Tuesday 4 September 2012

KATIBA MPYA KUPATIKANA APRIL, 2014


TUME ya Mabadiliko ya Katiba imesema imejipanga kukamilisha majukumu yake ndani ya muda uliowekwa na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, hivyo nchi kuwa na Katiba Mpya ifikapo Aprili, mwaka 2014.

Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji mstaafu Joseph Warioba, aliwaeleza mawaziri wa Katiba na Sheria kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwa pamoja na changamoto zilizopo, dhamira hiyo ya tume ipo palepale.

Mawaziri hao, Mathias Chikawe wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Abubakar Khamis Bakari wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar walitembelea ofisi za Tume ya Mabadiliko ya Katiba jana, ili kujionea utekelezaji wa shughuli mbalimbali za tume hiyo.

“Tunafahamu hii ni changamoto, lakini tumeikubali na tutajitahidi kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha kama taifa tunakuwa na Katiba Mpya ifikapo Aprili 26, mwaka 2014,” alisema Jaji Warioba.
“Ukiangalia hali ya kisiasa, tunadhani itakuwa vizuri tukiwa na Katiba Mpya kabla ya uchaguzi wa mwaka 2015,” alisema Jaji Warioba.

Pamoja na nia hiyo, Jaji Warioba pia aliwaeleza mawaziri hao kuwa kwa sasa tume yake imejikita katika kukusanya maoni binafsi ya wananchi na kuwa baada ya hatua hiyo tume itaanza kukusanya maoni ya makundi mbalimbali kama vyama vya siasa, taasisi za kidini, jumuiya za kitaaluma na asasi za kiraia.
Akizungumza katika mkutano huo, Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe, alieleza kufurahishwa na utekelezaji wa majukumu ya tume hiyo na kuahidi serikali itaendelea kutoa ushirikiano, ili kuhakikisha malengo yake yanafikiwa.

No comments:

GEITA DOCUMENTARY

Contributors