Monday 10 September 2012

Nyakua Nyakitita: Mhadhiri DIT anayeokota makopo barabarani


WASWAHILI siku zote husema hujafa hujaumbika! Ukweli wa usemi huu unatimia unapomwona mtu huyu.
Ungemwona miaka 13 iliyopita ungeshangaa, lakini leo mtu aliyeitwa mstaarabu, bondia wa kutegemewa na mcheza twist wa ukweli, Nyakua Nyakitita amebadilika kweli.

Mtu ambaye alikuwa mhadhiri wa kutegemewa katika Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), msomi aliyebobea katika uhandisi, kazi aliyoianza katika miaka ya 1990, sasa anaishi kwa kuombaomba, kuchora ramani na mambo yasiyojulikana!

Leo hii, msomi huyo yuko katika hali ya kusikitisha ya uchafu uliokithiri, anashinda karibu na maeneo ya chuo hicho makutano ya Barabara za Morogoro na Bibi Titi Mohammed  huku akiokota makopo na takataka nyingine na mara nyingine akikusanya mawe na kuyapanga kwa kutengeneza michoro ya vitu mbalimbali ikiwamo ramani ya Tanzania na  kuandika majina ya marafiki zake.

Nini kilichomsibu hadi kufikia hapo? 
Kabla ya kupata matatizo ya akili mwalimu  na mhandisi Nyakua aliishi maisha mazuri tu ambayo kwa vijana wa sasa wanasema, ‘yalimtoa’ kwani alitembelea nchi kadhaa kwa ajili ya ziara za mafunzo au kozi ndefu na ambazo zilimpa fursa nzuri ya ‘kujirusha’.

