Thursday 27 September 2012

WALIMU KORTINI KWA WIZI WA MITIHANI


WALIMU wanne wa Shule ya Msingi Hamkoko na msimamizi mmoja wa mitihani, wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza kwa tuhuma za wizi wa mtihani wa taifa wa darasa la saba, huku Jeshi la Polisi likiendelea kumtafuta mwalimu mwingine aliyetoroka.

Watuhumiwa hao walisomewa mashtaka yanayowakabili na Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Inspekta Samwel Onyango mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo, Charles Bilomela.
Mwendesha Mashtaka alidai mahakamani hapo kuwa washtakiwa hao kwa pamoja walitenda makosa hayo Septemba 19, mwaka huu majira ya saa 5:10 asubuhi katika Shule ya Msingi Hamkoko.
Alisema washtakiwa hao wanakabiliwa na tuhuma za makosa ya kula njama na kutenda kosa wakiwa watumishi wa umma, wizi wa mtihani wa taifa wa darasa la saba pamoja na kupatikana na nyaraka za serikali mali ya Baraza la Mitihani kinyume na sheria kifungu cha 183 cha makosa ya jinai.
Kwa mujibu wa Mwendesha Mashtaka washtakiwa hao walikamatwa nyumbani kwa Mwalimu Kija Songoli wakiendelea na harakati za kuandaa majibu ya mtihani wa Hisabati kwa lengo la kuwasaidia wanafunzi.
Walimu hao ni Kija Songoli (30), Jenifreda Edward (28), Mariam Kateti (26) na Marycelina Malisel (25) na Msimamizi wa Mitihani wa Taifa wa darasa la saba, Leonida Anthony (32).
Mwalimu mwingine aliyetambuliwa kwa jina la Diana Shishanga anayetuhumiwa kushiriki kutenda makosa hayo, anatafutwa na polisi ili aunganishwe na wenzake baada ya kutoroka.
Watuhumiwa hao walikana mashtaka na kesi hiyo itafikishwa tena mahakamani Oktoba 8, mwaka huu. Wapo nje kwa dhamana.

No comments:

GEITA DOCUMENTARY

Contributors