Siku ya Jumatatu tarehe 26/04/2011, Tanzania itaadhimisha miaka 47 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulioasisiwa tarehe 26/04/1964 kwa yaliyokuwa Mataifa mawili, Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar kuungana na kuzaliwa Taifa moja la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete atakuwa mgeni rasmi katika kilele cha Maadhimisho ya sherehe hizo Mwaka huu ambazo kitaifa zitafanyika kwenye Uwanja wa Amaan Mjini Zanzibar.
Mbali na Rais Kikwete, Viongozi mbalimbali wa Kitaifa,Mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa nchini pamoja na wananchi kutoka Mikoa mbalimbali wanatarajiwa kushiriki katika Maadhimisho hayo.
Mkataba wa Muungano ulitiwa saini na aliyekuwa Rais wa Tanganyika, Marehemu Mwalimu Julius KambarageNyerere na aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Marehemu Sheikh Abeid Amani Karume tarehe 22 Aprili 1964 Zanzibar.
Siku ya Jumatatu tarehe 26 Aprili, 1964, viongozi wa nchi zote mbili walikutana katika ukumbi wa Karimjee Jijini Dar es Salaam na kubadilishana Hati za Muungano.