Thursday, 12 April 2012

Wizi wa kazi za wasanii waibua mjadala Bungeni


SUALA la wizi wa kazi za wasanii nchini, limeibua mjadala mkali bungeni huku Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto akipendekeza mtu atakayekamatwa akiuza CD na DvD feki za kazi za wasanii atozwe faini isiyopungua sh50 milioni.

Mbunge huyo ambaye pia ni Naibu Msemaji wa Kambi rasmi ya upinzani Bungeni, alipendekeza kuwa mtu yeyote atakayekutwa na kazi feki za wasanii naye aadhibiwe vikali ili kujenga Utamaduni wa Watanzania kuacha kununua kazi za wizi wasaniii.

Wabunge hao walichachamaa Bungeni mjini Dodoma jana wakati wakichangia hotuba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Cyril Chami kuhusu muswada wa sheria ya marekebisho ya sheria mbalimbali za biashara wa mwaka 2011.


Zitto alisema biashara ya sanaa nchini imekukuwa haiangaliwi kikamilifu na kwamba mazishi ya msanii nguli wa filamu nchini, Steven Kanumba yaliyofanyika juzi yamedhihirisha kuwa Watanzania ni wapenzi wa sanaa ikiwamo filamu na muziki.

Mbunge huyo alipendekeza wasanii wote wasajiliwe na kila mmoja awe na nambari ya mlipa kodi (TIN) ili zoezi la Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA) la kutoa stika za ushuru liwe na mafanikio kwa kuwa kila msanii atakuwa anafahamika TRA.

Naye Mbunge wa Viti Maalumu, Martha Mlata (CCM) alipendekeza kuanzishwa kwa Wizara ya Utamaduni na Sanaa na kuhoji serikali inashikwa na kigugumizi gani kuipatia sekta ya sanaa wizara yake kamili kutokana na umuhimu wake.

Pia alibainisha kuwa suala la mikataba ya usambazaji wa kazi za sanaa za wasanii lina utata na kutoa mfano kwa CD moja ya muziki, msanii hulipwa Sh150 huku mapato makubwa yakiishia kwa wasambazaji wanaonufaika na kazi hizo.

“Wasanii wananufaika tu umaarufu lakini wanaendelea kuwa masikini kwa kuibiwa kazi zao na jasho lao….hivi kuna tatizo gani kuweka Wizara ya Utamaduni na Sanaa itakayosimamia kwa dhati haki za wasanii?”alihoji Mbunge huyo katika mchango wake huo.
Pia alipendekeza mabadiliko hayo ya sheria yatamke waziwazi wasanii wananufaika vipi na mapato wanayopata wamiliki wa vituo vya Televisheni vinavyotumia kazi za wasanii ikiwamo filamu na muziki kwa kuwa vingi havilipi mrahaba kwa wasanii.
 
Mbunge wa Mbeya mjini, Joseph Mbilinyi (Chadema) 'Sugu' alisema tatizo la viongozi wa serikali ni kushughulikia suala la haki miliki za kazi za wasanii kisiasa na kuwaacha wasanii wakiendelea kuibiwa kazi zao na kunufaisha watu wachache.

“Pamoja na Steven Kanumba (marehemu) kutengeneza filamu 50 lakini amekufa masikini… Rais wetu amekwenda vichochoroni alipokuwa akiiishi…Waziri Mkuu amekwenda vichochoroni kama kuna mtu angetaka kuwateka angewateka” alisema.

Mbunge huyo alipendekeza wanaokamatwa wakiiba kazi za wasanii washitakiwe kwa uhujumu uchumi huku akisisitiza Chama cha Haki Miliki na Shiriki (Cosota) imeshindwa kazi na kutaka pia studio ya wasanii iliyotolewa na Rais Jakaya Kikwete irudishwe Basata.

Akiwasilisha muswada huo wa sheria, Dk. Chami alisema mswada huo unapendekeza kufanya marekebisho katika sheria mbalimbali za biashara kwa lengo la kuboresha mazingira ya kufanyia biashara ikiwamo udhibiti wa bidhaa bandia.

Chini ya mabadiliko hayo ya sheria, serikali inapendekeza kuwapo kwa sheria mpya inayowapa nafasi watu mbalimbali kuweza kuanzisha kampuni zinazomilikiwa na mtu mmoja badala ya sheria ya sasa inayolazimisha kutafuta washirika.

Akiwasilisha maoni ya kamati ya kudumu ya Bunge ya viwanda na biashara, mwenyekiti wa kamati hiyo, Mahmoud Mgimwa alisema wafanyabiashara wengi wadogo wanaingia hatiani kwa kununua biadhaa bandia kwa wafanyabiashara wakubwa wasio waaminifu.

Kamati hiyo imeshauri kuwa udhibiti wa bidhaa bandia ufanyike kwa kufuatilia mwagizaji wa mwanzo na kumchukulia hatua ikiwamo kumwadhibu na kwamba adhabu kwa mfanyabiashara mdogo anayekutwa na bidhaa bandia iondolewe.

No comments:

GEITA DOCUMENTARY