Monday, 7 May 2012

Tanesco yakanusha uhaba wa kadi za Luku


SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) limesema kukosekana kwa kadi za umeme wa Luku kwenye baadhi ya vituo Jijini Dar es salaam kumesababishwa na wenye vituo hivyo kutofuatilia kadi hizo  baada ya kuisha katika vituo vyao vya mauzo.
Hali hiyo ya kukosekana kwa huduma ya umeme wa kadi za Luku imejitokeza kwa baadhi ya vituo Jijini hapa na kusababisha shida kwa watumiaji kwenda maeneo ya mbali na makazi yao kufuatilia huduma hiyo.
Akizungumza na Mwananchi jana, Meneja Mawasiliano wa Tanesco, Badra Masoud katika Makao Mkuu ya Shirika hilo alisema  kukosekana kwa huduma ya umeme wa kadi za luku unasababishwa na wauzaji katika maeneo mbalimbali.

“ Kutopatikana kwa huduma ya kadi za luku ni uzembe ambao unasababishwa na wahusika wa vituo vya mauzo, kadi hapa Makao Makuu zipo nyingi tena za kutosha lakini nashangaa tuhuma kama hizo kwenye vyombo vya habari, mimi nasema kadi zipo ila hao wenye vituo ndio sio wafatiliaji,” alisema.

Aliongezea kwamba kwa vituo vyote vilivyopewa dhamana ya kutoa huduma hiyo halafu wanasingizia Shirika wakati kadi zipo na wao hawafatilii, watawaangalia kwa mara mbili au tatu kisha baada ya hapo watawapokonya mamlaka  ya kutoa huduma hiyo na kuwakabidhisha watu au makampuni mengine yanayohitaji ili waweze kuendesha huduma hiyo kwa umakini.

Masoud alisema Shirika lina mpango wa kuondoa huduma ya Luku za kadi na kuleta Luku za digitali,  pia wataondoa mita zote za zamani na kuweka mita za kisasa, mabadiliko haya  yanafanyika taratibu taratibu kila nyumba hapa nchini ila huduma hiyo tayari imeshaanza katika jiji hili la Dar es salaam na kuendelea kwa baadhi ya mikoa mingine.

Meneja huyo aliwataka Wananchi wasishangae pindi mabadiliko yatakapoanza maana sasa tupo katika wakati wa sayansi na teknolojia kwa hiyo mambo yanabadilika kutokana na wakati tuliopo kinachotakiwa ni kutupa ushirikiano wenu ili tuweze kufanikiwa kwenye mabadiliko hayo. 
 

No comments:

GEITA DOCUMENTARY

Contributors