Tuesday, 24 April 2012

Maelfu wamzika Mutharika


MAELFU ya wananchi wa Malawi jana walifurika katika Shamba la Ndata, Thyolo kusini mwa Blantyre ambako aliyekuwa Rais wa Malawi, Bingu wa Mutharika alizikwa.

Rais wa Malawi, Joyce Banda aliwaongoza maelfu ya wananchi hao wakiwamo marais watano wa Afrika, wawakilishi wa nchi, mashirika ya kimataifa na jumuiya za kikanda katika mazishi hayo yaliyofanyika kutwa nzima ya jana.

Akizungumza katika mazishi hayo, Rais Banda alisema Malawi imepoteza kiongozi aliyekuwa mwalimu kwa wananchi wake na kwamba kifo chake kiwe ni fursa kwa taifa hilo kusimama pamoja na kujijenga.

“Kama Rais Mutharika alifanya makosa, hebu basi tusahau makosa na tuyaone na kuendeleza yale yote ambayo aliifanyia nchi hii. Sina haja ya kuyataja kwani yapo na kila mmoja wetu anayafahamu,” alisema Banda ambaye alikuwa Makamu wa Mutharika kabla ya kuapishwa kuchukua nafasi yake.
 
Baada ya shughuli za kiserikali katika Viwanja vya Ndata kumalizika saa 7.30, shughuli za mazishi zilikabidhiwa kwa Kanisa Katoliki. Ibada hiyo iliongozwa na Askofu wa Jimbo la Blantyre, Mhashamu Tarsius Ziyaye akisaidiwa na maaskofu wengine saba, mapadre na makasisi wasiopungua 60 na ilidumu kwa zaidi ya saa tatu.   
 
Mapema saa 3:00 asubuhi, wakuu hao wa nchi na wageni wengine kutoka nchi mbalimbali walitoa heshima za mwisho kwa Mutharika katika makazi ya kiongozi huyo na baadaye kuelekea kwenye viwanja ambavyo vilitumika kwa ajili ya kutoa hotuba na ibada ya mazishi.   

Marais waliohudhuria mazishi hayo ni Jakaya Kikwete, Hifikepunye Pohamba wa Namibia, Mwai Kibaki wa Kenya, Robert Mugabe wa Zimbabwe na Armando Guebuza wa Msumbiji.

Pia walikuwapo Naibu Rais wa Afrika Kusini, Kalema Motlante, Makamu wa Rais wa Zambia, Waziri Mkuu wa Zimbabwe, Robert Tsvangirai, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Afrika, Jean Ping na wawakilishi wa Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na Soko la Pamoja la Nchi za Kusini mwa Afrika (Comesa).

Mazishi hayo nusra yaingie dosari kutokana na kuwapo kwa vijembe vya kisiasa ambavyo vilikuwa vikitolewa na watu waliopata fursa ya kuzungumza, hasa wanachama wa kilichokuwa chama tawala cha Mutharika cha Democratic Progressive Party (DPP).

Mamia ya wafuasi wa chama hicho mara kadhaa walikuwa wakilipuka kwa nyimbo hivyo kukatisha hotuba ambazo zilikuwa zikitolewa, huku kukiwa na kundi jingine la watu waliokuwa wakizomea au kupiga kelele kupingana na wafuasi wa DPP.

Maombolezo Ndata

Viwanja vya ibada na shughuli za mazishi vilikuwa vimepambwa kwa rangi za bluu. Jukwaa kuu ambalo lilikuwa maalumu kwa wageni mashuhuri wakiongozwa na Rais Banda, lilikuwa limetazamana na madhabahu ya Kanisa Katoliki ambayo ilikuwa na Maaskofu wa Kanisa hilo walioongoza ibada ya mazishi.

Jeneza lililobeba mwili wa Mutharika lilikuwa katikati ya jukwaa kuu na madhabahu, ambavyo vilikuwa vikiunganishwa na mazulia mekundu yaliyotumiwa na wakuu wa nchi na wageni wengine wakati wote wa shughuli za mazishi.

Pande zote mbili za jeneza hilo walikaa ndugu wa karibu wa Mutharika na wanafamilia wengine chini ya moja ya mahema yaliyokuwa yamewekwa uwanjani hapo kuwakinga wasipatwe na jua.

Wakuu wa nchi walianza kuwasili kwenye viwanja vya ibada saa 4.30 asubuhi wakitanguliwa na Rais Kikwete na wa mwisho kufika uwanjani hapo alikuwa ni Rais Mugabe. Wote walilakiwa na Makamu Rais wa Malawi, Khumbo Kachali.