Watu walio karibu na mwalimu huyo wanasema alikuwa kijana mwerevu kweli kweli aliyefanya vyema katika masomo yake kote alikopita.
Kaka yake, , Peter Murya, anasema mdogo wake alikuwa na mwanzo mzuri kimaisha tangu anazaliwa mpaka anapata shahada zake mbili.
Anasema alikwenda kusoma nchini Urusi ambako alikaa kwa miaka saba na aliporudi alikuja akiwa na mke raia wa nchi ile  (Urusi) ambaye walibarikiwa kuwa na watoto wawili.
“Nadhani walifunga ndoa huko huko kwani walikuja tayari wakiwa na watoto wawili, wa kiume Paulus na wa kike Masha,” anasema Peter
Anaongeza kuwa mdogo wake aliporudi kutoka Urusi aliajiriwa katika  Shirika la Viwango  Tanzania (TBS)  na baada ya mwaka mmoja alipata mwanamke mwingine Mtanzania na hakutaka ushauri wa yeyote kuhusu suala hilo.
“Wakati anamwoa huyo mwanamke wa Kinyamwezi, hakutaka hata mama yake mzazi afike,” anasema Murya.
Anasema dalili za awali za maradhi yake zilianza kwa kushika Biblia na kuhubiri, jambo ambalo liliwatisha  ingawa si kwa kiasi kikubwa na hakuchukua muda kabla ya kwenda nchini Sweden kwa masomo ya  mwaka mmoja na nusu.
“Lakini, hakukaa sana huko kabla ya kurudishwa akiwa chini ya ulinzi wa polisi, polisi wa uhamiaji walituambia kuwa Nyakua amechanganyikiwa,” anasema
Anaongeza kuwa watoto hao wawili wapo hapa jijini ingawa Masha hajulikani ni eneo gani  anakoishi , lakini Paulus yupo Kwembe kwa shangazi yake.
Kuhusu matibabu, Murya anasema walijaribu kuhangaika sana  kwa tiba mbalimbali ikiwemo ya mitishamba, maombi na hata Hospitali ya Mirembe iliyoko Dodoma, kote  bila mafanikio na sasa wanasubiri muujiza wa Mungu ili aweze kumponya kaka yao.
Kauli ya Nyakua
Siku niliyokutana naye (Nyakua),alikuwa amevalia koti, t-shirt, suruali nyeupe na miguuni alikuwa amevaa viatu vya aina tofauti, mguu mmoja raba na mwingine  viatu aina ya ‘yeboyebo’.
Nilimwambia  nitampa fedha ndipo nilipoweza kufanya mazungumzo naye.
Nyakua akasema kuwa miongoni mwa mambo yaliyomsababishia maradhi hayo ni kujihusisha na siasa za vyama vingi ambapo anadai alimsaidia  Rais wa awamu ya tatu Benjamin Mkapa katika kampeni zake mwaka 1995.
Anapoulizwa kuhusu familia yake, Nyakua akasema: “Watoto wangu, Paulus na Masha wapo Kwembe, mke wangu yupo Urusi, nilikuwa huko miezi miwili iliyopita, hajambo kabisa. Hata kama tuligombana, lakini si amenizalia watoto bwana,”
Anasema: “Unajua Masha na Paulus wamefuatana sana kuzaliwa, Masha ni wa 1980 na Paulus ni wa 1981”
Hajasahau kiwango cha elimu yake na anasema: ‘Masters’ nimesomea Urusi, PhD  Sweden, na  wiki ijayo nataka nikachukue kozi ya udaktari”
Kuhusu majina ya Nzowa na Dina anaanza kucheka, kisha anajibu: “Nawapenda wale, hadi leo bado nawapenda.”
Anapohojiwa zaidi kuhusu kilichomfanya awe katika hali hiyo Nyakua anajibu hivi: “Siasa za vyama vingi ndizo zilizonifanya niwe hivi. Nilimfanyia kampeni Rais Mkapa hadi  akaingia madarakani, lakini hakunipa alichoahidi.”
Anaongeza: “Nilitakiwa aidha niwe Ikulu, jeshini au kule kwingine.”
Anapodadisiwa zaidi anajibu: “Unanipa hela au niondoke zangu, mbona unanichimba wewe.”
Anapoelezwa  kuwa  nahitaji kumpiga picha na bila kusita anapozi huku akinitaka  tukalifanyie zoezi hilo kwenye kivuli ili picha zitoke vizuri na  nimpelekee ‘negative’  ili akasafishe.
Shughuli za Nyakua
Aghalabu, Nyakua huketi nje ya uzio wa chuo cha DIT kisha huanza kuchora ramani ya Tanzania  au ya Afrika akitumia mawe aliyoyaokota baharini.  
Ndani ya ramani hiyo, Nyakua hutengeneza  vyumba vyumba, ambavyo hakuna mwenye uhakika kama ni mikoa ya nchi au ni vyumba tu.
Kisha huchora alama ya moyo na kuandika majina ya watu wawili kwa herufi kubwa, majina hayo ni Dina na Nzowa au Nyakua. Huweka viatu vya kike, pamoja na kikombe katika ramani hiyo. Wakati mwingine, Nyakua huandika neno NBAA au MME.
