TANZANIA inaweza kupunguza vifo vinavyotokana na ugonjwa wa malaria kwa kiwango kikubwa, iwapo Serikali itaweka mfumo maalumu wa uelimishaji jamii kwenye ngazi ya vijiji.
Kulingana na takwimu zilizotolewa na Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria (NMCP) nchini, watu 80,000 wanakadiriwa kufa kila mwaka kutokana na ugonjwa huo na asilimia 36, ni watoto wenye umri chini ya miaka mitano.
Uchunguzi uliofanywa na Mwandishi wa habari hizi kwenye maeneo ambayo elimu ya kina imetolewa kwa jamii, limebaini wagonjwa huwahi hospitali wanapoona dalili za awali na kuwaepusha kuingia kwenye hatua ya kupata malaria kali ambayo ndiyo imekuwa ikisababisha vifo.
Mwandishi wa habari hizi alitembelea Wilaya ya Kilosa na Kata ya Ngerengere, wilayani Morogoro Vijijini ambako mradi wa elimu ya badili jamii tabia uliendeshwa.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wakazi wa maeneo hayo, wataalamu wa afya, viongozi wa serikali na dini, walikiri kuwa elimu imesaidia watu wenye malaria kali kupungua kwenye hospitali na zahanati, huku wenye dalili za awali wakifurika na kupatiwa tiba.
Wahudumu wa Afya
“Kinachoonekana sasa ni kwamba malaria haitishi tena kama ilivyokuwa hapo miaka ya nyuma… Mapango unaonekana kupunguza zile ugumu kwenye tiba,” alisema Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Ngeregere, Isaak Soka na kuongeza:
“Hapa namaanisha kuwa wale wagonjwa wa malaria wanaokuja wakiwa wamezidiwa kutokana na degedege, ukosefu wa damu na kuchanganyikiwa wamepungua sana.”
Hata hivyo, Soka alisema kinachoonekana sasa ni wagonjwa wa malaria wanafurika kwa wingi kwenye zahanati hiyo, kuliko hapo awali na kuashiria kuwa kila wakiona dalili za awali, wanawahi hospitali.
Mhudumu wa Afya Kata ya Ngerengere, Omari Mrimka, alisema kuongezeka kwa wanaofika kutibiwa inatokana na wengi kuacha mila potofu za kutibu malaria kwa waganga wa jadi.
Mratibu wa Malaria na Mdhibiti wa Magonjwa ya Watoto kwa Uwiano Halmashauri ya Kilosa, Rose-Mary Nguruwe, alielezea mpango huo wa uelimishaji jamii kuwa umetoa mwamko siyo tu kuwezesha watu kuwahi tiba, bali hata wanawake kutumia vyandarua.
“Huko nyuma wajawazito waliokuwa wakipewa zile hati punguzo walikuwa hawaendi kuchukua vyandarua… Leo hii wanajitokeza kwa wingi na wanapofika kwa mara ya kwanza huwadai wahudumu wa afya wawapatie.”
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kilosa, Redegunda Ngowi, alisema wilaya hiyo kijiografia ipo kwenye ukanda wa malaria na mpango wa uelimishaji umeonyesha mafanikio.
Ngowi alisema halmshauri imetoa mapendekezo kwa serikali kuu kuweka mfumo ambao utaendeleza utaratibu huo mpya wa uelimishaji jamii kuhusu malaria.
Kwa hisani ya Mwananchi
No comments:
Post a Comment