Friday, 3 August 2012

MAHAKAMA YASITISHA MGOMO WA WALIMU


WALIMU nchini wazidi kubanwa baada ya mahakama Kuu ya Tanzania, Kitengo cha Kazi imesitisha mgomo wa walimu na kuwataka kurudi kazini mara moja.

Mahakama hiyo pia imeuagiza uongozi wa Chama cha Walimu (CWT) kuandaa taarifa kwa umma, kutangaza kusitishwa kwa mgomo huo kama walivyowatangazia wanachama wake wakati ulipoanza.Mahakama hiyo ilisitisha mgomo huo jana wakati ilipotoa uamuzi wa maombi yaliyowasilishwa mahakamani na Serikali. Jaji Sophia Wambura aliyekuwa akisikiliza maombi hayo, alisema mgomo huo ni batili kwa kuwa haukukidhi masharti ya Sheria ya Ajira na Uhusiano Kazini.

Katika uamuzi wake, mahakama hiyo pia imekitaka CWT kulipa hasara za kifedha au kuwafidia wanafunzi vipindi vya masomo walivyovikosa, hususan wale wa darasa la saba. Mahakama hiyo ilikwenda mbali zaidi na kuwaonya walimu na Serikali kwa kitendo cha kuzungumzia suala hilo wakati tayari lilikuwa mahakamani.

Jaji Wambura alisema kitendo hicho ni uvunjaji wa Ibara ya 4 na ya 107 A ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 kama ilivyokwisha kurekebishwa mara kadhaa.

“Vinginevyo, hakukuwa na haja ya kuja hapa mahakamani kabisa. Kama kila mmoja ataachwa awe jaji, itakuwa ni kero na uvunjaji wa utawala wa sheria,” alisema Jaji Wambura.

Jaji huyo alizitaka pande zote kurudi kwenye meza ya mazungumzo na kushauri kuwa, ikiwezekana zialike watu wenye ujuzi wa masuala ya sheria za kazi na uhusiano kazini kuwasaidia ili kufikia makubaliano kwa amani.

“Chini ya Masharti ya Kifungu cha 81 (1) (2) cha Sheria ya Ajira na Uhusiano Kazini, natamka kuwa mgomo ambao umekuwa ukiendelea kwa siku tatu sasa ni kinyume cha sheria. Ninaamuru usitishwe na walimu wote warudi kazini mara moja,” aliagiza Jaji Wambura.

Jaji Wambura alirejea hoja zilizowasilishwa na pande zote, waombaji wakiwakilishwa na Mawakili wa Serikali Wakuu, Obadia Kameya na Pius Mboya na wajibu maombi (CWT) wakiwakilishwa na Wakili Gabriel Mnyele.

Alisema baada ya kupitia hoja zote na vielelezo vilivyoambatanishwa kwenye hati za viapo pamoja na majibu husika, amebaini kuwa na kuridhika kuwa mgomo huo haukufuata sheria.

Alisema CWT hawakufuata masharti ya kifungu cha 80 (1), cha Sheria ya Ajira na Uhusiano Kazini na kwamba kulikuwa na dosari kwani kura zilizopigwa zilipotosha wanachama , kwa sababu hazikuwa za kuunga mkono mgomo, bali madai ya walimu.

Jaji huyo alisema upigaji kura ulikuwa ni batili kwani walimu hawakufahamishwa matokeo ya mgomo huo na kwamba haukuzingatia taratibu.

Pia alisema taarifa ya mgomo iliyowasilishwa kwa Katibu Mkuu Kiongozi Julai 27, 2012 saa 9:00 alasiri wakati mchakato wa upigaji kura ukiwa unaendelea, pia ilikuwa ni batili.

Dosari nyingine ni kutoeleza kikomo cha mgomo na kutokubainisha kama watawalipa wanachama wake wakati wa mgomo.

Aliongeza kwamba, CWT kwa kushindwa kutimiza masharti ya kanuni ya 42 na 43 za sheria husika, kulisababisha kero zisizo za lazima.

Alisisitiza kuwa kitendo cha CWT kuwasilisha taarifa ya mgomo Ijumaa saa 9:00 wakidai mgomo unaanza Jumatatu, hali wakijua kuwa Jumamosi na Jumapili hazikuwa siku za kazi, ni kinyume cha kanuni na kilifanywa kwa nia mbaya.
Wakili wa CWT, Mnyele alisema anasubiri maelekezo ya wateja wake, lakini Rais wa CWT, Gratian Mukoba alisema watatoa tamko leo.

No comments:

Inspirational Prayer of the Day

choose your favorite language

GEITA DOCUMENTARY

HABARI NYINGINE ZAIDI