Thursday, 14 June 2012

Vodacom Tanzania yalipa kodi ya mapato Sh700 bilioni


 
  KAMPUNI ya Mawasiliano ya Vodacom Tanzania inatarajia kuchangia jumla ya Sh130 bilioni kama malipo ya kodi kwa katika mwaka wa fedha 2012/13.

Malipo hayo yataifanya Vodacom kufikisha zaidi ya Sh700 bilioni ilizokwishalipa kama kodi tangu mwaka 2001.

Akizungumza jana na waandishi wa habari mjini hapa, baada ya kukutana na Spika wa Bunge, Anne Makinda, Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Rene Meza alisema malipo ya kodi kwa serikali yamefikia zaidi ya asilimia 60 ya jumla ya uwekezaji wa Vodacom wa Sh 1.13 trilioni tangu mwaka 2001.

Meza alisema kampuni yak ina mipango wa kutumia zaidi ya Sh120 bilioni katika kuboresha mtandao, huduma na maendeleo ya uanzishwaji wa teknolojia mpya katika mwaka wa 2012.

Alisisitiza dhamira ya kampuni hiyo katika kuendelea kulipa kodi ipasavyo kwa Mamlaka ya Kodi Tanzania (TRA) na Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA)

“Hivi punde tumeboresha mtandao kwa zaidi ya Sh100 bilioni kufikia mwishoni mwa Machi 2012, na tunao mpango wa kuwekeza zaidi ya Sh120 bilioni ili kuendelea kuimarisha mtandao wetu nchi nzima.

‘Vodacom pia imetengeneza ajira 450,000 ikiwa ni pamoja na za mawakala wa M- Pesa, wauzaji wa jumla na wadogo pamoja na waajiriwa wengine 450 wa moja kwa moja katika kampuni,” alisema Meza.

Aliongeza kuwa kampuni pia imetoa zaidi ya Sh3.4 bilioni kwa serikali kama mchango katika Mfuko wa Maendeleo ya Huduma za Mawasiliano Vijijini, wa kuisaidia jamii kuwa na mipango ya uwekezaji katika katika nyanja ya mazingira na wanyama pori, elimu, afya na ustawi wa jamii.

Pia alibainisha kuwa katika miaka mitano iliyopita, Kampuni imewekeza katika miradi ya huduma za jamii kupitia Vodacom Foundation, ambayo imefikia kiasi cha Sh5 bilioni na kwamba kiasi hicho kitaendelea kuongezeka kwa kuwa kampuni imedhamiria kuwekeza zaidi katika miradi ya maendeleo na huduma za jamii katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Vodacom inajivunia mafanikio katika kuunga mkono malengo ya Serikali ya kurahisisha huduma za kifedha kwa wananchi, ndani ya mwaka mmoja kati ya 2011 na 2012 ambapo Sh6.6 trilioni zilihamishwa katika njia ya M -PESA.

No comments:

Inspirational Prayer of the Day

choose your favorite language

GEITA DOCUMENTARY

HABARI NYINGINE ZAIDI