Wednesday, 15 April 2015
Kila kitu kinawezekana,, Hivi ndivyo Shule ya Jangwani ilivyoshinda tuzo ya ujasiriamali..
MAKALA YA MWANANCHI.
Wanafunzi wa shule ya wasichana ya Jangwani wakionyesha baadhi ya kazi wanazojifunza. Picha na Maimuna Kubegeya |
Programu ya mafunzo ya ujasiriamali kwa wanafunzi, ni malumu kwa ajili ya kuwaandaa kuingia kwenye dunia ya biashara
Hivi karibuni, Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Jangwani,
iliibuka mshindi kwenye shindano la ujasiriamali kwa ajili ya wanafunzi
wa shule za sekondari za jijini Dar es Salaam.
Shindano hilo lilitokana na mafunzo ya miezi
mitatu kuhusu ujasiriamali yaliyokuwa yakitolewa kwa wanafunzi wa shule
zaidi ya 10 za jijini humo na Taasisi isiyo ya kiserikali ya Junior
Achievment Tanzania (JAT).
Kufikia kilele cha mafunzo hayo, shule
zilizoshiriki zilipata wasaa wa kushindana na hatimaye, Jangwani
iliibuka kinara na kujishindia nafasi ya kuiwakilisha Tanzania kwenye
mashindano ya kimataifa yatakayofanyika nchini Gabon Disemba mwaka huu.
Nafasi ya pili ilichukuliwa na Shule ya Benjamin Mkapa, huku Chuo cha Ufundi Stadi Kipawa kikichukua nafasi ya tatu.
Shule nyingine zilizoshiriki ni pamoja na Shule za
sekondari za Pugu , Kibasila, Middland, Tegeta na Jitegemee pamoja na
vyuo vya Paradgims, Chuo cha Ufundi Stadi Kipawa na Chang’ombe.
Mkurugenzi wa kampuni E-Smart Creators ya
Jangwani, Sonia Apolo, anasema kuwa siri pekee ya ushindi wao ni ule
ubunifu waliotumia katika kutengeneza bidhaa yao ya kipekee.
“Mkaa wa makaratasi ndio bidhaa iliyotupa ushindi
na hata kuweza kupata nafasi hii. Tulitumia muda wetu mwingi kujifunza
tukiwa kwenye programu hii ya mafunzo na baada ya kufuzu, tuliuingiza
kwenye biashara” anasema na kuongeza:
“Mkaa huu unatumika kwa kupikia na hata kuongeza
joto majumbani kwa maeneo yenye baridi, hivyo mipango yetu ya baadaye ni
kuhakikisha bidhaa yetu inawafikia Watanzania wengi.”
Pamoja na bidhaa hii ya kipekee, shule ya Jangwani
ilionyesha bidhaa zake nyingine walizoziingiza sokoni ikiwa ni baada ya
kuuza hisa na kupata mtaji wa kuendesha biashara yao.
Miongoni mwa bidhaa hizo zilikuwa ni pamoja na fulana zilizochapishwa nembo ya kampuni yao, bangili, hereni na vifaa vya shule.
Shindano la ujasiriamali
Mratibu wa programu hiyo, Hamis Kasongo anasema
kuwa shindano hilo ni miongoni mwa programu za kawaida zinazoendeshwa na
taasisi yake, zikilenga kumtayarisha kijana wa Kitanzania kuingia
kwenye ulimwengu wa biashara, huku akijua thamani halisi ya pesa na
matumizi yake.
“Tumekuwa tukiendesha programu mbalimbali kwa vijana wa rika
tofauti tofauti. Baadhi yake ni pamoja na program ya kampuni, ‘Its
tyme’, Job shadow na nyingine nyingi zikiwa na nia ya kumuandaa kijana
kupambana na ulimwengu wa kibiashara” anafafanua.
Anasema kuwa wanafunzi hufundishwa jinsi ya
kuendesha kampuni, wakianza kujitengenezea mfumo wa kampuni na baadaye
kununua hisa zinazowawezesha kuanzisha mradi utakaweza kuwaingizia pesa.
Katika mfumo huo, anasema kunakuwa na wakurugenzi
na pia mameneja wanaoratibu kazi za kila siku na hatimaye kufanikiwa
kutengeneza faida.
Program hiyo inayoendeshwa kwa miezi mitatu pia
hutoa fursa kwa vijana hao kujifunza jinsi ya kuandika michanganuo ya
kibishara na pia ripoti wakati wa kufunga hesabu za kampuni.
Meneja wa masoko wa benki ya Baclays, ambao ndio
wadhamini wa program hiyo, Joel Bendera, anasema kuwa mpango wao ni
kuhakikisha vijana wengi zaidi wanapata mafunzo hayo, kwani licha ya
kuwapanua kiuelewa, yatasaidia kuwapa ujasiri wa kujiajiri mara
wamalizapo masomo yao.
“Tangu kuanzishwa kwa programu hii mwaka 1998,
tumekuwa mstari wa mbele kuhakikisha vijana wengi zaidi wanafikiwa.
Tutahakikisha kila mwaka tunakuwa bega kwa bega na JAT, ili kufikia
malengo yetu” anaeleza,
Ushuhuda
Issac Uswege ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe,tawi la Mbeya ambaye ni miongoni mwa wanafunzi waliopitia programu hiyo.
“Nilifanya programu hii nikiwa Shule ya Sekondari
Tambaza wakati ule nilitekeleza majukumu kama mkurugenzi. Nikiwa katika
wadhifa wangu huo nilifanikiwa kutengeneza mikakati iliyoboresha kampuni
yetu na hata kufanikiwa kupata ushindi kwenye mashindano kama haya”
anafafanua
Anasema mafunzo hayo yalimjenga kiujasiriamali
hata kumshawishi kufungua biashara yake binafsi mara baada ya kumaliza
kidato cha sita.
“Nilianza na biashara ya pikipiki na baadaye
niliziuza na kununua bajaji. Nilianza kufanya biashara wakati nasubiri
matokeo yangu lakini hata baada ya kutoka matokeo na kufaulu, bado
niliendelea na biashara huku nikisoma katika Chuo Kikuu cha Mzumbe”
anasema na kuongeza.
“Hivi sasa nimemaliza masomo nimeajiriwa kama
mwalimu wa biashara, lakini pia naendelea na ujasiriamali. Kwa sasa
nimejikita katika kilimo cha miti” anafafanua. Junior Achievment ni taasisi iliyoanzishwa nchini Marekani na imeenea
katika nchi 121 duniani, zikiwamo 15 zilizopo barani Afrika. Hadi sasa
imetoa mafunzo kwa vijana zaidi ya vijana 25,000.
Subscribe to:
Posts (Atom)