Friday 15 June 2012

BAJETI YA TANZANIA KWA MWAKA WA FEDHA 2012/2013



I   UTANGULIZI:
1.         Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu liweze kujadili na kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2012/2013.  Pamoja na hotuba hii, nimewasilisha vitabu vinne vya Bajeti vinavyoelezea takwimu mbalimbali za Bajeti. Kitabu cha Kwanza kinaelezea makisio ya mapato.   Kitabu cha Pili kinaelezea makisio ya matumizi ya kawaida kwa Wizara, Idara zinazojitegemea; Taasisi na Wakala wa Serikali; cha Tatu kinahusu makisio ya matumizi ya kawaida kwa Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa na cha Nne kinaelezea makadirio ya matumizi ya maendeleo kwa Wizara, Idara zinazojitegemea, Taasisi na Wakala za Serikali; Mikoa na
Mamlaka za Serikali za Mitaa. Aidha, upo Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2012 ambao ni sehemu ya Bajeti hii.

2.  Mheshimiwa Spika, awali ya yote, naomba nitumie fursa hii kumshukuru kwa dhati Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho
Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa imani kubwa aliyonayo kwangu kwa kuniteua kuwa Waziri wa Fedha. Naahidi kutekeleza majukumu niliyokabidhiwa kwa umakini na uaminifu mkubwa.

Thursday 14 June 2012

Vodacom Tanzania yalipa kodi ya mapato Sh700 bilioni


 
  KAMPUNI ya Mawasiliano ya Vodacom Tanzania inatarajia kuchangia jumla ya Sh130 bilioni kama malipo ya kodi kwa katika mwaka wa fedha 2012/13.

Malipo hayo yataifanya Vodacom kufikisha zaidi ya Sh700 bilioni ilizokwishalipa kama kodi tangu mwaka 2001.

Akizungumza jana na waandishi wa habari mjini hapa, baada ya kukutana na Spika wa Bunge, Anne Makinda, Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Rene Meza alisema malipo ya kodi kwa serikali yamefikia zaidi ya asilimia 60 ya jumla ya uwekezaji wa Vodacom wa Sh 1.13 trilioni tangu mwaka 2001.

Meza alisema kampuni yak ina mipango wa kutumia zaidi ya Sh120 bilioni katika kuboresha mtandao, huduma na maendeleo ya uanzishwaji wa teknolojia mpya katika mwaka wa 2012.

Alisisitiza dhamira ya kampuni hiyo katika kuendelea kulipa kodi ipasavyo kwa Mamlaka ya Kodi Tanzania (TRA) na Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA)

“Hivi punde tumeboresha mtandao kwa zaidi ya Sh100 bilioni kufikia mwishoni mwa Machi 2012, na tunao mpango wa kuwekeza zaidi ya Sh120 bilioni ili kuendelea kuimarisha mtandao wetu nchi nzima.

‘Vodacom pia imetengeneza ajira 450,000 ikiwa ni pamoja na za mawakala wa M- Pesa, wauzaji wa jumla na wadogo pamoja na waajiriwa wengine 450 wa moja kwa moja katika kampuni,” alisema Meza.

Aliongeza kuwa kampuni pia imetoa zaidi ya Sh3.4 bilioni kwa serikali kama mchango katika Mfuko wa Maendeleo ya Huduma za Mawasiliano Vijijini, wa kuisaidia jamii kuwa na mipango ya uwekezaji katika katika nyanja ya mazingira na wanyama pori, elimu, afya na ustawi wa jamii.

Pia alibainisha kuwa katika miaka mitano iliyopita, Kampuni imewekeza katika miradi ya huduma za jamii kupitia Vodacom Foundation, ambayo imefikia kiasi cha Sh5 bilioni na kwamba kiasi hicho kitaendelea kuongezeka kwa kuwa kampuni imedhamiria kuwekeza zaidi katika miradi ya maendeleo na huduma za jamii katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Vodacom inajivunia mafanikio katika kuunga mkono malengo ya Serikali ya kurahisisha huduma za kifedha kwa wananchi, ndani ya mwaka mmoja kati ya 2011 na 2012 ambapo Sh6.6 trilioni zilihamishwa katika njia ya M -PESA.