Anapenda kuwaomba fedha wahadhiri wa DIT na wanapompa, basi hukimbilia maeneo ya Keko na kununua pombe.
Wakati mwingine Nyakua hulala katika makutano ya barabara kuu inayotokea Mnazi Mmoja kuelekea Posta karibu na kituo cha Akiba.
Rafiki yake wa karibu, Dk Ambogo Nathan, ambaye ni mhadhiri katika kitengo cha Uhandisi  cha DIT anasema anamfahamu Nyakua kama ndugu, mfanyakazi  na mwanafunzi mwenzake.
Dk Ambogo anasema Nyakua alikuwa ni kiranja wao  walipokuwa shule, mcheza masumbwi mahiri na mwerevu mno katika masomo yake.
Mhandisi Ambogo ambaye  ni mwenyeji wa Mkoa wa Mara kama alivyo Nyakua anasema:  “Nyakua alikuwa na uwezo mkubwa darasani, uwezo wake ulijulikana kwa kila mtu, alikuwa ni boxer (bondia) mzuri kweli”
Nyakua na Dk Ambogo walikwenda masomoni Urusi kusomea Shahada ya Kwanza ya Uhandisi na wakafanikiwa pia kuipata pia ya pili.
“Nyakua alitangulia kwenda Urusi kwa kuwa alinizidi mwaka mmoja kimasomo,  hata hivyo yeye alikuwa mji wa Baku ( mji mkuu wa sasa wa nchi ya Azerbaijan) na mimi nilikuwa Moscow,” anasema
Anasema Nyakua akiwa masomoni alipata mwanamke wa Kirusi na alimuoa akiwa huko huko na baada ya kumaliza masomo yake, alirudi naye Tanzania.
Anaendelea kusema kuwa   baada ya kurejea nchini alifanya kazi katika Shirika la Viwango Tanzania(TBS)  na alipata bahati nyingine ya kwenda masomoni nchini Sweden  kwa ajili ya kozi fupi.
“Baada ya kurudi Sweden ndipo nilipoona mabadiliko makubwa. Alianza kuwa mlevi kupindukia” anasema
Anasema pamoja na ulevi huo bado alikuwa ni mwalimu mzuri na alipata kazi katika chuo hicho wakati huo bado hakijabadilishwa kuwa taasisi.
“Alifundisha hapa kwa muda hadi mwaka 1999 alipohamishiwa wizarani ( Sayansi na Teknolojia),” anasema.
Dk Ambogo anahisi kuwa uhamisho wa Nyakua ulitokana na utendaji mbovu kazini uliotokana na ulevi.
“Ulevi huo ulienda sambamba na kuzungumza peke yake, kuokota makopo, kuchorachora ramani hapo mbele ya chuo  na mambo mengine mengi tu,” anasema
Anasema  kwa sasa Nyakua ana uwezo wa kuelewa na kuzungumza mambo mbalimbali,  anazo kumbukumbu za watu aliofanya nao kazi hapo zamani, lakini anastaajabisha katika baadhi ya mambo kama kulala barabarani, kula majalalani na  kujisaidia katika mavazi yake.
Anaongeza kuwa baadhi ya ndugu zake walimkamata na kumrudisha kijijini kwao, huko Mara, lakini alirejea jijini kwa kutembea kwa miguu, jambo ambalo analikiri hata yeye mwenyewe (Nyakua).
Mkuu wa Kitengo cha Uhandisi, Dk Frederick Mgonja anasema  Nyakua alijiunga na taasisi hiyo mwaka 1995, wakati huo DIT  haijabadilishwa kuwa taasisi.
Anamtaja kuwa ni  miongoni mwa wahadhiri werevu  hapa nchini, kwani alikuwa na uwezo wa  kufundisha kwa ufanisi karibu kila fani katika kada ya teknolojia.
“Nyakua ni miongoni mwa wafanyakazi wazuri sana. Tunasikitishwa kwa kupoteza nguvu kazi hiyo muhimu,” anasema  
Historia yake inaonyesha kuwa Nyakua alianza kazi mwaka 1995 na aliendelea kufanya kazi hadi mwaka 1999  wakati ambapo chuo kilibadilishwa na kuwa taasisi.
Dk Mgonja anasema Nyakua anapenda kukaa maeneo ya DIT kwa kuwa ana kumbukumbu ya muda mrefu ya mahali hapo kwani licha ya kuwa mhadhiri lakini pia  aliwahi kuwa mwanafunzi  wa chuo hicho wakati huo taasisi hiyo ilikuwa  ikiitwa Chuo cha Ufundi Dar Technical College  wengi wakiita Dar Tech.
“Alisomea hapa hapa DIT, masomo ya ngazi ya cheti, ambapo alitunukiwa cheti na  kufuzu  FTC kabla ya kwenda Urusi na Sweden,” anasema.
Kuhusu matibabu, Dk Ambogo anasema chuo kilifanya utaratibu wa kumpeleka katika kituo cha wagonjwa wa akili cha Rutindi, Tanga ambako alitibiwa na kupona, lakini baadaye hali ilirejea tena.

