Friday, 31 August 2012

R.I.P HAWA NGULUME


MWANAMAMA machachali ambaye amewahi kuwa mkuu wa wilaya za Kinondoni, Bagamoyo na Mbarali kwa vipindi tofauti, Hawa Ngulume, amefariki dunia katika Hospitali ya Lugalo jijini Dar es Salaam jana asubuhi.
Kwa kujibu wa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Jordan Rugimbana, Ngulume alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya kansa kwa kipindi kirefu.

Ngulume atakumbukwa kwa ushupavu wake katika kusimamia mambo mbalimbali, kwani hata katika uchaguzi mkuu uliopita 2010 alijitosa kupambana na Mbunge wa Singida Mjini, Mohamed Dewji, akiomba kuteuliwa na CCM kupeperusha bendera hiyo.

Mwanasiasa huyo pia atakumbukwa sana na wafugaji katika Bonde tengefu la Ihefu kwani ndiye alisimamia kuwahamisha kwa nguvu wakati huo akiwa mkuu wa Wilaya ya Mbarali.
Naye Katibu Tarafa mstaafu wa Wilaya ya Kinondoni, Suleiman Mwenda, alisema kuwa Ngulume alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya kansa ya moyo.

Mwenda alisema kuwa mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Lugalo na mazishi yanatarajiwa kufanyika leo nyumbani kwake Goba jijini Dar es Salaam baada ya kumalizika kwa swala ya Ijumaa.
Alisema kwa muda huo, wanatarajia kuwa ndugu zake kadhaa kutoka Singida watakuwa wamekwisha kufika kuhudhuria shughuli hiyo.

Mwenda alifafanua kuwa Ngulume aliwahi kutibiwa katika hospitali mbalimbali, ikiwamo ya Ocean Road ya jijini Dar es Salaam na nchini India.
Kufuatia kifo hicho, Rais Jakaya Kikwete, ametuma salamu za rambirambi kwa familia yake akisema kuwa enzi za uhai wake alikuwa kiongozi shupavu aliyesimamia maamuzi yake katika majukumu muhimu ya kitaifa kwa lengo la kuwaletea wananchi maendeleo.

“Nilimfahamu marehemu enzi za uhai wake, kama kiongozi mwanamke shupavu aliyesimamia kikamilifu maamuzi yake, hivyo kuthibitisha ukweli kwamba wanawake wakipewa fursa wanaweza.
“Natuma salamu za rambirambi kutoka dhati ya moyo wangu kwa familia ya marehemu, Mama Ngulume kwa kuondokewa na mhimili muhimu na kiongozi wa familia. Natambua machungu mliyonayo hivi sasa kwa kumpoteza mama wa familia, lakini nawahakikishia kuwa niko pamoja nanyi katika kuomboleza msiba huu mkubwa,” alisema Rais Kikwete.

No comments:

GEITA DOCUMENTARY