Monday, 9 December 2013

RAIS KIKWETE AONGOZA MAADHIMISHO YA MIAKA 52 YA UHURU WA TANGANYIKA UWANJA WA UHURU.

Bendera zikipepea nusu mlingoti ikiwa ni ishara ya kuomboleza kifo cha Mzee Nelson Mandela.
Rais Kikwete akiwasili uwanja wa uhuru katika maadhimisho ya miaka 52 ya uhuru wa Tanganyika

Vikosi vya usalama katika gwaride la heshima kuadhimisha miaka 52 ya uhuru wa Tanganyika.

Vijana wa vikosi vya usalama wakiwa kazini katka Gwaride la heshima la kuadhimisha miaka 52 ya uhuru wa Tanganyika
Vikosi vya usalama katika gwaride la heshima.

Watoto wa halaiki wakitoa burudani ya aina yake katika maadhimisho ya miaka 52 ya uhuru katika uwanja wa uhuru leo.
Dar es Salaam.
     Happy birthday Tanganyika’. Miaka 52 imetimia tangu Tanganyika (sasa Tanzania), kupata uhuru wake kutoka kwa wakoloni wa Kiingereza, Desemba 9, mwaka 1961.
Kama ilivyo ada, katika maadhimisho hayo yatakayofanyika kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam, Rais Jakaya Kikwete anatarajia kukagua gwaride la vikosi mbalimbali vya ulinzi na usalama ambavyo pia vitatoa heshima kwa kiongozi huyo kwa mwendo wa pole na haraka. Baadaye kikosi cha anga kitatoa heshima zake na kufuatiwa na burudani mbalimbali ikiwamo ngoma na michezo ya halaiki. Sherehe hizo pia zitahudhuriwa na wageni mbalimbali waalikwa wa ndani na nje ya nchi, wakiwamo mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini.
Katika sherehe hizo, Rais Kikwete hutoa msamaha kwa wafungwa na mwaka jana aliwasamehe wafungwa 3,814 waliokuwa na umri zaidi ya miaka 70, wenye ulemavu wa mwili na akili, magonjwa kama Ukimwi, kifua kikuu na saratani ambao wako kwenye hatua ya mwisho ya ugonjwa,
Wengine ni wafungwa wa kike walioingia na mimba gerezani na walioingia na watoto wanaonyonya na wanaotumikia kifungo kisichozidi miaka mitano ambao hadi siku ya msamaha, walikuwa wametumikia robo ya vifungo vyao.
Katika maadhimisho hayo mwaka jana, yaliyohudhuriwa na viongozi 14 wa kutoka Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), Rais Kikwete aliwataka Watanzania kujivunia na kuyaenzi mafanikio ya kisiasa, kiuchumi na kijamii yaliyopatika tangu nchi ilipopata uhuru.

Wasomi wazungumzia miaka 52

      Wakizungumzia maadhimisho hayo, baadhi ya wasomi waliohojiwa jana kwa nyakati tofauti walisema nchi haiwezi kupiga hatua kimaendeleo bila kufuta ujinga, umaskini na maradhi.
Wamesema sababu za Tanzania kupiga hatua ndogo ya maendeleo kisiasa, kiuchumi na kijamii katika miaka hiyo 52, kunachangiwa na mfumo mbovu wa elimu, huduma za afya zisizoridhisha na wananchi wake kukabiliwa na umaskini wa kipato.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana alisema mafanikio makubwa ya kujivunia ni kitendo cha Tanzania kulinda uhuru wake, kwamba tatizo linaloikabili nchi ni viongozi wake kuwa wazungumzaji zaidi kuliko kufanya kazi.
“Viongozi wetu wamekuwa wazungumzaji zaidi kuliko kufanya kazi, hakuna jitihada za makusudi za kuwakomboa Watanzania maskini,” alisema Dk Bana. Alisema mpaka sasa baadhi ya mambo yanakwenda kombo kutokana na viongozi wa Serikali kushindwa kufuta maadui watatu ambao ni maradhi, ujinga na umaskini.
“Mfano ni katika elimu yetu, kwa miaka takriban mitano inaporomoka tu lakini hakuna jitihada zozote za msingi za kumaliza tatizo hilo. Vyama vya siasa navyo havina mikakati imara ya maendeleo, vimebaki kutupiana maneno tu,” alisema na kuongeza:
“Wabunge na viongozi wetu wawaelimishe wananchi jinsi ya kusimamia rasilimali zao. Hali ni mbaya maana tangu uhuru tumebinafsisha viwanda vingi na hiyo ni moja ya sababu ya kutopiga hatua kimaendeleo maana bila viwanda nchi haiwezi kukua kiuchumi.” Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo hicho, Profesa Gaudence Mpangala alisema uchumi umekuwa katika makaratasi na kitakwimu tu.
“Wanasema tumekuwa kiuchumi lakini hatuna maendeleo ya kiuchumi, nchi yenye maendeleo na watu wake nao wanakuwa na maendeleo” alisema Profesa Mpangala.
Alisema tatizo jingine linaloikabili Tanzania ni kuwa na mfumo mbovu wa elimu na kufafanua kuwa kama yasipofanyika mabadiliko makubwa katika tasnia hiyo, hali ya uchumi ya Watanzania na nchi itazidi kudorora.
Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu Dodoma (Udom), Dk Honest Ngowi alisema: “Uchumi wa Tanzania umekuwa kwa asilimia saba lakini wananchi bado ni maskini mno.
“Tunatakiwa kuhakikisha kuwa ukuaji wa uchumi unapunguza umaskini kwa mtu mmojammoja, binafsi naweza kusema tumepata uhuru wa kisiasa, uhuru wa kiuchumi bado.”
Mhadhiri mwingine wa UDSM, Bashiru Ally alisema: “Tatizo ninaloliona katika miaka hii 52 ya uhuru ni wanyonge kuwaachia wanasiasa, wahisani, asasi za kiraia na wabunge kuzungumzia matatizo yao badala ya wao kuwa mstari wa mbele kudai haki zao za msingi.”
Alisema kuwa Watanzania wanatakiwa kuamka na kuanza kudai rasilimali zao zinazotoroshwa kila kukicha... “Watambue kuwa ukombozi wa nchi yao wanao wao wenyewe. Hilo ni jukumu lao na siyo la mtu mwingine.”..

CREDIT:- Mwananchi  na   Steven Mruma.

No comments:

GEITA DOCUMENTARY