Rais wa Malawi, Banda alifika uwanjani saa 4.55 akiambatana na mumewe, Jaji Mstaafu wa Malawi na Swaziland, Richard Banda na baada ya kuwasili, wimbo wa Taifa ulipigwa kisha kuchukua nafasi yake kwenye jukwaa kuu.
 
Mwili wa Mutharika uliwasili kwenye viwanja vya maombolezo saa 5.20 ukisindikizwa na maofisa wanane wa Jeshi la Malawi (MDF), waliokuwa wamevalia sare nyeusi za kijeshi na nyuma yao walikuwapo maofisa wengine wapatao 16 waliokuwa wamevalia sare za khaki.

Baada ya kuwekwa mahala pake, wimbo wa Taifa la Malawi ulipigwa hivyo kutoa fursa ya kuanza kutolewa kwa salaam mbalimbali za rambimrabi.

Ndata yatikisika

Makundi ya watu yalianza kuingia kwa wingi katika Viwanja vya Ndata kuanzia saa 12:00 alfajiri huku kukiwa na misururu mirefu ya magari katika Barabara Kuu ya Midima kuelekea katika eneo la maziko.

Miongoni mwa magari yaliyokuwa yekielekea katika eneo hilo ni malori ambayo yalisafirisha mamia ya wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya Kanda ya Kusini (Blantyre) ambayo yaliegeshwa umbali wa kilometa tatu hivyo watu kutembea kwa miguu.

Uliwekwa utaratibu wa malango makubwa mawili ya kuingilia na kila lango likiwa na milango midogo mitatu. Mbele ya milango hiyo kulikuwa na askari wa ukaguzi na kila aliyeingia alikaguliwa.

Baada ya ukaguzi kila aliyeingia, wengi wakiwa wamevalia mavazi maalumu ambayo ni vitenge vya maombolezo, alipewa chupa moja ya maji au juisi na mkate mdogo, kisha kuelekezwa sehemu ya kwenda kuketi.

Baadhi ya waombolezaji walipata viti chini ya mahema yaliyokuwa yamewekwa uwanjani hapo,lakini wengi kwa mamia waliketi chini wakipigwa jua kutwa nzima ya jana lakini hawakuondoka hadi saa 11:00 jioni mwili wa Mutharika ulipoingizwa kaburini.


Vijembe vya kisiasa

Vijembe vya kisiasa vilianza wakati mdogo wake Mutharika, Peter ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirkiano wa Kimataifa wa Malawi alipokaribishwa kuzungumza kwa niaba ya familia.
 
Wafuasi wa DPP walianza kuimba, wimbo wenye maneno “Mutharika tutaendelea kukutaja hata kama wengine hawataki kukukumbuka..” hivyo Peter kulazimka kusubiri kwa zaidi ya dakika tano.

Pamoja na kuwapo kwa mvutano wa wazi baina ya wafuasi hao na kiongozi wa shughuli hizo (MC) ambaye aliwataka kukatisha wimbo wao huku akiwaeleza bayana kwamba wanakosa nidhamu, Peter alipoanza mazungumzo yake aliwasifu kwa wimbo wao mzuri ambao alisema: “umenifurahisha”.

Peter ambaye alitangazwa kuwa kiongozi wa DPP baada ya kifo cha kaka yake, aliwaahidi wafuasi hao akisema: “Haijalishi ni ugumu gani nitakaoupata, lakini nawaahidi kwamba kamwe sitawaacha.”

Mwanafamilia mwingine ambaye ni Balozi wa Malawi nchini China pia mpwa wa hayati Mutharika, alisema wale wanaoshangilia kifo cha ndugu yao (Mutharika) kwa sababu za kisiasa wajue kwamba hii ni dunia. Alisema licha ya kwamba alikuwa akiendelea na kazi lakini alikuwa na ugonjwa mwingine wa kansa ya damu, mbali na ugonjwa wa moyo ambao unatajwa kwamba ulisababisha kifo chake.
 
Hata hivyo, vijembe hivyo vya kisiasa vilipozwa na hotuba ya Katibu Mkuu wa DPP ambaye kwa upande wake, alimwomba radhi hadharani Rais Banda akisema: “Inawezekana sisi ndani ya DPP tulisema mambo mabaya dhidi yako, tunakuomba utusamehe. Mutharika sas ani roho maana mwili tunakwenda kuuzika, tunaomba yale mabaya tuyazike na Mutharika na sisi wote tuanze kuijenga Malawi mpya kwa kushirikiana na Rais Banda.”

No comments:

Inspirational Prayer of the Day

choose your favorite language

GEITA DOCUMENTARY

HABARI NYINGINE ZAIDI