Wednesday 13 June 2012

BOB MAKANI KUZIKWA LEO



 
MAELFU ya wakazi wa Manispaa ya Shinyanga na makada wa Chadema, jana walijitokeza kwa wingi viwanja vya Shycom mjini hapa kutoa heshima zao za mwisho kwa muasisi wa chama hicho, Mohamed Bob Makani.
Chadema kilisema watamuenzi muasisi huyo kwa kuendeleza mapambano Bungeni, hususan katika Bunge la Bajeti ambalo limeanza jana.

Akizungumza mkoani hapa, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi,  John Mnyika, alisema wabunge wa chama hicho watamuenzi Bungeni kwa vitendo kwa kusimamia masuala aliyoyapa kipaumbele.

Mnyika alisema wataanza kumuenzi Makani katika mkutano wa Bunge unaoendelea kwa niaba ya wananchi wa Shinyanga na Watanzania kwa kusimamia haki, uwajibikaji na mabadiliko kwenye mfumo wa utawala, mambo ambayo  alikuwa akisisitiza wakati wa uhai wake.

“Wakati wa uhai wake Mzee Makani alikuwa akisema anawapenda Watanzania kila mara, hivyo tuendelee kumuombea kama ambavyo alitupenda ili jina lake liendelee kudumu siku zote,” alisema.
Mnyika alisema hayo baada ya wananchi kupaza sauti ya kutaka apewe nafasi ya kuzungumza wakati wa kutoa heshima ya mwisho kwa mwili wa marehemu.

Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini wa Chadema, Silyvesta Masinde, alisema kuzikwa kwa muasisi wa Chadema ni ishara ya kuzikwa kwa CCM, kwa vile misingi aliyoiacha bado wataendelea kuisimamia.
Masinde alisema licha ya kupoteza nguvu muhimu katika chama, hawatorudi nyumba bali watazidi kusonga mbele, kutokana na misingi waliyoachiwa.

Alisema mchango wa Makani katika chama ulikuwa ni mkubwa na ulikisaidia kuwa taasisi, jambo ambalo limekuwa likiwasaidia k utatua migogoro ya ndani na kitaifa.
Makamu Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Said Amour Arfi, alisema kufariki kwa Makani ni pigo kwa vile chama kimepoteza nguvu kazi na kubainisha kuwa alikuwa mwadilifu, huku akiomba wananchi na wafuasi wao kuzingatia mafundisho yake.

Kwa upande wake, Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga, Aloysius Balina, alisema amekuwa akimkumbuka Makani kwa sala kutokana na mchango wake kwa jamii na kuahidi kuendelea kumuombea zaidi.
Naye Mkurugenzi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Edda Balele, alisema wao wanamtambua Makni kama kiongozi aliyekuwa akionyesha njia na uzalendo kwenye uamuzi wake na kwamb, licha ya tayari alikuwa ameacha kazi, walipomhitaji aliwasaidia mawazo.

Viongozi wengine waliokuwapo ni Mbunge wa zamani wa Shinyanga Mjini,  Leonard Derefa, Meya wa Manispaa ya Shinyanga, Gulamu Hafidhi, Katibu wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Adamu Ngallawa na Katibu Tawala wa Mkoa (Ras), Ancelin Ntalimo.

Wengine ni Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Katibu Mkuu wake, Dk Willibrod Slaa, Naibu katibu mkuu, Zitto Kabwe, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu. Makani anatarajiwa kuzikwa leo nyumbani kwao, Kijiji cha Negezi, wilayani Kishapu.

No comments:

GEITA DOCUMENTARY

Contributors