Wednesday 13 June 2012

BOB MAKANI KUZIKWA LEO



 
MAELFU ya wakazi wa Manispaa ya Shinyanga na makada wa Chadema, jana walijitokeza kwa wingi viwanja vya Shycom mjini hapa kutoa heshima zao za mwisho kwa muasisi wa chama hicho, Mohamed Bob Makani.
Chadema kilisema watamuenzi muasisi huyo kwa kuendeleza mapambano Bungeni, hususan katika Bunge la Bajeti ambalo limeanza jana.

Akizungumza mkoani hapa, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi,  John Mnyika, alisema wabunge wa chama hicho watamuenzi Bungeni kwa vitendo kwa kusimamia masuala aliyoyapa kipaumbele.

Mnyika alisema wataanza kumuenzi Makani katika mkutano wa Bunge unaoendelea kwa niaba ya wananchi wa Shinyanga na Watanzania kwa kusimamia haki, uwajibikaji na mabadiliko kwenye mfumo wa utawala, mambo ambayo  alikuwa akisisitiza wakati wa uhai wake.

Tuesday 12 June 2012

MAELFU WAMWAGA BOB MAKANI



 


RAIS Jakaya Kikwete ameongoza mamia ya waombolezaji kutoa heshima za mwisho kwa mwasisi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Bob Makani (76), aliyefariki dunia Jumamosi iliyopita.
Akizungumza katika shughuli hiyo, iliyofanyika kwenye Viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam, Rais Kikwete alisema mchango wa hayati Makani hasa katika nyanja za kisiasa na kiuchumi utakumbukwa daima na Watanzania.

“Aliitumia vizuri nafasi yake kama mwanasiasa, hali kadhalika, alipokuwa mfanyakazi wa umma katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), alikuwa mchapakazi,” alisema Rais Kikwete.
Katika hotuba yake fupi, Rais alieleza jinsi alivyozipata taarifa za msiba huo mkubwa na jinsi alivyoguswa kwa kumpoteza mwanasiasa mkongwe.... “Binadamu anaweza kupata urefu au ufupi, unene au wembamba, lakini kifo ni cha kila mtu.”

Mbowe: mfumo ulimsaliti Makani
Akimzungumzia hayati Makani, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema alikuwa ni mwanasiasa mahiri na mkweli, lakini mfumo wa kisiasa Tanzania haukumpa fursa ya kupata nafasi ya uongozi kitaifa.

Alisema, Makani aligombea ubunge zaidi ya mara mbili lakini hakuwahi kushinda kwa kile ambacho Mbowe alidai kuwa ni tatizo la mfumo.

“Bob alikuwa akishinda katika kila chaguzi, lakini mfumo haukumkubali,” alidai.
Mwenyekiti huyo alishauri kuwa Katiba Mpya haina budi kuwaangalia watu muhimu wenye kazi zilizotukuka ili wawepo bungeni kwa ajili ya kutoa mawazo, ushauri na hekima zao pamoja na kuwaenzi.

“Wapo wanasiasa wengi, wengine ni waongo na wasiotekeleza ahadi zao lakini wanaingia bungeni, lakini pia wapo wanasiasa werevu na wa kweli, ila tu wanakosa fursa za kuongoza,” alisema Mbowe.
Katika hotuba yake, Mbowe alikumbuka nyakati muhimu za marehemu Makani alizowahi kuzishuhudia ikiwemo kutoa hotuba fupi kuliko zote katika moja ya kampeni zake za kugombea ubunge huko Shinyanga.

