Friday, 20 April 2012

Makamu wa Rais aipa somo mifuko ya jamii

MAKAMU wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal ameitaka mifuko ya hifadhi ya jamii kutoa kinga dhidi ya majanga ili kuhakikisha kuwa wanachama wake wanaishi vyema hata majanga yanapotokea. 

Dk. Bilal aliyasema hayo jana wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Nne wa Wadau wa Mfuko wa Akiba wa Wafanyakazi wa Serikali (GEPF) uliofanyika jijini hapa. 


Alisema pamoja na michango mikubwa na mifuko hiyo katika uchumi na maendeleo ya Taifa, bado ni sehemu ndogo ya Watanzania wanapata kinga dhidi ya majanga kupitia mifuko hiyo. 

Alisema takwimu zinaonesha kuwa kati ya Watanzania milioni 22.4 wenye uwezo wa kuzalisha kipato, walio katika mifuko hiyo ya hifadhi si zaidi ya asilimia sita hivyo kuifanya Serikali kuanzisha Mamlaka ya Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi za Jamii (SSRA) ili kupanua wigo wa wanachama wanaojiunga na mifuko hiyo. 

Alisema lengo ni kuhakikisha asilimia kubwa ya Watanzania wanapata kinga dhidi ya majanga yanayoweza kutokea kutokana na kupungukiwa au kupoteza kipato kutokana na umri mkubwa, maradhi, kufariki au kuumia kazini. 

Makamu wa Rais alisema hata hivyo, mifuko ya hifadhi za jamii imekuwa ikichangia asilimia 21 sekta ya fedha na kuifanya sekta hiyo kukua kutoka Sh trilioni 1.637 mwaka 2001 hadi kufikia Sh trilioni 10.040 mwaka 2009. 

Katika mkutano huo, Makamu wa Rais ilizindua huduma ya Airtel money ambayo itawarahisishia wanachama wa Mpango wa hiari wa kujiwekea akiba uzeeni (VSRS) kutuma michango yao kwa urahisi. 

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Fedha, Gregory Teu ameitaka mifuko ya hifadhi za jamii kuweka wazi taratibu za uendeshaji wa mifuko ili kutoa nafasi ya kuchangia maendeleo na kwamba mifuko ambayo haijaanza kuitisha mikutano ya wanachama na wadau wafanye hivyo mapema.


Kwa hisani ya HabariLeo 

No comments:

GEITA DOCUMENTARY

Contributors