Tuesday, 8 May 2012

TUTUMIE NISHATI MBADALA YA UMEME WA JUA

KITUO cha Nishati na Maendeleo cha jijini Dar es Salaam, kimehimiza wananchi kutumia nishati mbadala ya umeme unaotokana na mionzi ya jua, ili kukabiliana na tatizo la umeme nchini.

Rai hiyo ilitolewa juzi na Mratibu wa kituo hicho, Hassan Bussiga alipokuwa akifunga mafunzo ya siku kumi kwa mafundi umeme wa majumbani waliokuwa wakijifunza namna ya kutengeneza umeme wa jua.
Alisema kwa sasa taifa linakabiliwa na changamoto kubwa inayotokana na kiwango kidogo cha uzalishaji wa umeme, jambo linalosababisha Watanzania wengi kuishi bila nishati hiyo.

“Hii inatokana na umeme kuwa wa gharama kubwa, umeme wetu unategema maji na mafuta na ni gharama sana, ndio sababu tunatoa mafunzo ili mafundi waweze kusaidia jamii kutumia umeme wa jua ambao ni wa gharama nafuu,”alisema Bussiga.

Bussiga alitaja faida ya matumizi ya umeme wa jua kuwa ni urahisi katika kuupata na pia gharama zake ni nafuu ikilinganishwa na umeme wa Gridi ya Taifa ambao pia si wa uhakika.

Kuhusu mafunzo kwa mafundi alisema yalilenga kuwajengea uwezo namna ya kutengeneza umeme huo pindi wanapoukuta kwenye nyumba za watu.

“Tumetoa mafunzo kwa mafundi umeme wa majumbani na wauzaji wa vifaa vya kutumia umeme wa jua, lengo ni kuongeza idadi ya wataalamu wa nishati ya umeme katika sekta hiyo inayokua kwa kasi hapa nchini,”alisema Bussiga.

Akizungumza kwa niaba ya mafundi wenzake, mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Kennedy Lameck alisema yeye pamoja na wenzake wamepata maarifa zaidi kuhusu umeme wa jua.


Kwa hisani: Mwananchi Comm

No comments:

Inspirational Prayer of the Day

choose your favorite language

GEITA DOCUMENTARY

HABARI NYINGINE ZAIDI