Tuesday, 10 July 2012

Wanaoiibia Tanesco watangaziwa ‘kiama’


  1.  

Mkurugenzi wa Shirika la Umeme nchini (Tanesco), William Mhando
MKURUGENZI wa Shirika la Umeme nchini (Tanesco),  William Mhando amefanya ukaguzi wa mita za wateja baada ya kupata taarifa za kuwapo kwa watu wanaotumia umeme bila kulipia.Zoezi hilo ambalo lilifanyika jana Kanda ya Temeke jijini Dar es Salaam, Mhando alisema   walipokea taarifa  za wizi wa umeme kwa njia ya mtandao hali iliyomlazimu kufuatilia kwa makini kuanzia ngazi ya chini.

Alisema tangu zoezi hilo kuanza wamefanikiwa kuwakamata watu wawili mkoani Dodoma na watatu jijini Dar es Salaam ambao kesi zao zimefikishwa mahakamani wakituhumiwa  kutumia umeme ambao haujulikani umenunuliwa wapi.

“Utakuta mteja amenunua umeme wa Sh10,000 kwetu lakini unapokwenda kukagua utakuta ana umeme wa zaidi ya pesa hiyo na hii inamaanisha kuna sehemu zingine wananunua tofauti na Tanesco ambapo kwenye mfumo haupo,” alisema  Mhando. 

Mkurugezni huyo alifafanua kuwepo kwa tatizo hilo ambapo alisema kuwa, kuna uwezekano mtaalamu aliyekuja kuingiza mfumo huo aliacha programu mtaani na kufanya watu wenye nia mbaya kutumia nafasi hiyo.

“Tatizo hili limegundulika haraka kutokana na mita maalumu (Automatic Meter Reader) zilizofungwa ambazo husomwa moja kwa moja kwenye ofisi zetu bila ya kwenda kwa mteja na ndiyo maana tumeweza kuwabaini na tutaendela kuwabaini,” alisema Mhando na kuongeza:

Tumeanza kufunga mfumo mwingine wa kudhibiti wizi aina hiyo kwa kufunga kifaa maalumu (Supply Group Hold) ambacho hadi sasa kimefungwa kwa wateja wakubwa 3,000 jijini Dar es Salaam na kudhibiti wizi wa aina hiyo na zoezi hilo litaendelea kwa wateja wa kawaida.

Mbali na wizi wa mtandao mkurugenzi huyo aliamuru wateja wake wawili kukatiwa umeme na kulitaka Jeshi la Polisi kuwachukulia hatua baada ya kujiunganishia umeme kabla haujafika kwenye mita.
Katika eneo la Keko mbali na nyumba za kawaida, umeme ulikatwa kwenye nyumba za wageni pamoja na baa mbalimbali zikiwamo Baa ya Miami Shambwe  na King Paris zilizopo kwenye eneo hilo.

Kwa upande wake  Meneja wa Kanda Richard Mallamia alisema, hasara inayotokana na wizi wa umeme ni zaidi ya Sh89 millioni kwa mwezi kwa watumiaji wa kawaida ambapo tangu kuanza kwa zoezi hilo wamefanikiwa kukusanya Sh40 milioni kutokana na faini pamoja na ukusanyaji wa madeni.

Tanesco hukusanya mapato mengi zaidi ya asilimia  80 kutoka kwa watumiaji wakubwa wa umeme ambao ni asilimia 20 ya wateja wote na ndiyo sehemu waliyoanza kufanya udhibiti wa ufungaji wa vifaa maalumu vya kuzuia wizi.

Mhando alisema wamewafukuza wafanyakazi watano na wengine kesi zao zinaendelea mahakamani baada ya kuwanasa na mitego ya rushwa.

No comments:

GEITA DOCUMENTARY

Contributors