Thursday, 28 June 2012

DOCTOR ULIMBOKA ATEKWA , NA KUJERUHIWA



Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk Steven Ulimboka ametekwa na watu wasiojulikana, kupigwa na kujeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili, kisha kutupwa katika Msitu wa Pande, nje kidogo ya jiji Dar es Salaam.Daktari huyo ambaye amekuwa akiratibu mgomo wa madaktari unaoendelea, aliokotwa na msamaria mwema akiwa amefungwa mikono na miguu akiwa katika hali mbaya.

Baada ya kuokotwa na wasamaria wema na kufikishwa katika Kituo cha Polisi, Dk Ulimboka aliwahishwa katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (Moi) kwa matibabu, na ilielezwa kuwa hali yake haikuwa nzuri.

Taarifa za kujeruhiwa kwa Dk Ulimboka zilisambaa kwa kasi katika vyombo vya habari, mitandao ya kijamii na ujumbe mfupi wa simu.



Kutokana na tukio hilo, wanaharakati wa haki za binadamu wameituhumu Serikali kuhusika na tukio hilo, huku Serikali ikikana tuhuma hizo, na papohapo ikiagiza Jeshi la Polisi kuwasaka waliohusika.

Akisimulia mkasa huo kupitia Kituo cha Redio cha Clouds FM, Dk Ulimboka alisema tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia jana katika klabu ya Leaders jijini Dar es Salaam, alikokuwa na wenzake wawili.

Alisema baada ya kukaa kwenye baa hiyo kwa muda, alianza kujisikia vibaya tofauti na siku zingine.

"Mara, katikati ya maongezi tukaona mtu anaongea na simu. Ghafla tukiwa tunasema tuagane, wakaja watu kama watano hivi na bunduki, wakasema wewe na yule bwana mko free (huru), tunakuchukua wewe (Dk. Ulimboka)," alieleza na kuongeza,

"Sijakaa sawa, nikaona nimeshaburutwa nikaanguka kwenye lami, wakaniinua na kuniingiza kwenye gari nyeusi, lakini ilikuwa haina namba."

Taarifa zaidi zilizolifikia Mwananchi kutoka Moi alikolazwa kwenye chumba cha uangalizi maalumu, zilieleza kuwa baada ya uchunguzi, ilibainika kuwa daktari huyo aliteswa vibaya, ikiwamo kuumizwa sehemu za siri, kuvunjwa meno kadhaa, mbavu na miguu.

Habari zaidi zilisema kuwa, baada ya kufikishwa katika Msitu wa Pande na kupata kipigo, alizimia kwa muda na alipozinduka aliwachomoka watekaji hao na kujaribu kukimbia. 

Msitu wa Pande ulioko wilayani Kinondoni, ndiko wafanyabiashara watatu wa madini kutoka Mahenge, Morogoro na dereva teksi wa Manzese Dar es Salaam waliuawa na polisi mwaka 2006.

Chanzo chetu cha habari kilisema, baada ya Dk Ulimboka kujaribu kuwatoroka watekaji, walipiga risasi mbili hewani, aliposimama wakamshika na kumpa kipigo na mateso zaidi, hivyo kusababisha avunjike maeneo mbalimbali ya mwili.

Polisi waunda tume
Jeshi la Polisi limeunda jopo kuchunguza tukio la utekaji nyara na shambulio la kudhuru mwili wa Dk Ulimboka.

Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema jana kuwa tukio hilo ni la aina yake na kwamba halijawahi kutokea hapa nchini.

Alisema jopo hilo ambalo linaongozwa na Kamishna Msaidizi wa Polisi, Ahmed Msangi linahusisha wapelelezi wa fani mbalimbali.
“Ni issue (jambo) ambayo imetokea bila kutegemea katika namna ambayo ina utata, hivyo kazi yetu ni kutegua utata huo,” alisema Kova na kuongeza:
“Hatutaki katika nchi yetu matukio kama haya yawe ya kawaida, tunataka liwe la mwanzo na la mwisho.”

Kamanda huyo alisema yeye alipata taarifa za kutekwa Dk Ulimboka usiku wa kuamkia jana saa 7 usiku.

