SHRIKA la Ndege la Air Tanzania (ATCL), limejipanga kurudisha safari zake kuanzia Ijumaa hii na kuahidi kujikita katika safari za ndani na kimataifa.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za makao makuu ya shirika hilo jijini Dar es Salaam jana, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, Kapteni Milton Lazaro, alisema shirika lake limeanza kutekeleza mpango wa maendeleo utakaosaidia kuboresha utoaji huduma pamoja na upanuzi wa safari zake.
“Tumejipanga kurejesha huduma zetu Ijumaa hii huku tukiwa tumepanga kuongeza safari nyingine katika mkakati wetu wa kuhakikisha kuwa tunafika maeneo mengi nchini.
“Tutaanza na safari ya Dar es Salaam-Mwanza-Kilimanjaro kabla ya kuanzisha safari ya Dar es Salaam-Arusha-Zanzibar itakayozinduliwa Novemba 2.
“Tunawashukuru wateja wetu kwa kuwa nasi katika kipindi hiki kigumu tuliposimamisha huduma zetu na tunaahidi kuwapatia huduma bora na za kipekee kipindi tutakapoanza safari,” alisema Lazaro.
Lazaro aliongeza kuwa, shirika hilo lina mpango wa kuzindua safari ya Dar es Salaam-Mtwara itakayoanza Novemba 16, kwa kutumia ndege ya Dash 8-300 iliyokuwa katika matengenezo baada ya kuhusika kwenye ajali kipindi kifupi kilichopita.
“Changamoto kubwa sasa ni kujikita katika urejeshaji wa heshima ya shirika. Tumejipanga kununua ndege mbili mpya, ili kupanua huduma zetu na wakati mwingine tutaingia ubia na mashirika makubwa ya ndege, ili kuongeza safari zetu,” aliongeza.
Akizungumzia usitishwaji wa mkataba kati ya Kampuni ya ATCL na kampuni ya Aero Vista Agosti ambayo iliwakodisha ndege aina ya Boeing 737-500, Lusajo alisema mazungumzo kati ya kampuni hizo mbili yanaendelea na kusema wanategemea kufikia makubaliano muda si mrefu.
1 comment:
Awesome post, where is the rss? I cant find it!
Post a Comment