Monday 9 July 2012

Ukosefu wa nishati vijijini ni janga la taifa


 

NI miaka 50 sasa tangu Tanzania ilipojipatia uhuru wake huku ikiendelea kuogelea kwenye lindi la umaskini. Siyo kwa sababu ya kukosa rasilimali, bali kutokana na sababu mtambuka.
Moja kati ya mambo yanayodhihirisha umaskini huo ni ukosefu wa nishati ya uhakika katika maisha ya kila siku na kwa maendeleo ya taifa.
Ni kweli tuna umeme wa Gridi ya Taifa, lakini hadi sasa umeme unatumiwa na asilimia 14 pekee ya Watanzania. Maana yake, hadi sasa asilimia 86 ya Watanzania hawana umeme huo, badala yake ama wanatumia umeme unaozalishwa kwa jenereta, jua au njia nyingine zisizo za uhakika.
Asilimia 14 ya hao wanaotumia  umeme ni wanaoishi mijini huku pia kukiwa na viwanda vichache vinavyozalisha bidhaa kwa masoko ya ndani na nje.

Watanzania wengine asilimia 80 ya wanaoishi vijijini hubaki wakitumia misitu kama chanzo kikuu cha nishati kwa kukata miti ili kupata kuni na kuchoma mkaa.
Kwa jumla, asilimia 90 ya nishati inayotumika nchini inatokana na mimea yaani matumizi ya mkaa na kuni huku asilimia nane pekee ya nishati inayotumika nchini hutokana na mafuta na kiasi kilichobaki hutegemea maji.
Matumizi ya kuni na mkaa huchangia kwa kiasi kikubwa uharibifu wa mazingira.
Takwimu za hivi karibuni zinaonyesha kuwa Tanzania ina ekari 33 milioni za misitu, ambazo ni sawa na asilimia 39 ya ardhi yake yote.
Lakini kutokana na uharibifu wa misitu hiyo, inakadiriwa kuwa kila mwaka Tanzania hupoteza hekta 500,000 za misitu ambapo hekta 300,000 sawa na kilometa za mraba 3,320 za misitu hupotea kwa kuchoma mkaa kila mwaka.
Katika matumizi ya mkaa, tafiti zinaonyesha kuwa Jiji la Dar es Salaam pekee hutumia magunia 35,000 ya kuni kwa siku, huku taarifa nyingine zikionyesha magunia kati ya 15,000 hadi 20,000 ya mkaa huingia Dar es Salaam kila siku.
Mikoa mingine inayotajwa kwa matumizi makubwa ya mkaa ni pamoja na Mwanza, Shinyanga, Tabora, Morogoro na Mbeya.
Benki ya Dunia inakadiria kuwa, kila mwaka Tanzania hutumia tani milioni moja za mkaa, huku Jiji la Dar es Salaam likitumia nusu ya mkaa huo kwa mwaka.
Kwa hali hiyo, wataalamu wanasema kuwa Tanzania itakuwa imemaliza misitu yote miaka 10 ijayo ikiwa juhudi za makusudi hazitachukuliwa kunusuru misitu. Hili ni janga linaloinyemelea Tanzania.
Pamoja na tishio hilo, bado Serikali haionekani kuchukua hatua madhubuti  ili kupambana nalo.
Serikali imejikita zaidi kwenye miradi ya umeme wa maji, gesi ili kutafuta suluhisho la nishati nchini.
Miradi hiyo siyo tu imeshindwa kupanua wigo wa watumiaji wa umeme, bali pia imeliingiza taifa kwenye kashfa za ufisadi huku baadhi ya viongozi wa Serikali na wafanyabiashara wakijinufaisha na miradi hiyo.
Mfano wa miradi hiyo ni mitambo ya Kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), ambayo iliwekwa kwa lengo kuongeza umeme kwenye Gridi ya Taifa.Hata hivyo, kuna wakati mitambo hiyo ilikuwa ikiligharimu Shirika la Umeme Tanzania(Tanesco) karibu Sh3 bilioni kwa mwezi, kiasi ambacho kilikuwa mzigo kwa shirika hilo.
Vilevile taifa lilishuhudia madudu kwenye mradi wa umeme wa dharura wa Kampuni ya Richmond na baadaye Dowans.
Ni hadithi ndefu, lakini ni ushahidi tosha kwamba viongozi wa Serikali wamepoteza mwelekeo katika kutafuta suluhisho la upungufu wa nishati nchini.
Kwa sasa Serikali imekuwa ikiendelea na mikakati ya matumizi ya gesi inayotoka mikoa ya Lindi na Mtwara katika kuongeza nishati hiyo kwenye Gridi ya Taifa.
Kwa mfano sasa upo mradi wa kusambaza gesi viwandani na majumbani unaofanywa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), ili kunusuru uharibifu wa mazingira.
Hata hivyo, mradi huo unakwenda taratibu ukilinganishwa na kasi ya uharibifu wa mazingira ilivyo sasa. Mradi huo unakabiliwa pia na upungufu wa fedha hata kabla haujafika mbali.
