Monday 6 August 2012

MAHAKAMA ZATAKIWA KUHARAKISHA KESI ZA UKATILI DHIDI YA WANAWAKE


NAIBU Waziri wa Sheria na Katiba, Angellah Kairuki, amezitaka mahakama kuharakisha kesi zinazohusu ukatili wa kingono dhidi ya wanawake na watoto, pia amewaonya watu kutokuingilia uhuru wa mahakama.
Kairuki alisema hayo mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam katika uzinduzi wa Mradi wa Haki za Wanawake (HAWA), na kushauri kesi hizo zimalizike ndani ya miezi sita.


Aliwataka wadau wote wa haki za binadamu kuwatetea wafanyakazi wa sekta zote hususan wafanyakazi wa ndani, walinzi, madereva, wafanyakazi wa mashambani, vibarua wa aina mbalimbali na wahudumu wa baa kwa kuwa hawatambuliwi wala hawapatiwi haki zao za msingi.

Naye Mkurugenzi wa HAWA, Joyce Kiria, alisema kuwa mradi huo umegawanyika katika sehemu tatu, ya kwanza ikiwa ni mradi wa Dada Jijue utakaowezesha wafanyakazi wa ndani na mama lishe kupambana na changamoto wanazokutana nazo ili wafikie ndoto zao.

Joyce alitaja mradi wa pili kuwa ni Okoa Mtoto utakaowasaidia watoto waliofanyiwa vitendo vya ukatili ikiwa ni pamoja na kuwalinda kutokana na vitendo hivyo huku mradi wa tatu ukiwa ni Haki ya Mama Kupata Usawa, Haki, Elimu ya Kujilinda na Ukatili wa Ngono.



Habari kwa hisani ya Tanzania Daima

No comments:

GEITA DOCUMENTARY

Contributors