Wednesday, 6 June 2012

Ajali yaua 13 Mbeya, 16 wajeruhiwa


WATU 13 akiwamo mjamzito wamefariki dunia, huku wengine 16 wakijeruhiwa kufuatia ajali iliyotokea Mbeya mjini baada ya basi dogo aina ya Coaster na lori aina ya Scania kugongana uso kwa uso.
Ajali hiyo ilitokea jana saa 6:30 mchana eneo la Mlima Mzalendo, Igawilo baada ya basi hilo lililokuwa limejaza abiria kutoka Mbeya kwenda Kyela liligongana na lori lililokuwa na tela likitokea nchini Malawi.
Mashuhuda wa tukio hilo walisema chanzo cha ajali hiyo ni breki za lori lililokuwa likiteremka kushindwa kufanya kazi na kuvamia basi hilo kwenye kona kali na kusababisha vifo hivyo.
Kwa mujibu wa maofisa wa polisi waliokuwa kwenye tukio hilo, watu waliokufa ni 13 na wengine 16 walijeruhiwa.
Walisema waliokufa papo hapo ni tisa na wanne walifia hospitalini wakiendelea kupata matibabu.
Miongoni mwa waliokufa yumo dereva wa basi aliyetambulika kwa jina la Mwasa Diamond (32), mkazi wa Ilomba, Mbeya na mwanamke mmoja aliyetajwa kuwa alikuwa ni mjamzito ambaye hakufahamika jina lake.
Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufani Mbeya, Eliuter Samky, alithibitisha kupokea miili ya marehemu na kwamba, hali za majeruhi zilikuwa mbaya.
Alisema baadhi ya miili ya marehemu haijatambuliwa na amewataka wananchi kujitokeza.Kamanda wa Polisi mkoani Mbeya, Athuman Diwani, hakupatikana kuzungumzia tukio hilo.

Kwa hisani ya Mwananchi comm 

No comments:

Inspirational Prayer of the Day

choose your favorite language

GEITA DOCUMENTARY

HABARI NYINGINE ZAIDI