Monday, 4 June 2012

TANESCO KUFUNGA TRANSFOMA MBILI MPYA

SHIRIKA la Umeme  Tanzania (Tanesco) jana, limeanza kufunga transfoma mbili mpya zenye uwezo wa kuzalisha umeme  wa megawati 12 kila mmoja katika kituo cha kuzalisha umeme cha City Centre, kilichopo Jijini Dar es Salaam.

Transifoma hizo ambazo zilikabidhiwa kwa Tanesco na Wizara ya Nishati na Madini kuanza kufungwa eneo hilo, zinachukua nafasi ya nyingine ambazo ziliungua kwa vipindi tofauti kati ya Januari na Machi mwaka huu.

Kamishna Msaidizi wa Madini wizarani hapo, Innocent Luago aliieleza  Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini kuwa , zoezi hilo ni mwanzo wa  sehemu ya kuziba pengo la transifoma zilizoungua ambapo  nyingine sita zinazotarajiwa kuwasili nchini hivi karibuni.

 Luago alisema, tranfoma hizo mbili ni miongoni mwa  chache zinazotarajiwa  kutoka nchini Uturuki na kufanya  jumla  yake kuwa nne, zenye  thamani ya Sh1.8 bilioni  kwa mchakato mzima hadi kufungwa jenereta zote ambAzo zitagharimu Sh2 bilioni.

“Kuna transifoma nyingine nne kutoka  India tunazitaraji wa pia” alisema na kuongeza kuwa  ufungaji wa transifoma hizo utasaidia kuongeza kiwango cha umeme katika maeneo kadhaa ya jiji.

Aliyataja maeneo ambayo yatanufaika baada ya kukamilika kwa zoezi hilo kuwa ni pamoja na Mtaa wa Mkwepu, hospitali za jirani na katikati ya jiji, mahoteli, benki na ofisi zinginezo” alisema.
Alisema Tanesco hivi sasa wapo katika maboresho kwa jiji la Dar es Salaam na maboresho hayo yataenda pia katika mikoa yote ya Tanzania na vituo zaidi katika jiji la Dar es Salaam.

“Dar es Salaam tuna vituo 27 vya kuzalishia umeme na tutaanza na vituo saba” alisema na kuvitaja vituo hivyo kuwa ni Kurasini, Kariakoo, Mnazi Mmoja, Kipawa na Mbagala.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, Suleiman Zedi aliipongeza wizara kwa hatua hiyo ya kukabiliana na changamoto zinazolikabili shirika hilo katika uzalishaji wa umeme.
“Tanesco ndiyo shirika nyeti katika uzalishaji pamoja na ukuaji wa uchumi , hivyo linahitaji kuwezeshwa kadiri itakavyowezekana” alisema mwenyekiti huyo.

No comments:

GEITA DOCUMENTARY

Contributors