariki dunia katika Hospitali ya Bugando jijini Mwanza.

Msemaji wa Jeshi la Wananchi Tanzania ( JWTZ), Kanali Kapambala Mgawe alithibitisha kutokea kwa kifo hicho akieleza kuwa Jenerali Mwita Kyaro alifariki dunia saa 4 asubuhi jana katika hospitali ya Bugando alipokuwa akitibiwa.

Akieleza wasifu wa marehemu huyo, Mgawe alisema Jenerali Kyaro aliongoza jeshi hilo akiwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama (CDF) kati ya mwaka 1988 hadi 1994 alipostaafu.

“Jenerali Kyaro alistaafu akiwa amelitumikia jeshi kwa miaka 50, miezi 11 na siku 13,” alisema Mgawe na kufafanua kuwa jenerali huyo alizaliwa mwaka 1925, Kijiji cha Nyamwaga, Tarafa Igwe Tarime, mkoani Mara.

Tuesday 10 April 2012

R.I.P KANUMBA...TUTAKUKUMBUKA DAIMA

we will always miss u

Gari iliyobeba Mwili wa Marehemu Mpendwa wetu Steven C. Kanumba ikielekea viwanja vya Leaders Club asubuhi hii tayari kwa shughuli ya kuaga na mazishi.


RATIBA RASMI YA MAZISHI YA STEVEN KANUMBA LEO


Msanii wa filamu, aliyebeba mapenzi makubwa ya Watanzania, Waafrika na dunia kwa jumla, Steven Charles Kanumba aliyefikwa na mauti ghafla Aprili 7, 2012, atazikwa kesho Makaburi ya Kinondoni, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam.

Mazishi ya Kanumba, yamepangwa na kuratibiwa kwa kuzingatia heshima, umaarufu, mapenzi yake kwa watu na hadhi ya kimataifa aliyonayo, hivyo imetolewa fursa ya wengi kumuaga msanii huyo ambaye ni mwanamapinduzi wa tasnia ya filamu ukanda wote wa Afrika Mashariki na Kati.

Mpangilio wa ratiba na nafasi itatolewa kwa kila mtu mwenye kuhitaji kushiriki mazishi ya Kanumba, kufanya hivyo katika tukio la kihistoria la kumsindikiza ndugu yetu huyo kwenye maisha ya milele. Hivyo, wito unatolewa kwa kila mtu kujitokeza kwenye shughuli nzima.

RATIBA
Mwili wa marehemu Steven Kanumba utachukuliwa kwa msafara kutoka Hospitali ya Taifa, Muhimbili saa 2:30 asubuhi. Utapitishwa Barabara ya Umoja wa Mataifa na Ali Hassan Mwinyi hadi Viwanja vya Leaders Club, Kinondoni ambako Misa ya kumuombea itasomwa pamoja na salamu mbalimbali kabla ya watu wote kumuaga.
Wito unatolewa kwa watu kujitokeza kwa wingi kuanzia saa 2:00 asubuhi, wakijipanga kando ya Barabara za Umoja wa Mataifa na Ali Hassan Mwinyi ili wautolee heshima mwili wa Kanumba wakati ukitolewa Muhimbili kwenda Leaders Club.

Saa 3:30 asubuhi, mwili wa Kanumba utapokelewa Viwanja vya Leaders, ukitanguliwa na mapokezi ya wazazi wake, viongozi mbalimbali wa serikali ambao juu yao kabisa atakuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mohamed Gharib Bilal.
Saa 4:00, itakuwa ni muda wa kusoma Misa ambayo itachukua dakika 60, saa 5:00 kitakuwa kipindi cha salamu kutoka kwa watu mbalimbali.

Saa 6:00 mchana, ratiba ya kumuaga Kanumba itaanza mpaka saa 9:00 alasiri na baada ya hapo, utakuwa wakati wa kuusafirisha mwili kwa msafara kutoka Leaders Club mpaka Makaburi ya Kinondoni, msafara ukipita Barabara ya Tunisia, utakatisha Barabara ya Kinondoni kuelekea makaburini.

Saa 10:00 alasiri, mazishi yatafanyika kwa kufuata utaratibu wa imani ya marehemu.
Kamati ya Mazishi inatoa wito kwa watu watakaohudhuria shughuli ya kumzika ndugu yetu Kanumba, kuja na maua ili kumuaga kwa heshima.
Utulivu, unyenyekevu na ustahimilivu ni mambo muhimu yanayohitajika katika kipindi chote cha kumuaga mpendwa wetu Kanumba.

Bwana alitoa, Bwana ametwaa. Sisi wote tulimpenda kwa dhati na tulitamani aendelee kuwa nasi siku zote ila Mungu aliyemleta kwa mapenzi yake ameamua kumchukua. Jina lake lihimidiwe.

K.N.Y GABRIEL MTITU
MWENYEKITI WA KAMATI YA MAZISHI

MADAKTARI WAELEZA KILICHOMUUA KANUMBA


 Msanii nyota wa filamu nchini, Steven Kanumba amefariki kutokana na tatizo la mtikisiko wa ubongo linalojulikana kitaalamu kama BRAIN CONCUSSION, taarifa za kitabibu zimeeleza.

Taarifa hizo za ndani, zimepatikana jana baada ya jopo la madaktari bingwa watano wa hospitali ya taifa Muhimbili kuufanyia uchunguzi mwili wa marehem, zimeeleza kuwa tatizo hilo linaweza kumfanya mtu apoteze maisha mara moja au baada ya siku kadhaa.Mmoja wa madaktari hao ambae aliomba jina lake lisitajwe gazetini alisema waligundua tatizo hilo baada ya kumfanyia uchunguzi huo kwa zaidi ya masaa mawili.

"tulianza kuufanyia uchunguzi mwili wa marehemu kuanzia saa 4 asubuhi hadi saa 6:45 mchana na tukagundua kuwa marehemu alifariki kutokana na mtikisiko wa ubongo kwa kitaalamu Brain Concussion" alisema. Kanumba alipata mtikisko huo ambao husababisha kufeli kwa mfumo wa upumuaji (cardio-respiratory failure) "kilichomuua hasa ni mtikisiko wa ubongo, ambao endapo unatokea katika sehem ya nyuma ua ubongo (cerebram), huua kwa haraka" alisema daktari huyo na kuongeza kuwa mtikisiko wa ubongo wa nyuma husababusha matatizo ya mfumo wa upumuaji na hilo limeonekana katika mwili wake.

"Baada ya ubongo wake kutikiswa kwa nguvu, mfumo wa upumuaji unafeli na ndio maana tumekuta kucha za kanumba zikiwa na rangi ya blue, huku mapafu yake yakiwa yamevilia damu na kubadilika kuwa kama maini, hizo ni dalili za kufeli kwa mfumo wa upumuaji"

"Mtu aliepata mtikisko wa ubongo huweza kutokwa na mapovu mdomoni na hukoroma kabla ya kukata roho na ndivyo ilivyokuwa kwa Kanumba kabla hajafariki.

Daktari mwingine alieshiriki katika uchunguzi huo ambae pia aliomba jina lake lisitahwe alisema ubongo wa mwigizaji huyo umevimba na kushuka karibu na uti wa mgongo na hivyo kuathiri mfumo wa upumuaji. Alisema sehemu ya maini na maji maji ya machoni ya marehemu, vimepelekwa kwa mkemia mkuu wa Serikali ili kubaini endapo kuna sumu au kitu kingine katika mwili huo

GEITA DOCUMENTARY

Contributors