Friday, 28 December 2012

UJIO WA TEKNOLOJIA YA DIJITALI UTAWAKOMBOA WASANII?


KUMEKUWA na hofu miongoni mwa wasanii na Watanzania wengine kuhusu ujio wa mpango wa dijitali kwamba ni nani atasalimika.
Wasanii ninyi mtakuwa wa kwanza kusalimika kwani hivi sasa mtaweza kuuza kazi zenu bila masharti kuwa lazima sura za fulani na fulani ziwepo.
Bila shaka mfumo huu wa dijitali sasa utakuwa mkombozi na mwarobaini kwa wacheza filamu nchini.
Ni kweli utakuwa mkombozi kwa sababu kuu moja tu, kwani hivi sasa msanii/ kikundi cha wasanii kinaweza kujikusanya na kuamua kucheza filamu ya hadithi watakayotunga na kukubaliana bila kujali ndani ya filamu hiyo msanii gani mwenye jina kubwa amecheza na wataweza kuiuza katika luninga na kujipatia mkate wao wa kila siku.
Kwakuwa Tanzania inatarajiwa kuingia katika idadi ya nchi ambazo zitakuwa zimetekeleza kwa vitendo maazimio ya Tume ya Kimataifa ya Mawasiliano ( ITU), kwa kuchukua uamuzi wa kutoka katika mfumo wa utangazaji wa analojia na kuingia katika mfumo wa dijitali, ukoloni wa filamu kuuzika ama kuchezwa na wasanii /msanii nyota sasa utakufa kwa kufuatia mfumo huu wa dijitali.

Ni vigumu kukubaliana na mimi lakini hivi ndivyo itakavyokuwa kwani kitakachoangaliwa katika luninga nyingi ni ubora na maudhui ya filamu na si umaarufu wa msanii kama lilivyo soko la sasa.
Hivyo basi, kwa hatua hii tunatarajia kwamba wasanii wengi chipukizi wataweza kuonesha vipaji vyao, hali itakayozalisha ajira kwa vijana wa kada mbalimbali nchini.
Yale mazoea ya wasambazaji kugubikwa na ugonjwa ndugu wa kutoithaminisha filamu hadi iwe na msanii mwenye jina kubwa sasa wamepata mwarobaini wake.
Unyonyaji utapungua na hata kama utakuwepo hautakuwa mkubwa kiasi cha kutisha kama ilivyo sasa. Malipo kwa vikundi vya sanaa katika kila luninga wanayoonesha vitakuwa wazi, si siri kama ilivyokuwa enzi za analojia.
Enzi za analojia wasanii wengi walinyimwa haki zao huku wengi wao wakijikuta wakiigiza kwa lengo la kujenga jina tu na si kupata malipo.
Sasa wakati umefika ambapo kila msanii atakayeonekana kwenye luninga ahakikishe kwamba amepata haki yake ipasavyo na si kuuza sura kama ilivyozoeleka.
Kama hiyo haitoshi, ni bora katika kipindi hiki cha dijitali kila msanii akajipanga kuleta ushindani kwa msanii mwingine ili kuleta ufanisi zaidi katika kazi, kwani kazi ikiwa nzuri ndiyo italeta sifa na kumjengea jina mhusika.
Hivyo basi kuingia katika teknolojia hii kusiwape kiburi wasanii na wasambazaji nao wasivunjike moyo, kadhalika wenye kusimamia vipindi katika luninga mbalimbali endeleeni kupokea kazi za wasanii wachanga endapo tunataka kuvumbua vipaji vya wasanii wapya.
Katika hili hatutegemei kuwa na mfumuko wa vipindi ili mradi tu kwamba wewe una fedha basi, ndiyo iwe mfumuko wa vipindi vya tamthilia mbalimbali.
Nasema hivyo kwa sababu kama jinsi ilivyo katika muziki wa kizazi kipya na hata muziki wa dansi, kwani mtu akijiona ana fedha tu, hukurupuka na kuanzisha bendi bila ya kujiangalia kama ana kipaji cha fani husika ama ni kufuata mkumbo.
Mwaka 2013 tufanye kazi kulingana na kipawa cha mtu na si mradi kukurupuka tu kwa kuwa una rasilimali watu na fedha za kutosha kufanya kile unachokitaka, hapo tutakuwa tunapotosha maana halisi ya fani na usanii kwa ujumla.
Ni wazi kwamba kila mtu ana uwezo wa kuwa na fani zaidi ya moja lakini je, inakuwaje kwa wale ambao wanalazimisha kuwa wasanii?
Tunatarajia kwamba Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF) sasa ndio wakati muafaka wa kufanya kazi na kuonesha jinsi wanavyowajibika mbele ya jamii, fuatilieni kazi zote kwani mfumo wa dijitali unaweza kuwafanya mbweteke na kusababisha kazi kwenda hewani ikiwa na upungufu.Habari na freemedia

No comments:

Inspirational Prayer of the Day

choose your favorite language

GEITA DOCUMENTARY

HABARI NYINGINE ZAIDI