Tuesday, 16 October 2012
KAMANDA BARLOW KUAGWA LEO DAR ES SALAAM
BAADA ya kuagwa na maelfu ya watu katika Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza jana, leo aliyekuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, marehemu Liberatus Barlow ataagwa Dar es Salaam
Jana saa 4.15 asubuhi msafara wa magari kutoka Pasiansi, nyumbani kwa marehemu uliingia katika uwanja huo uliokuwa tayari umefurika watu kuanzia saa 2 asubuhi huku wengine wakiendelea kuingia.
Kuagwa kwa Barlow kulitanguliwa na Misa iliyoongoza na Padri Raymond Mayanga na baadaye watu mbalimbali walipata nafasi ya kutoa salamu zao. Na baada ya shughuli hiyo mwili huo ulisafirishwa kwenda Dar es Salaam iliko familia yake.
Ratiba Dar Leo mwili wa Kamanda Barlow unatarajiwa kuagwa kuanzia saa tano asubuhi katika Kanisa Katoliki Ukonga. Kwa mujibu wa taarifa ya Polisi, baada ya kuagwa, mwili utasafirishwa kwenda nyumbani kwao Kilema, Moshi Vijijini, Kilimanjaro kwa maziko yatakayofanyika kesho mchana kwa kufuata taratibu za kidini na kuhitimishwa na taratibu za kijeshi.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Polisi nchini (IGP) Said Mwema, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini (DCI), Robert Manumba alisema Polisi itahakikisha inakamata wote waliohusika na mauaji ya Kamanda Barlow sambamba na mauaji ya vikongwe, wenye ulemavu wa ngozi na wanaochukua sheria mkononi.
“Huu ni wakati wa kutafakari, tukio hili linatufundisha nini katika kuwekeza kwenye mapambano dhidi ya uhalifu wa kijambazi, migogoro ya kidini, koo, viongozi wa siasa kuhamasisha wafuasi kufanya vurugu, kuelekeza mashambulizi kwa vikongwe, albino na utamaduni wa kuchukua sheria mkononi bila kujali kama kuna Mahakama.
“Tujiulize, tunapowekeza kwenye vurugu tunalipeleka wapi Taifa, kwani kinachodumu kwenye jamii ni usalama na amani ambavyo vitatuwezesha kufanya shughuli zetu,” alisema Manumba.
RC asema ni unyama Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Evarist Ndikilo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa alisema mkoa umepata pigo kwa RPC kuuawa.
Alisema saa chache kabla ya kifo chake, alikuwa ofisini kwake na viongozi wengine wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wakizungumzia masuala ya kikazi huku akitoa michango mizuri ya uboreshaji.
Alisema Jamii ya Watanzania imechukizwa na tukio hilo ovu kwa mtu ambaye alikuwa akiongoza Jeshi la Polisi kwa ufanisi mkubwa na kufanikiwa kupunguza uhalifu wa kutumia silaha, katika Ziwa Victoria, dawa ya kulevya na mauaji ya albino kwa kiasi kikubwa.
Padri Akiongoza Misa, Padri Mayanga alisema Kamanda Barlow alijitahidi kutumikia Watanzania wenzake kuhakikisha haki inatendeka na kama alikuwa na upungufu basi ni wa kibinadamu ambao kila mtu anao.
Alisema kifo cha Barlow kinatoa fursa ya kujifunza kwa kujiuliza kwa nini kimetokea katika hali hii na kila mmoja ajichunguze moyoni mchango wake ni nini katika hilo kwani watu wanashindwa hata kumwogopa Mungu.
“Maisha ya binadamu ni zawadi kutoka kwa Mungu na hakuna mwenye haki ya kuyatoa, Watanzania tumwogope Mungu, ndiyo maana maandiko yanasema heri walio wapatanishi wataitwa wana wa Mungu,” alisema.
Akiwasilisha salamu za Serikali kwa Niaba ya Waziri Mkuu, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera na Uratibu, William Lukuvi alisema Serikali imeshitushwa na kifo hicho.
“Natoa pole kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Mwema kwa msiba huu mkubwa, lakini pia niwape pole Mkuu wa Mkoa wa Mwanza na wananchi wote wa mkoa huu kwa kuondokewa na mtumishi wenu namba moja, najua wote tutakufa, lakini RPC wenu kwa mazingira haya ndivyo alivyoandikiwa kifo chake,” alisema.
Alitaka wakazi wa hapa kuondoa hofu ya kuondokewa na kiongozi wao kwa kuwa Serikali iko kamili katika kulinda mali na maisha yao na kuwataka waendelee na shughuli za uzalishaji mali kama kawaida.
Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk Chalres Tizeba alisema ameguswa na msiba wa Kamanda Barlow ambaye aliwahi kufanya kazi naye akiwa Mkuu wa Wilaya ya Sikonge, yeye akiwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tabora.
Naibu Waziri wa Maji, Dk Binilithi Mahenge, alisema kifo cha Kamanda Barlow ni pigo kwa Taifa na alitoa salamu za pole kwa Mkuu wa Mkoa, Polisi nchini na wakazi wa Mwanza.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment