Thursday, 4 October 2012

Ajali yaua 10 Mbeya, mbunge anusurika




MBUNGE wa viti maalum mkoani Mbeya kupitia tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk. Mary Mwanjelwa, amenusurika kufa katika ajali mbaya iliyogharimu maisha ya watu takriban 10.
Katika ajali hiyo iliyotokea jana eneo la Mbalizi wilaya ya Mbeya Vijijini mkoani hapa, gari la mbunge huyo liligongwa na kuteketea kwa moto papo hapo.
Ajali hiyo imehusisha magari manne likiwemo lori la mafuta la kampuni ya Lake Oil lenye namba za usajili T 814 BTC, gari ndogo ya abiria (Hiace) yenye namba za usajili T 299 BCE na gari ya Mbunge huyo Mary Mwanjelwa Toyota Hilux T 671 ABM.


Watu takriban kumi wanaelezwa kupoteza maisha katika ajali hiyo huku wengine miili yao ikiwa imeteketea vibaya kwa moto baada ya gari hilo kugongana kisha kulipuka.
Idadi ya watu waliojeruhiwa akiwamo mbunge huyo, imeelezwa kufikia 25 huku wengine wakiwa katika hali mbaya.
Mashuhuda wa ajali hiyo wakiwemo majeruhi, walisema ajali hiyo ilisababishwa na lori hilo lililokuwa limebeba mafuta baada ya breki kufeli katika mteremko wa mlima Iwambi, hivyo kuliparamia lori jingine.
Baada ya lori hilo kuligonga lori jingine, ndipo likaigonga gari ya Mbunge Mwanjelwa kabla ya kuvaana uso kwa uso na gari la abiria lililokuwa likitokea katika eneo la Mbalizi.
Zoezi la uokoaji kwa mara ya kwanza lilifanywa na Koplo Mathias Joachim wa Kikosi cha Jeshi la Wananchi wa Tanzania 44 KJ Mbalizi Mbeya Karume Camp.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro, alifika eneo la tukio na alitoa pole kwa wafiwa kabla ya kuelekea Hospitali ya Ifisi Mbalizi kwa ajili ya kuwajulia hali majeruhi akiwemo mbunge huyo.
Mbunge Mary Mwanjelwa, akiwa hospitalini hapo alimshukuru Mungu kwa kumnusuru kisha akauliza hali ya dereva wake anayejulikana kwa jina moja la Rajab na katibu wake Muhtasi Amina.
Alipewa majibu ya haraka zaidi kwa lengo la kumridhisha; akaelezwa kuwa walikuwa wamekimbizwa hospitalini kwa matibabu zaidi.
Hata hivyo, ilielezwa kuwa dereva wake (Rajabu) ambaye alipelekwa katika hospitali hiyo ya Ifisi, alikuwa ameumia vibaya kichwani na miguu yote miwili huku Amina ikielezwa ni kati ya waliokufa katika ajali hiyo.
Aidha miongoni mwa watu waliopoteza maisha yumo pia askari polisi wa kituo kidogo cha Mbalizi aliyetajwa kwa jina la PC Samson.

No comments:

GEITA DOCUMENTARY

Contributors