“Katika kampeni hiyo, Makani alitoa hotuba fupi pengine kuliko zote. Alinyoosha mikono yake na kusema, ‘Nawapenda’ kisha akamaliza” alisema Mbowe

Mtei amlilia
Mwasisi wa Chadema, Edwin Mtei aliyeanzisha chama hicho pamoja na Makani alisema taifa limepoteza nguzo imara wakati huu likiwa katika mchakato wa mabadiliko muhimu ya nchi.
Hotuba hiyo ya Mtei iliyosomwa kwa niaba yake na Mzee wa Chadema, Victor Kimesera ilieleza historia ya wawili hao wakiwa wanafunzi katika Shule ya Sekondari Tabora na baadaye wafanyakazi wa BoT.
“Mimi na Makani tumekutana mwaka 1951 na tangu wakati huo tumekuwa pamoja tukishirikiana katika mambo mengi,” alisema Mtei.

Slaa: ni pengo lisilozibika
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alimtaja marehemu Makani kuwa mtu jasiri ambaye alianzisha chama cha upinzani hasa enzi zile ambazo upinzani ulionekana kama uhaini... “Alikuwa ni mtu ambaye haogopi, alisema hadharani kile alichokiona kinafaa.”

Dk Slaa alisema japokuwa Makani alikuwa mgonjwa na umri wake kuwa mkubwa, lakini bado aliendelea kufanya kazi za chama bila makosa.

“Unaweza kumuamsha Makani usiku wa manane na akafanya kazi za chama. Kwetu sisi hili ni pigo kwani tumempoteza mshauri na jemedari wa jeshi la kuleta mabadiliko.”

Wengine waliotoa hotuba katika hafla hiyo ni mwakilishi wa vyama vya upinzani, Profesa Ibrahim Lipumba (CUF) ambaye alimtaja marehemu kama mchezaji wa mpira hodari na mwerevu.

“Nilisoma na Makani shule moja, ingawa aliniacha kwa miaka mingi. Alikuwa ni mchezaji hodari na mwerevu,” alisema Profesa Lipumba.

Alimtaja hayati Makani kuwa ni Mtanzania mzalendo aliyejitoa kwa kiasi kikubwa kuifikisha nchi ilipo hasa katika mchakato wa kuleta Katiba Mpya.

Naibu Gavana wa BoT, Dk Natu Mwamba alisema taasisi hiyo haitamsahau kamwe Makani kutokana na uchapaji kazi wake na kuishi vizuri na wafanyakazi wengine.

Alisema aliteuliwa kuwa Naibu Gavana wa BoT mwaka 1966 na alikuwa ni mmoja wa maofisa waliofanya kazi kubwa katika kushughulikia tatizo la kuungua kwa Benki Kuu miaka ya 1970.
Mwili wa Makani ambaye alizaliwa mwaka 1936, ulisafirishwa jana jioni kwa ndege kwenda Shinyanga kwa mazishi.

Makani ilianza kupata matatizo ya kiafya katika miaka ya karibuni na wakati wa uzinduzi wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2010 katika Viwanja vya Jangwani, Dar es Salaam, aliishiwa nguvu na kudondoka. Alisimama baadaye na kuwasalimia wananchi.

Pia Januari 17, mwaka huu katika msiba wa aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Regia Mtema alianguka tena muda mfupi baada ya kuaga mwili wa marehemu.

Wasifu
Marehemu Makani alizaliwa mwaka 1936 huko Kolandoto, Shinyaga.
Alianza darasa la kwanza akiwa na umri wa miaka sita, mwaka 1942 katika Shule ya Ibadakuli, hukohuko Shinyanga.

Alijiunga na Shule ya Sekondari ya Tabora ambako alifaulu vizuri na kuchaguliwa kujiunga na Chuo Kikuu cha Makerere, Uganda.

Alipata shahada ya pili ya sheria katika Chuo Kikuu cha Liverpool, Uingereza.
Mwaka 1965 alirejea nchini na kuajiriwa katika utumishi wa umma akiwa Mwanasheria wa Serikali.
Hakudumu katika nafasi hiyo kwani alipandishwa cheo na kuteuliwa kuwa Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania wakati huo, Edwin Mtei, akiwa ni Gavana.