“Inasikitisha kwa mtu kama Nyakua kuwa vile, kwani ni msomi na angekuwa na maisha mazuri iwapo angekuwa mzima,” anamaliza Dk Ambogo
Rafiki  mwingine  wa Nyakua, Kanuti Baregi ambaye ni mwalimu wa ufundi katika chuo cha DIT, anasema Nyakua alikuwa ni rafiki mzuri na walifanya mambo mengi pamoja.
Anayakumbuka matendo ya kufurahisha ya Nyakua, kama kucheza ‘twist’ kwa umaridadi mkubwa, ambao  anasema ulimwezesha kupata zawadi mara nyingi katika maisha yake.
“Wakati ule, kila Ijumaa tulikuwa tunakwenda kustarehe katika ukumbi wa Vijana ulioko Kinondoni ambao unaweka nyimbo za zamani, halafu linakuwepo shindano la kucheza twist. Nyakua alikuwa akiibuka mshindi kila siku.
“Zawadi kubwa ilikuwa ni kupewa kreti la bia, wakati ule ni  bia  aina ya bingwa au safari,” anasema Kanuti
Antunansile Nzowa, ni mhadhiri ambaye jina lake limekuwa likiandikwa kwa mawe  na Nyakua mara kwa mara mbele ya chuo cha DIT.
Nzowa anasema anakoseshwa amani na kushangazwa na kitendo cha Nyakua kuandika jina lake.
Anasema yeye na Nyakua  ingawa walisoma nchini Urusi pamoja, lakini hawakuwa na mazoea ya ukaribu sana na walikuwa wakiishi miji miwili tofauti.
“Mimi mwenyewe kitendo cha Nyakua kuniandika kinanikosesha raha, lakini sina la kufanya, ila nahisi anapenda kuniandika kwa sababu mimi ni shemeji yake, yeye ni kabila moja na mume wangu,” anasema Nzowa.
Anasema hakuwa na mazoea ya karibu na Nyakua zaidi ya ushemeji na kuwa mfanyakazi mwenzake.
Kuhusu ugonjwa wa akili alionao Nyakua,Nzowa anasema wahadhiri chuoni hapo wamekuwa wakijiuliza chanzo cha maradhi ya Nyakua na wamekuwa wakishindwa kupata jibu.
“Mwanzoni tulidhani anaigiza au ni mpelelezi kwa sababu anaonekana ana akili zake. Anawakumbuka watu na mambo yote aliyowahi kuyafanya hapa chuoni. Lakini kinachotuchanganya ni jinsi anavyojichafua kwa kinyesi na kulala barabarani” anasema  na kuongeza:
“Kwa kweli tumepoteza nguvu kazi muhimu. Nyakua alikuwa na uwezo mkubwa kitaaluma.”


habari na mwananchi communication 

2 comments:

Anonymous said...

Kwakweli hii habari inasikitisha sana. cjui ni nini Mungu wangu.

Anonymous said...

… Unbelievable , but I just found software which can do all hard work promoting your vicky-kamata.blogspot.com website on complete autopilot - building backlinks and getting your website on top of Google and other search engines 1st pages, so your site finally can get laser targeted qualified traffic, and so you can get lot more visitors for your website.

YEP, that’s right, there’s this little known website which shows you how to get to the top 10 of Google and other search engines guaranteed.

I used it and in just 7 days… got floods of traffic to my site...

…Well check out the incredible results for yourself -
http://auto-website-promoter.com

I’m not trying to be rude here, but I believe when you find something that finally works you should share it…

…so that’s what I’m doing today, sharing it with you:

http://auto-website-promoter.com

Take care - your friend Jessica

GEITA DOCUMENTARY

Contributors