Kwa mujibu wa Kamanda Kova, Dk Ulimboka aliokotwa na raia mwema katika eneo la Msitu wa Pande jana saa 2:30 asubuhi karibu na barabara huku akiwa na majeraha sehemu mbalimbali za mwili, ikiwamo kichwani na mikononi.
Alisema raia huyo (jina limehifadhiwa) alitoa taarifa katika Kituo cha Polisi Bunju, na askari walikwenda kwenye gari la raia huyo na kumkuta Dk Ulimboka wakamchukua na kwenda naye ndani.
 Kova alisema: “Aliyemuokota alisema alimkuta amefungwa mikono na miguu, na inaonekana kama watu hao walikuwa wanalipiza kisasi.”
Kwa mujibu wa kamanda huyo, akiwa kituoni hapo, Dk Ulimboka alijieleza kwamba juzi saa 5:30 usiku akiwa katika klabu ya Leaders na wenzake wanapata vinywaji pamoja na wateja wengine, walikuja watu watano na kuwatishia.
Alisema watu hao waliwataka walale chini na kwamba walitii, kisha watu hao walimchukua Ulimboka na kuwaambia wengine waendelee na vinywaji.
“Ulimboka alisema watu hao walikuwa na gari aina ya Escudo lenye rangi nyeusi na hili gari halikuwa na namba na walichukua ufunguo wake wa gari, nyaraka kadhaa na hela alizokuwa nazo,” alisema Kova.
Alisema akiwa katika gari hilo na watu wengine watano, ghafla walianza kumpiga huku wakiwa hawasemi chochote na kwamba baadaye walimfunika kichwani na fulana nyeusi hadi Msitu wa Pande.
Kova alisema baada ya maelezo hayo, Dk Ulimboka alitoa namba za simu za rafiki yake Dk Deogratius, na baada ya hapo alipewa fomu ya matibabu (PF3) na kupelekwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa matibabu.
Kamanda huyo alitoa wito kwa wananchi na mtu yeyote mwenye taarifa kamili kuhusu tukio hilo atoe taarifa, kwani lisipojulikana vizuri linaweza kuzua minong’ono mingi.
Askari ajeruhiwa MNH
Katika hatua nyingine, Kova alisema watu wasiojulikana wamemjeruhi Mkuu wa Upelelezi wa Kituo cha Polisi cha Selander Bridge ambaye alikwenda MNH kufanya upelelezi wa tukio hilo.
Kwa mujibu wa Kova, Mkuu huyo wa upelelezi alijeruhiwa wakati akiwa anaongea na simu, na kwamba watu hao pia walimpora vitu alivyokuwa navyo ikiwemo simu.
Mkurugenzi Moi

Mkurugenzi wa Tiba katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (Moi), Cuthbert Mchalo alisema majeruhi huyo alifikishwa hospitalini hapo saa 4:25  asubuhi, kwa msaada wa gari la wagonjwa la Kampuni AAR, kutoka Kituo Kidogo cha Polisi Bunju.

“Tumempokea, anaendelea vizuri na amepata maumivu katika maeneo ya kifuani, kichwani na tumboni,” alisema na kuongeza kuwa taarifa zaidi zitatolewa baadaye.

Alifafanua kwamba kwa sasa wanajitahidi kumpatia matibabu, ingawa alipelekwa hospitalini hapo akiwa katika hali ambayo siyo nzuri, na uchunguzi zaidi unaendelea.

Wanaharakati walaumu Serikali
Miongoni mwa watu wa kwanza kufika katika Kituo cha Polisi Bunju kumuona Dk Ulimboka ni Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo-Bisimba ambaye alisema kilichotokea kinaonyesha jinsi gani Serikali ilivyo na woga katika kushughulikia  matatizo ya wananchi.

Dk Bisimba alisema wao wanaamini kuwa tukio hilo lina mkono wa Serikali na kama ni kinyume cha hapo, basi inapaswa kuwaridhisha wananchi kuwa hawana mkono wao katika sakata hilo.

“Kama wao hawana mkono wao basi wanapaswa kuwaridhisha wananchi kuwa hawahusiki kwa kuwatia mbaroni wahusika na kuwafikisha katika vyombo vya sheria,” alisema Bisimba.

Mkurugenzi huyo alisema matamshi ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda bungeni jana kuwa wanashughulikia suala la madaktari na watalimaliza liwalo na liwe inaleta tafsiri kuwa kilichotokea kina mkono wao.

“Alivyosema liwalo na liwe na kinachotokea sasa kinabainisha kuwa mengi zaidi yatafuata,” alisema Bisimba na kuongeza kuwa hali hiyo inasikitisha na haikuwahi kufikiriwa.

Bisimba alisema baada ya wasamaria kumkuta mnamo saa 12:00 asubuhi, walimpeleka katika kituo kidogo cha Polisi cha Bunju ambako polisi walifungua mashtaka ya wizi wa maungoni na kupatiwa RB yenye namba BJ/RB/1870/2012.
“Mimi nilipata taarifa za kutekwa kwake kutoka kwa mwenzie aliyekuwa naye mnamo saa nane usiku, na baada ya kupata taarifa hizo niliwaeleza wanaharakati wenzangu juu ya hatua za kuchukua,” alisema Bisimba.

Bisimba alisema aliwasili katika Kituo cha Polisi cha Bunju, jana mapema asubuhi na kumkuta Dk Ulimboka akiwa amejeruhiwa vibaya, lakini hakuwa amepatiwa huduma yoyote.

“Tulikwenda kumchukua na kukuta hali yake ni mbaya, lakini cha ajabu pamoja na majeraha yote hakupatiwa msaada wowote wa huduma, jambo ambalo lilitusikitisha sana,” alisema.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sikika, Irenea Kiria alisema kilichotokea ni kitu kibaya na kinaonyesha jinsi gani Serikali inavyoshughulika na watu, badala ya kujali hoja za msingi ambazo zinawasilishwa.

Kiria alisema hoja za madaktari zilipaswa kusikilizwa kwani licha ya madai ya masilahi yao lakini pia wanapigania mazingira bora yenye utu kwa ajili ya wagonjwa.