Mwaka 1991-92 wakati vuguvugu la mfumo wa vyama vingi likianza, Makani akishirikiana na Mtei walianzisha Chadema.Namba ya kadi ya uanachama ya Makani ilikuwa ni tatu.
Mwaka 1991 alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa kwanza wa Chadema na mwaka 1995 aliteuliwa kuwa Mwenyekiti nafasi aliyoishika hadi 2005 alipostaafu.

Baada ya kustaafu, Makani alibaki kuwa mshauri na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya chama hicho.
Vyeo vingine alivyowahi kushika ni pamoja na Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mkurugenzi wa Kiwanda cha Bia Tanzania (TBL) na Mkurugenzi wa Kampuni ya Uwakili ya “Makani and Adovacate Company.’

Makani alifariki dunia katika Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam Jumamosi iliyopita, baada ya kuugua maradhi ya moyo yaliyomsumbua tangu mwaka 2009.

Monday 11 June 2012

Makani kuzikwa Shinyanga



 
MWILI wa Mwasisi wa Chadema, Ali Makani au maarufu kwa jina la Bob Makani (76) ambaye alifariki dunia juzi usiku, unaagwa leo Dar es Salaam na utazikwa keshokutwa katika Kijiji cha Negesi, Wilaya ya Kishapu, Shinyanga.
Bob Makani ambaye alikuwa akiugua kwa muda mrefu, alifariki juzi saa 4.15 usiku katika Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam alikopelekwa baada ya kuzidiwa ghafla.
Mtoto wa Marehemu, Mohamed Makani aliwaambia waandishi wa habari nyumbani kwa marehemu, Mbezi Beach kwamba mwili wa marehemu utaagwa leo katika Ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam.
Alisema baada ya mwili huo kuagwa, utapelekwa katika Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere tayari kwa kusafirishwa kesho.
“Bado hatujafahamu mwili utaagwa kuanzia saa ngapi katika Ukumbi wa Karimjee, lakini tutaendelea kuwafahamisha wananchi baada ya mawasiliano ya wanafamilia,” alisema.
Alisema marehemu baba yake, alikuwa akisumbuliwa na kibofu cha mkojo na moyo.
“Aliwahi kupelekwa India kwa ajili ya matibabu ya moyo na Aprili mwaka huu nilimpeleka Kenya ambako alifanyiwa operesheni ya kibofu,” alisema.
Mohamed alisema baba yake aliumwa kwa muda mrefu na mara kadhaa alilazwa katika hospitali mbalimbali na kuruhusiwa.
Akizungumzia utabiri wa baba yake, alisema mara kwa mara alikuwa akisema CCM ni chama ambacho kimekufa na kilichobakia ni kuizika.
“Amekuwa akiitabiria Chadema kuwa ni chama kitakachotawala katika nchi hii na mara kwa mara amekuwa akisema mwisho wa CCM sasa umefika,” alisema Mohamed.
Akizungumzia michezo alisema marehemu enzi za uhai wake alikuwa mpenzi wa timu ya Liverpool ya Uingereza.
“ Hakuwa akizipenda timu kubwa za Yanga na Simba, bali alikuwa mpenzi mkubwa wa timu ya Liverpool ya Uingereza,” alisema.
Bendera za Chadema nusu mlingoti
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika alisema chama hicho kimepokea taarifa za kifo hicho kwa masikitiko na kimeamua kupeperusha bendera zake nusu mlingoti kwa siku saba.
Akitoa taarifa za awali, Mnyika alisema viongozi wa chama hicho waliokuwa katika Operesheni Okoa mikoa ya Kusini wamekatisha ziara na walitarajiwa kuwasili Dar es Salaam jana jioni.
“Operesheni hii ilitakiwa kumalizika kesho (Juni 12, mwaka huu), lakini kutokana na kifo hicho cha mwasisi wa Chadema tumeamua kuisitisha na viongozi wako njiani kurejea Dar es Salaam,” alisema Mnyika.