Kwa hali hiyo, bado kuna changamoto kubwa ya kumaliza tatizo la nishati hasa kwa kuwa miradi mingi inafanywa na kampuni za nje ambazo hulenga kupata faida zaidi kuliko kutatua tatizo husika.
Nadhani Serikali sasa inapaswa kuliangalia tatizo hili kwa mtazamo mwingine wa kutumia nishati mbadala. Kuna vyanzo vya nishati ambavyo iwapo Serikali itavipa kipaumbele, vinaweza kupunguza tatizo la nishati nchini na kuacha utegemezi wa misitu, mafuta na maji kama vyanzo pekee vya nishati.
Vipo vyanzo vingine kama vile upepo, mionzi ya jua na nishati mimea. Zipo taasisi zilizofanya tafiti na kubainisha vyanzo hivyo kama njia mbadala ya upatikanaji wa nishati hiyo.
Kwa mfano taasisi ya Haki Ardhi ya Dar es Salaam imefanya tafiti kuhusu matumizi ya mafuta ya mimea kama vile mibono ili kuendeshea mitambo kama vile jenereta na mashine nyinginezo.
Kama wananchi vijijini watahamasishwa kutenga maeneo yao na kulima zao hili, kuna uwezekano wa kukamua mafuta mengi, ambayo hufanyiwa marekebisho ya kikemikali ili kupata mafuta bora ya kuendeshea mitambo.
Shirika la kijasiriamali lisilo la kiserikali linalojishughulisha na uendelezaji wa nishati endelevu (Tatedo), pia limetoa mchango mkubwa katika utafutaji wa nishati mbadala.
Moja ya jitihada hizo ni uundaji na uagizaji wa mashine ambazo mitambo yake huendeshwa kwa mafuta ya mibono na huweza kufua umeme, kusaga na kukoboa nafaka.
Mashine moja ya aina hiyo huweza kuzalisha  umeme kwa kaya zipatazo 50, hivyo kama Serikali itanunua mashine hizo na kuhamasisha uzalishaji wa mafuta ya mibono, kuna uwezekano wananchi vijijini wakanufaika na nishati hiyo badala ya kusubiri umeme wa Gridi ya Taifa.
Zipo pia mashine za kutengeneza mkaa kwa kutumia pumba za mchele, karatasi na takataka za mbao. Mkaa huo licha ya kutumika kidogo kulinganisha na mkaa wa miti, hupunguza kwa kiasi kikubwa ukataji wa misitu unaotishia kuwepo kwa jangwa nchini.
Kuna uwezekano pia wa kutumia upepo katika kuzalisha umeme. Umeme huo una nguvu sawa tu na ule wa Gridi ya Taifa.
Kuna wakati Serikali ilikuwa na mkakati wa kuanzisha mradi huo mkoani Singida, hata hivyo haieleweki umeishia wapi. Mradi huo pamoja na mingine ya aina hiyo unaweza kabisa kukabili tatizo la ukosefu wa nishati nchini.
Zipo baadhi ya taasisi ambazo zimejikita kwenye uzalishaji wa umeme wa mionzi ya jua. Hata hivyo bado umeme huo haupewi kipaumbele kwa kuwa nguvu yake ni ndogo kulinganisha na vyanzo vingine.
Yapo mashirika mengi yanayofanya tafiti kuhusu nishati mbadala, lakini Serikali imewaachia wafadhili wahangaike nayo badala ya kuyakumbatia.
Ni kweli kuna wakala wa umeme vijijini (REA), lakini hapewi kipaumbele kama vyanzo vya umeme wa maji, mafuta na gesi.
Kwa kuwa kwa miaka yote 50 ya uhuru tumeishia kwenye asilimia 14 tu ya watumiaji wa umeme, huku mazingira yakiharibika kwa kasi, kuna haja ya kuchukua hatua madhubuti.
Kama Serikali katika bajeti zake ingejikita zaidi katika kuimarisha umeme vijijini ambako kuna Watanzania wengi  tatizo hili la nishati lingepungua kama siyo kwisha kabisa.
Lengo ni kutunza mazingira kwa kuzuia watu kukata miti ovyo na kuhakikisha kuwa wananchi wanapata nishati itakayowasaidia maishani mwao.
Serikali inapaswa kuunga mkono jitihada za taasisi, mashirika na watu binafsi wanaobuni njia za upatikanaji wa nishati mbadala, badala ya kuwaachia wahisani pekee.
Taasisi nyingi zimejitolea kupeleka nishati vijijini, lakini kutokana na ufinyu wa bajeti zao, zimeshindwa kufika mbali.
Serikali inapaswa kuziwezesha taasisi hizo kifedha kwa sababu wanaohudumiwa ni wananchi na mazingira yanayoharibiwa ni yetu sote.
Kinyume cha hapo, tunajipeleka kwenye janga la uharibifu mkubwa wa mazingira kwa sababu tu wananchi wanajitafutia nishati bila kujali uharibifu huo.

Kwa hisani ya Mwananchi Comm.

No comments:

GEITA DOCUMENTARY

Contributors