MAGONJWA mengi yasiyoambukiza yakiwemo shinikizo la damu, kisukari na moyo huwaandama wananchi wengi kutokana na ulaji wa vyakula usiofaa pamoja na kutofanya mazoezi.
Hayo yalibanishwa jijini Dar es Salaam jana na Rais wa Chama cha Wauguzi nchini (TANNA), Ntuli Mwambingu, alipozungumza na waandishi wa habari alipokuwa akizungumzia mkutano mkuu wa chama hicho utakaofanyika kati ya Septemba 26 na 28 mwaka huu mjini Morogoro, wenye kauli mbiu ‘changamoto wanazopata wauguzi katika kuhudimua wagonjwa wenye magonjwa yasiyoambukiza’.
Alisema pamoja na vyanzo hivyo vya magonjwa hayo, vitu vingine ni unywaji pombe kupita kiasi pamoja na uvutaji wa sigara.
“Hivi sasa mtindo wa maisha umebadilika sana, watu wameacha kula vyakula vya asili na kula vya fast food ambavyo sio vizuri… pia uandaaji wa vyakula vyetu siku hizi umebadilika, unakuta mtu amejaza mafuta na watu hawafanyi mazoezi, wanatumia sana magari hata kwa mwendo mfupi. Mambo haya na mengi yanasababisha magonjwa ya moyo na shinikizo la damu.
“Tumegundua wabunge wengi wanakabiliwa na matatizo haya, hivyo jamii inapaswa kuelimishwa ili kujiepusha na magonjwa haya,” alisema.
Alisema magonjwa hayo yamekuwa yakisababisha vifo vingi duniani kwa nchi tajiri na masikini na kuongeza kuwa karibu asilimia 80 ya vifo hivyo hutokea katika nchi zinazoendelea na zisizoendelea.
“Magonjwa hata yameathiri rika zote, lakini tafiti zinaonyesha zaidi ya vifo milioni tisa vinavyohusiana na magonjwa yasiyoambukiza vinatokea chini ya umri wa miaka 60,” alisema.
Kwa upande wa Tanzania, alisema vifo hivyo vimeongezeka na kufikia kati ya asilimia 15 hadi 28 kwa mwaka.
Pamoja na mambo mengine, alisema mkutano huo utasisitiza namna ya kuboresha taaluma ya uuguzi nchini na kuhamasisha wauguzi wengi kujiunga na chama kutoka idadi iliyopo ya wanachama 8,000.
Kwa upande wake, Mweka Hazina wa chama hicho, Kulwa Kaombwe, alisema idadi ya wauguzi nchini bado ni ndogo, kwani badala ya muuguzi mmoja kuhudumia wagonjwa sita hadi nane kwa viwango vya kimataifa, hapa nchini muuguzi mmoja huhudumia wagonjwa 60 hadi 80.
No comments:
Post a Comment