Monday, 13 August 2012

Wasanii walia na kigogo anayehujumu kazi zao


WASANII wa Tanzania, wamemlilia mkazi mmoja wa jijini Dar es Salaam kutokana na kubobea katika kuhujumu kazi zao, hivyo kuamua kuungana pamoja kupambana na wezi na maharamia wa kazi zao.
Akizungumza jijini Dar es Salaam juzi, Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF), Simon Mwakifamba, alisema, wamembaini mtu anayeitwa ‘Msukuma’ ambaye amekuwa akijitajirisha kutokana na wizi wa kazi za wasanii.
“Huyu Msukuma ndiyo umaarufu wake, ana mbinu nyingi za kimataifa za kufanya, kwani hana hofu na dhuluma anayoifanya ya  ubadhirifu wa kazi za wasanii,” alisema na kuongeza:

“Huyu mtu ni hatari sana, kwani alikamatwa na mitambo ambayo inasaidia katika kudurufu kazi za wasanii, lakini hivi sasa ameweza kununua mtambo mwingine, hali ambayo inaonesha kuwa ana mtandao mkubwa unaomsaidia, hivyo tunaiomba serikali imchukulie hatua kali.”

Mwakifamba, aliyataja maeneo ambayo ndiyo machimbo ya wizi wa kazi za wasanii, ambako watu wameweka mashine za kudurufu kuwa ni Buguruni, Yombo, Tegeta na Mbezi Mwisho.
Naye Mwenyekiti wa Bongo Movie, Jacob Steven ‘JB’ ameiomba serikali kunusuru sekta ya filamu na wizi huo uliokithiri na kurudisha nyuma maendeleo ya taifa.

“Kusema kweli, wasanii tuna hali mbaya, hawa wezi wako dunia nzima, lakini hapa kwetu Tanzania wamekithiri, kwani wanaiba bila woga, tena mbele ya macho yako, hali inayopelekea kutishia uhai wa wasambazaji wetu, kwani wapo waliojitoa kufanya kazi ya usambazaji kutokana na kutopata faida,” alisema JB.
Aliongeza kuwa, hata wasambazaji walionao hivi sasa, Steps Entertainment, nao wametetereka sokoni kutokana na kuathirika na wizi wa kudurufu kazi hizo.Habari na Freemedia

No comments:

Inspirational Prayer of the Day

choose your favorite language

GEITA DOCUMENTARY

HABARI NYINGINE ZAIDI