Madai mengine ni upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwa ajili ya kuwahudumia wananchi pamoja na upatikanaji wa dawa, mambo ambayo alisema hayahitaji mjadala.

“Suala la masilahi ya madaktari linazungumzika lakini siyo suala la dawa, mazingira bora ya kuwahudumia wagonjwa na upatikanaji wa vifaa tiba na vipimo vingine,” alisema Kiria.

Nchimbi: Tutawasaka
Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi alisema Serikali imeliagiza Jeshi la Polisi kuwasaka na kuwachukulia hatua watakaobainika kuhusika na utekaji huo.

Dk Nchimbi alisema mjini Dodoma kuwa Serikali haihusiki kwa namna yoyote ile na utekaji nyara huo, na kwamba kitendo hicho kinapaswa kulaaniwa kwani hakikubaliki katika jamii hasa kwa zama hizi.

“Kwanza, madaktari ni watu muhimu ambao wao ndio wanaotuwezesha sisi kuishi, kwa hiyo wapo kwa ajili ya maisha yetu, hata kama asingekuwa daktari, kwa mtu yeyote yule, jambo hili halikubaliki katika nchi yetu,” alisema Dk Nchimbi na kuongeza:

“Tumewaagiza polisi wafanye uchunguzi ili kuwabaini wahusika na wakipatikana wafikishwe katika vyombo vya sheria, maana hatuwezi kwa namna yoyote kuvumilia vitendo vya aina hii.”

Alisema Serikali imestushwa sana na tukio hilo na haitavumilia kwa namna yoyote vitendo hivyo pamoja na vile vya unyanyasaji kwani ni kinyume cha sheria.

Kuhusu kupigwa kwa Mkuu wa Upelelezi (OC- CID), ASP Mukiri, Dk Nchimbi alisema lilikuwa ni tukio la bahati mbaya kwamba madaktari waliokuwapo Muhimbili walishindwa kuwa na uvumilivu kwani askari aliyepigwa alikuwa ameagizwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela kwenda kufuatilia matibabu ya Dk Ulimboka.

“Hapa ndipo ninapotofautiana na watu wengi, mnampigaje polisi, maana yule anapaswa kuwa rafiki wa raia, sasa unampigaje mtu ambaye ni mlinzi na umemwajiri, analipwa kwa kodi yako?” alihoji Dk Nchimbi.

Yaliyojiri bungeni
Tukio hilo lililosambaa kwa kasi katika mitandao ya kijamii na vyombo vya habari, liliibuka bungeni, ambako Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee alilaani vikali kitendo cha watu wanaodaiwa ni maofisa wa vyombo vya usalama kumpiga Dk Ulimboka.Alisema kitendo hicho ni unyama unaostahili kukemewa na kila mpenda amani hapa nchini.

“Tumestushwa na tukio hilo na tunalaani vikali kitendo hicho na kumwombea Dk Ulimboka ili apone haraka,” alisema Mdee.Katika hatua nyingine, Mwananchi lilitembelea hospitali za Mwananyamala, Temeke na Amana, kujionea hali ilivyokuwa baada ya kusambaa kwa taarifa za kupigwa kwa Dk Ulimboka.
Katika hospitali ya Mwananyamala, wengi walioonekana walikuwa ni wauguzi huku madaktari wakidaiwa kwenda katika hospitali ya Muhimbili kumuona mwenzao aliyejeruhiwa.
Dk Ulimboka aliwahi kufanya kazi katika hospitali hiyo ya Mwananyamala katika miaka ya nyuma.

Hata hivyo, juhudi za waandishi kuzungumza na uongozi wa hospitali hiyo, hazikufanikiwa baada ya wafanyakazi wa Ofisi ya Mganga Mkuu kusema kuwa mganga huyo amekataa kuzungumza, akiwataka waandishi wafike ofisini kwake leo.
“Ameniambia niwapeleke kwa katibu wake, lakini na yeye nimemkosa, sasa nimerudi kwake ameniambia niwaambie mrudi kesho,” alisema katibu muhtasi wake.
Katika hospitali za Temeke na Amana, hali pia ilikuwa hivyo, baadhi ya wahudumu waliokutwa katika hospitali hizo wakikataa kuzungumza kwa madai kuwa wanaotakiwa kuzungumza hawapo.

Madaktari jeshini waitwa kazini
Taarifa zilizotufikia wakati tukienda mitamboni, ambazo hazijathibitishwa, zilieleza kwamba madaktari wote wanaofanya kazi kwenye hospitali za jeshi ikiwamo Lugalo ambao hawakuwa zamu jana jioni, waliitwa kazini, tukio ambalo linahusishwa na tamko la Serikali linalotarajiwa kutolewa leo.

Imeandikwa na Nora Damian, Boniface Meena,  Fredy Azzah, Elizabeth Edward, Geofrey Nyang’oro, Zakhia Abdallah , Joseph Zablon, Raymond Kaminyoge, Aidan Mhando, Dar; Neville Meena, Dodoma

No comments:

GEITA DOCUMENTARY

Contributors