MWILI wa Mwasisi wa Chadema, Ali Makani au maarufu kwa jina la Bob Makani (76) ambaye alifariki dunia juzi usiku, unaagwa leo Dar es Salaam na utazikwa keshokutwa katika Kijiji cha Negesi, Wilaya ya Kishapu, Shinyanga.
Bob Makani ambaye alikuwa akiugua kwa muda mrefu, alifariki juzi saa 4.15 usiku katika Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam alikopelekwa baada ya kuzidiwa ghafla.Mtoto wa Marehemu, Mohamed Makani aliwaambia waandishi wa habari nyumbani kwa marehemu, Mbezi Beach kwamba mwili wa marehemu utaagwa leo katika Ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam. Alisema baada ya mwili huo kuagwa, utapelekwa katika Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere tayari kwa kusafirishwa kesho. “Bado hatujafahamu mwili utaagwa kuanzia saa ngapi katika Ukumbi wa Karimjee, lakini tutaendelea kuwafahamisha wananchi baada ya mawasiliano ya wanafamilia,” alisema. Alisema marehemu baba yake, alikuwa akisumbuliwa na kibofu cha mkojo na moyo. “Aliwahi kupelekwa India kwa ajili ya matibabu ya moyo na Aprili mwaka huu nilimpeleka Kenya ambako alifanyiwa operesheni ya kibofu,” alisema. Mohamed alisema baba yake aliumwa kwa muda mrefu na mara kadhaa alilazwa katika hospitali mbalimbali na kuruhusiwa. Akizungumzia utabiri wa baba yake, alisema mara kwa mara alikuwa akisema CCM ni chama ambacho kimekufa na kilichobakia ni kuizika. “Amekuwa akiitabiria Chadema kuwa ni chama kitakachotawala katika nchi hii na mara kwa mara amekuwa akisema mwisho wa CCM sasa umefika,” alisema Mohamed. Akizungumzia michezo alisema marehemu enzi za uhai wake alikuwa mpenzi wa timu ya Liverpool ya Uingereza. “ Hakuwa akizipenda timu kubwa za Yanga na Simba, bali alikuwa mpenzi mkubwa wa timu ya Liverpool ya Uingereza,” alisema. Bendera za Chadema nusu mlingoti Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika alisema chama hicho kimepokea taarifa za kifo hicho kwa masikitiko na kimeamua kupeperusha bendera zake nusu mlingoti kwa siku saba. Akitoa taarifa za awali, Mnyika alisema viongozi wa chama hicho waliokuwa katika Operesheni Okoa mikoa ya Kusini wamekatisha ziara na walitarajiwa kuwasili Dar es Salaam jana jioni. “Operesheni hii ilitakiwa kumalizika kesho (Juni 12, mwaka huu), lakini kutokana na kifo hicho cha mwasisi wa Chadema tumeamua kuisitisha na viongozi wako njiani kurejea Dar es Salaam,” alisema Mnyika. Akitoa taarifa za awali baada ya kuwasiliana na familia ya marehemu, Mnyika alisema atazikwa kwa heshima zote za Chadema na za dini ya Kiislamu. Alisema kitabu cha maombolezo kitakuwa katika ofisi za Makao Makuu ya Chadema zilizopo Kinondoni, Dar es Salaam. Mnyika alisema mipango mingine ya mazishi inaendelea kufanyika katika eneo la Uzunguni, mkoani Shinyanga. “ Hizi ni taarifa za awali, wakifika viongozi wa ngazi za juu tutaendelea kuwapa taarifa kwa kadri tutakavyojadiliana,” alisema. Profesa Baregu Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Profesa Baregu alisema anamkumbuka marehemu Bob Makani kama mwasisi wa mageuzi ambaye alikuwa shupavu na mwaminifu katika kukijenga chama hicho. “Chama kitaendelea kukua kwa kasi kama wanachama wake watawaiga waasisi wake kama alivyofanya marehemu Bob Makani enzi za uhai wake,” alisema. Profesa Baregu alisema hata kipindi alichokuwa akiumwa, aliendelea kuonekana kwenye shughuli za chama. JK atuma salamu za rambirambi Rais Jakaya Kikwete ametuma salamu za rambirambi kwa familia ya marehemu Bob Makani. Katika salamu zake, Rais Kikwete alisema amehuzunishwa na kusikitishwa na taarifa za kifo cha Mzee Makani. Alisema marehemu enzi za uhai wake alilitumikia taifa kwa uadilifu na uzalendo katika nafasi zote alizozishika ikiwamo ya Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT). “Nimepokea kwa huzuni na masikitiko habari za kifo cha Mzee Makani ambaye nimejulishwa kuwa aliaga dunia usiku wa kuamkia jana katika Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam,” alisema Rais Kikwete. Alisema alimfahamu Bob Makani kama mtumishi mwadilifu wa umma, sifa ambazo alizithibitisha katika nafasi zote alizozishikilia katika utumishi wa umma ama kwenye siasa.” “Nawatumieni salamu za rambirambi za dhati ya moyo wangu, nikiwajulisheni kuwa niko nanyi katika msiba huu mkubwa ambao umewaondolea mpendwa wenu, baba yenu, babu yenu na mhimili wa familia yenu,” alisema. Wasifu Siasa: Alikuwa Katibu Makuu wa kwanza wa Chadema kati ya mwaka 1993 hadi 1998, alikuwa Mwenyekiti wa chama hicho kuanzia mwaka 1998 hadi 2004 na amegombea ubunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini kwa mara tatu kati ya mwaka 1995 na 2000 na mwaka 2005. Kazi serikalini: Alikuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), mwaka 1966 Elimu: Ana shahada ya sheria kutoka Chuo Kikuu Cha Makarere, Uganda. Kulizaliwa: Ni mzaliwa wa Kijiji cha Korandoto, wilayani Kishapu, Shinyangaakitokea kwenye ukoo wa kichifu wa Makani. |
Monday, 11 June 2012
Makani kuzikwa Shinyanga
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment