MENEJA wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Mkoa wa Mbeya, Mhandisi John Bandiye amesema , sababu ya kukosa huduma ya umeme kwa baadhi ya maeneo Jijini Mbeya, imetokana na watu kuiba zaidi ya lita 1,000 za mafuta ya transfoma 12 katika maeneo tofauti mkoani hapo.
Bandiye alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, ambapo alisema, kutokana na wizi wa lita hizo za mafuta baadhi ya wakazi wa Iyunga,Forest Mpya na Mji mdogo wa Mbalizi kwa takribani mwezi mmoja wamekosa huduma hiyo muhimu.
Bandiye alisema, kufuatia hali hiyo wananchi hao waliamua kufika katika ofisi yake na kutoa malalamiko hayo ya kukosa umeme ambapo aliwaeleza tatizo lililopo ambalo ni la wizi wa mafuta katika baadhi ya transfoma katika maeneo tofauti tofauti jijini hapo.
Alisema, baada ya wananchi kuelezwa tatizo lililopo waliweza kushirikiana kwa pamoja kuwabaini wanaohusika wanaoiba mafuta hayo ikiwa ni kwa mwananchi mmoja kutoa taarifa za kuwapo mtu anayejihusisha na uuzaji wa mafuta hayo katika maeneo ya Wilaya ya Mbarali na Mbozi.
Bandiye alisema baada ya kupatia taarifa hizo waliweza kwenda na Polisi katika eneo la Chimala, wilayani Mbarali na kufanikiwa kumkamata mtu mmoja anayejihusisha na biashara hiyo ya mafuta ya transfoma pamoja na wengine watatu wilayani Mbozi, huku mmoja akiwa na mafuta hayo na nyaya za shaba mali ya shirika hilo na wengine wawili wakiwa na vyuma vinavyotumika kwenye nguzo zinazosafirisha umeme mkubwa.
"kufuatia hali hiyo tulifanikwa kuwakamata watu wanne katika wilaya ya Mbarali na Mbozi wakiwa na mafuta baadhi ya mfuta hayo, nyaya za shaba mali ya shirika hilo pia wengine walikutwa wakiwa na vyuma vinavyotumika kwenye nguzo zinazosafirisha kiasi kikubwa cha umeme", alisema Bandiye.
Aidha,Mhandisi Bandiye alisema Katika kipindi cha miezi miwili zaidi ya lita 1,000 za mafuta hayo ziliibiwa katika transfoma kumi na mbili maeneo tofauti mkoani hapa na walizofanikiwa kuzikamata kwa watuhumiwa hao ni lita 150 pekee.
"Katika kipindi cha miezi miwili zaidi ya lita 1000 za mafuta hayo ziliibiwa katika transfoma 12 maeneo tofauti tofauti mkoani hapa , lakini hadi sasa tumefanikiwa kukamata lita 150 pekee ambazo tulizikuta kwa watuhumiwa tuliowakamata katika operesheni yetu, tukishirikiana na wananchi na polisi kwa ujumla." alisema Bandiye.
Aliongeza kwamba hadi sasa hawaelewi mafuta hayo yanatumika kwa shughuli zipi, kwani mtoa taarifa aliyetumwa kujifanya mnunuzi wa mafuta hayo, alielezwa na mtuhumiwa wa Mbarali kuwa kwa lita 500 anazohitaji anatakiwa kulipia Sh1 milioni.
Alisema kufuatia hali hiyo ya wizi wa mafuta hayo, Tanesco mkoani hapa imeingia hasara kubwa kutokana na wizi huo, sambamba na miundombinu mingine kuhujumiwa kwani wateja wao wengi wakiwamo wenye viwanda vikubwa walilazimika kukosa huduma hiyo kwa kipindi kirefu.
Mbali na hilo Mhandisi Bandiye alisema walipokea malalamiko kutoka kwa baadhi ya zahanati katika mji mdogo wa Mbalizi, kuwa dawa zilizokuwa zimehifadhiwa katika friji zimeharibika kufuatia kukosekana kwa umeme.
Aliendele kuwaomba wananchi kutoa taarifa za mara kwa mara katika eneo husika pindi wanapobaini ubadhirifu wa aina yoyote ndani ya shirika hilo sambamba na kuwafichuwa wale wote wanaojihusisha na vitendo vya wizi wa mali za Tanesco.
No comments:
Post a Comment