Wednesday, 11 April 2012

Jenerali Mwita Kyaro afariki dunia

MKUU wa Majeshi Mstaafu Jenerali Ernest Mwita Kyaro, amefariki dunia katika Hospitali ya Bugando jijini Mwanza.

Msemaji wa Jeshi la Wananchi Tanzania ( JWTZ), Kanali Kapambala Mgawe alithibitisha kutokea kwa kifo hicho akieleza kuwa Jenerali Mwita Kyaro alifariki dunia saa 4 asubuhi jana katika hospitali ya Bugando alipokuwa akitibiwa.

Akieleza wasifu wa marehemu huyo, Mgawe alisema Jenerali Kyaro aliongoza jeshi hilo akiwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama (CDF) kati ya mwaka 1988 hadi 1994 alipostaafu.

“Jenerali Kyaro alistaafu akiwa amelitumikia jeshi kwa miaka 50, miezi 11 na siku 13,” alisema Mgawe na kufafanua kuwa jenerali huyo alizaliwa mwaka 1925, Kijiji cha Nyamwaga, Tarafa Igwe Tarime, mkoani Mara.


Hata hivyo, alisema hadi sasa ratiba ya mazishi ya halijajulikana kwa kuwa, familia yake ndiyo itakayosema marehemu huyo azikwe wapi.

“Lakini kwa upande wetu sisi (jeshi) tumeanza kujiandaa, wenzetu huko Mwanza na Tabora wanaendelea na maandalizi na tunasubiri tu familia ituambie ni wapi wanataka marehemu azikwe,” alieleza.

Kuhusu sababu ya kifo cha Jenerali Kyaro, msemaji huyo wa jeshi alisema kuwa bado hawajafahamu kwa kuwa hawajapata taarifa za madaktari.

Wasifu wa marehemu
Akieleza wasifu wa marehemu kwa kifupi tangu alipoingia kazini, Mgawe alisema kuwa alijiunga na jeshi Aprili 19 mwaka 1943.

“Wakati huo lilikuwa ni Jeshi la Mkoloni Kings African Rifles (KAR), baadaye baada ya uhuru akajiunga na Tanganyika Rifles, aliendelea kuwa jeshini hata lilipokuja kuundwa JWTZ mwaka 1964,” alisema Kanali Mgawe.

Alisema kuwa Jenerali Kyaro aliendelea kulitumikia jeshi hadi alipostaafu Machi 31 mwaka 1994 na kwamba katika utumishi wake aliwahi kutunukiwa nishani mbalimbali ikiwa ni pamoja na ya miaka 20 ya JWT, Utumishi Uliotukuka Tanzania na Utumishi wa Muda Mrefu Tanzania.
Alizitaja nyingine kuwa ni Medali ya Vita, Medali ya Kagera, Medali ya Uhuru na Medali ya Muungano.
Jenerali Kyaro ameacha sifa ya uaminifu ambayo haijavunjwa jeshini baada ya CDF pekee aliyewahi kurejesha masurufu aliyolipwa kwenda kutibiwa nje ya nchi, kutokana na kudai kuwa akila na kutibiwa bure bila kutumia fedha hizo.

Ikulu yamlilia

Wakati huohuo, Rais Jakaya Kikwete ametuma salamu za ramburambi kwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Davis Mwamunyange kufuatia kifo hicho cha Kyaro.

“Katika salamu zake kwa Jenerali Mwamunyange, Rais Kikwete amemwomba Mkuu huyo wa Majeshi ya Ulinzi kumfikishia salamu za rambirambi za dhati ya moyo wake kwa familia ya Jenerali Mstaafu Kyaro na kwa makamanda na wapiganaji wote wa Majeshi ya Ulinzi kwa kumpoteza mdau, mwenzi wao na kiongozi wao,” inasema taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu.

Taarifa hiyo inamnukuu Rais Kikwete akisema: “Nimepokea kwa huzuni nyingi na majonzi makubwa taarifa ya kifo cha Jenerali Mstaafu Ernest Mwita Kyaro ambaye ameaga dunia asubuhi ya leo katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando, Mwanza, ambako alikuwa amelazwa.”

“Nilifahamu vizuri na nilifanya kazi na Jenerali Kyaro wakati wa enzi ya uhai wake. Alikuwa Mtanzania mzalendo wa kuigwa, mwadilifu na mwaminifu kwa taifa lake, mchapakazi hodari na mpiganaji na kamanda wa mfano kabisa kwa waliokuwa chini yake."

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Rais Kikwete alisema marehemu alithibitisha sifa zake hizo katika kipindi chote cha miaka 50 na miezi 11 alipokuwa katika ulinzi wa nchi hii.

Alisema tangu alipokuwa mpiganaji hadi alipopanda na kuwa kamanda, hatimaye Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi kwa kipindi cha miaka minne kati ya 1988 hadi Februari 25, 1992, alipostaafu utumishi wa Jeshi, marehemu alithibitisha kuwa ni mtu wa kipekee.

"Tutaendelea kumkumbuka na kumuenzi kwa utumishi wake uliotukuka kwa taifa letu.”

No comments:

Inspirational Prayer of the Day

choose your favorite language

GEITA DOCUMENTARY

HABARI NYINGINE ZAIDI