Wednesday 4 August 2021

MAKALA MAALUM.."HUU NDIO UKWELI" Afrika inaweza kuwa na "nguvu kubwa ya uchumi duniani"


        Mabadiliko katika mfumo wa dunia tangu kuingia kwa karne mpya, ikiwa ni pamoja na utulivu mkubwa wa hali ya kisiasa barani Afrika na kuongezeka kwa bidhaa muhimu, kama vikitumiwa vizuri, vitatoa fursa kwa Afrika kuwa nguvu kubwa ya uchumi duniani. Hayo yamo kwenye utangulizi wa Ripoti ya uchumi kuhusu Afrika inayoitwa "Kutumia vizuri bidhaa za Afrika: mabadiliko ya viwanda kwa ukuaji, ajira, na mageuzi ya kiuchumi" ulioandikwa na Carlos Lopes, naibu katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa ambaye pia ni mkurugenzi mtendaji wa Kamati ya Umoja wa Mataifa kuhusu uchumi wa Afrika akishirikiana na mwenyekiti wa Kamati ya Umoja wa Afrika, Nkosazana Dlamini-Zuma.
       Maofisa hao wamesema mabadiliko ya uchumi wa dunia na ya siasa za kijiografia katika miongo miwili iliyopita yamebadilisha muundo wa desturi ya makundi ya uchumi wa dunia, pia yameshuhudia kuibuka kwa nguvu mpya kutoka upande wa kusini. Mabadiliko haya yaliyochangiwa zaidi na mageuzi ya teknolojia ya habari na mawasiliano, yamesabaisha kuongezeka kwa muingiliano wa mitaji na biashara ya bidhaa za kati, hivyo kuonyesha wazi thamani kubwa ya kimantiki ya mzunguko huo. 
       Pia wamesema nchi za Afrika zina fursa kubwa ya kutumia vizuri rasilimali zilizo nazo na bei kubwa ya bidhaa katika soko la kimataifa, pia zinaweza kutumia fursa zinazotokana na mabadiliko ya uchumi wa dunia kuinua zaidi uchumi wao kupitia mageuzi ya viwanda na kukabiliana na umasikini, ukosefu wa usawa, na tatizo la ajira hasa kwa wasomi lukuki waliopo afrika na pia watu wenye elimu ya chini. Endapo fursa hizi zitatumiwa ipasavyo, zitaisaidia Afrika kuongeza uwezo wake wa ushindani, kupunguza kutegemea usafirishaji wa bidhaa ghafi na udhaifu unaotokana na mambo hayo, hivyo kuibuka kuwa nguzo muhimu ya ukuaji wa uchumi wa dunia.
       Ripoti hiyo imeongeza kuwa ili kutumia vizuri malighafi za Afrika, nchi za bara hilo zinatakiwa kuwa na mpango wa mfumo wa maendeleo na sera zinazofaa za biashara ambazo ni halisi. Aidha, ripoti hiyo imeweka wazi kuwa mbegu ya matatizo ya Afrika ilipandwa wakati wa ukoloni, lakini matatizo hayo yalizidi baada ya uhuru kutokana na kushindwa kwa sera za biashara zinazotoka nje ya nchi husika. Ripoti hiyo imetoa mfano wa miundombinu ya barabara na reli iliyojengwa wakati wa ukoloni ambayo ilikuwa ni maalum kwa kusafirisha madini na malighafi nyingine kueleka bandarini na kwenda Ulaya, na si kwa lengo la kuunganisha sehemu moja ya bara hilo na nyingine. Mpaka karne hii ya 21, hali hiyo bado inaendelea, kwa nchi hizo kusafirisha bidhaa ambazo nchi za Ulaya zilizotawala zinahitaji, na si kwa lengo la kuongeza thamani. 

GEITA DOCUMENTARY

Contributors