Akitoa taarifa za awali baada ya kuwasiliana na familia ya marehemu, Mnyika alisema atazikwa kwa heshima zote za Chadema na za dini ya Kiislamu.
Alisema kitabu cha maombolezo kitakuwa katika ofisi za Makao Makuu ya Chadema zilizopo Kinondoni, Dar es Salaam.
Mnyika alisema mipango mingine ya mazishi inaendelea kufanyika katika eneo la Uzunguni, mkoani Shinyanga.
“ Hizi ni taarifa za awali, wakifika viongozi wa ngazi za juu tutaendelea kuwapa taarifa kwa kadri tutakavyojadiliana,” alisema.
Profesa Baregu
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Profesa Baregu alisema anamkumbuka marehemu Bob Makani kama mwasisi wa mageuzi ambaye alikuwa shupavu na mwaminifu katika kukijenga chama hicho.
“Chama kitaendelea kukua kwa kasi kama wanachama wake watawaiga waasisi wake kama alivyofanya marehemu Bob Makani enzi za uhai wake,” alisema.
Profesa Baregu alisema hata kipindi alichokuwa akiumwa, aliendelea kuonekana kwenye shughuli za chama.
JK atuma salamu za rambirambi
Rais Jakaya Kikwete ametuma salamu za rambirambi kwa familia ya marehemu Bob Makani.
Katika salamu zake, Rais Kikwete alisema amehuzunishwa na kusikitishwa na taarifa za kifo cha Mzee Makani.
Alisema marehemu enzi za uhai wake alilitumikia taifa kwa uadilifu na uzalendo katika nafasi zote alizozishika ikiwamo ya Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
“Nimepokea kwa huzuni na masikitiko habari za kifo cha Mzee Makani ambaye nimejulishwa kuwa aliaga dunia usiku wa kuamkia jana katika Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam,” alisema Rais Kikwete.
Alisema alimfahamu Bob Makani kama mtumishi mwadilifu wa umma, sifa ambazo alizithibitisha katika nafasi zote alizozishikilia katika utumishi wa umma ama kwenye siasa.”
“Nawatumieni salamu za rambirambi za dhati ya moyo wangu, nikiwajulisheni kuwa niko nanyi katika msiba huu mkubwa ambao umewaondolea mpendwa wenu, baba yenu, babu yenu na mhimili wa familia yenu,” alisema.
Wasifu 
Siasa: Alikuwa Katibu Makuu wa kwanza wa Chadema kati ya mwaka 1993 hadi 1998, alikuwa Mwenyekiti wa chama hicho kuanzia mwaka 1998 hadi 2004 na amegombea ubunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini kwa mara tatu kati ya mwaka 1995 na 2000 na mwaka 2005.
Kazi serikalini: Alikuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), mwaka 1966
Elimu: Ana shahada ya sheria kutoka Chuo Kikuu Cha Makarere, Uganda.
Kulizaliwa: Ni mzaliwa wa Kijiji cha Korandoto, wilayani Kishapu, Shinyangaakitokea kwenye ukoo wa kichifu wa Makani.

Mawaziri Kenya wafariki ajali ya helikopta





WAZIRI wa Usalama wa Ndani Kenya, Profesa George Saitoti na Naibu wake, Orwa Ojode pamoja na maofisa wengine watano, wamefariki dunia baada ya helikopta ya Polisi waliyokuwa wamepanda kuanguka msituni.
Profesa Saitoti ambaye ni mmoja wa mawaziri waandamizi katika Serikali ya Rais Mwai Kibaki na mmoja wa wanasiasa wakongwe wanaoheshimika Kenya, aliwahi pia kuwa Makamu wa Rais kati ya mwaka 1976 hadi 1979 na alishatangaza kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwakani.

GEITA DOCUMENTARY

Contributors