Wednesday, 20 June 2012

SCF kusaidia wasindika vyakula



WAJASIRIAMALI wanaosindika vyakula na vinywaji visivyo na kileo Kanda ya Ziwa, wanatarajiwa kunufaika zaidi baada ya Mfuko wa Kukuza na Kuendeleza Ushindani wa Wajasiriamali (SCF) Tanzania, kuzindua mfumo wa taarifa kwa ajili yao.

Akizungumza katika uzinduzi huo jana, Mkurugenzi wa SCF, Casmir Makoye, alisema mfumo huo utawarahisishia wajasiriamali hao kufikia masoko makubwa yenye viwango vya kimataifa, yaliyopo Dar es Salaam na Zanzibar.

“Mfumo huu utawasaidia wajasiriamali kupata taarifa za vituo vya wanunuzi wa bidhaa zao, hivyo kujitathmini kwa kuchagua vituo vya wanunuzi wanavyovutiwa navyo kwa ajili ya kupata faida ya kuridhisha,” alisema Makoye.

Makoye alisema mfumo huo utawezesha wajasiriamali kuwasiliana moja kwa moja na vituo vya wanunuzi, kujua maeneo vilipo na idadi ya watu wanaotumia bidhaa wanazotengeneza.
“Pia, mfumo huu utawapunguzia wajasiriamali gharama za kutafuta masoko makuu yanayothamini ubora wa bidhaa, hivi sasa tunalenga wanaoweza kukidhi viwango vya masoko makubwa yenye tija kwa wajasiriamali,” alisema.

Alisema hadi sasa SCF kupitia mfumo wake wa taarifa, una uwezo wa kuwawezesha wajasiriamali kufikia vituo 14,904 vya wanunuzi wa vyakula na vinywaji visivyo na kileo mikoa ya Dar es Salaam na Zanzibar.

Wajasiriamali kutoka mikoa ya Mwanza, Mara, Kagera na Shinyanga, waliohudhuria uzinduzi huo walilezea kufurahia ujio wa mfumo huo, huku wakiwa na matarajio ya kukuza uchumi wao kutokana na uzalishaji na uzindikaji vyakula na vinywaji mbalimbali visivyo na kileo.

Bidhaa hizo ni matunda, kahawa, maziwa, nyama, sukari, samaki, maji, asali, mboga za majani na nafaka mbalimbali kama vile mchele, mahindi, mtama, ulezi, karanga, ufuta na dengu.

Akibainisha manufaa ya huduma ya POS database kwa mjasiriliamali, Meneja Biashara wa SCF Kanda ya Ziwa, Djaluo Franco, alisema itamrahisishia msindikaji kupanga jinsi ya kufikia eneo kubwa kulingana na kiwango cha uzalishaji wake, hatua ambayo itamsaidia kupunguza gharama za usafirishaji.

“Pili, inamrahisishia kuona ni maeneo gani pengine yana wasambazaji wachache ambao wana bidhaa yanayofanana na yake, ili kusudi aweze kupeleka huko... inamsaidia sana kulenga njia ya usambazaji,” alisema Franco na kuongeza:

“Akitumia matokeo ya hii POS,  inamsaidia vilevile kujua bidhaa ambazo haziko sokoni ama ziko kwa uchache sana na ikamfanya abadilishe aina ya bidhaa anazoziuza baada ya kuona pengo katika soko.”

No comments:

GEITA DOCUMENTARY

Contributors