Friday, 31 August 2012

Wanafunzi 51 UDSM wafutiwa kesi


MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu ya jijini Dar es Salaam, imewaachia huru wanafunzi 51 wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya kufanya mkusanyiko na maandamano kinyume cha sheria.
Akitoa hukumu hiyo jana, Hakimu Waliarwande Lema, alisema ameamua kuifuta kesi hiyo kutokana na kupitia mwenendo mzima na kujiridhisha kutokana na upande wa mashtaka kushindwa kupeleka hata shahidi mmoja hadi leo.

Alisema awali mashahidi walitakiwa kufika mahakamani hapo Septemba 8 mwaka huu, lakini upande wa mashtaka unaoongozwa na wakili wa serikali Ladslaus Komanya, ulidai kuwa askari waliotakiwa kutoa ushaidi huo walikuwa na kazi ya kusimamia mgomo wa madaktari.

Baada ya kutoa sababu hizo, hakimu alitoa tarehe ya ahirisho la mwisho ambalo ni jana na mashahidi walishindwa kufika tena na wakili wa serikali kuieleza mahakama kuwa wako katika kusimamia sensa.
Kutokana na sababu hiyo, Lema alisema upande wa mashtaka umeidharau mahakama kutokana na kuwepo na taratibu za kuomba ruhusa ingawa sensa ina umuhimu wake na kesi hiyo ina umuhimu wake pia.

Alisema kwa mujibu wa kifungu cha 225 (4) kifungu cha makosa ya jinai kulikuwa na utaratibu wake ambao wakili wa upande wa serikali alitakiwa kufanya kuliko hivyo alivyofanya.
Kutokana na hali hiyo Hakimu Lema alisema hana sababu ya kuendelea tena na kesi, hivyo ni bora kuwaachia huru kwa maana shauri zima halitakuwa na sababu ya kuendelea nalo.
“Kwa mujibu wa kifungu cha 225(5) sura ya 20 nawaachia huru washtakiwa wote kwa kuwa kesi hii haina haja tena ya kuendelea nayo,” alisema Lema.

Awali walipokuwa wanasomewa maelezo ya awali watuhumiwa hao walidaiwa kuwa pamoja na kupewa ishara ya kusitisha maandamano na askari polisi walikiuka na kuwashambulia kwa mawe.
Komanya alidai kuwa Novemba 11, 2011 wanafunzi hao walifanya mkusanyiko katika Uwanja wa Revolution lililopo katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na baadaye waliandamana kuelekea eneo la Ubungo Maji huku wakiwa wamebeba mabango yenye ujumbe unaoilaumu Serikali na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu kuwa haiwatendei haki.

Novemba 14 mwaka jana, wanafunzi hao walifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza wakidaiwa kufanya mkusanyiko usio wa halali na kusababisha uvunjifu wa amani katika eneo la UDSM.
Nje ya mahakama, nderemo na vifijo vilitawala ambapo wanafunzi hao walikuwa na furaha huku wakishangilia na kuelekea katika Barabara kuu ya Bibi Titi Mohamed kutokana na kuachiwa huko.


Na freemedia 

No comments:

GEITA DOCUMENTARY

Contributors