Saturday, 19 May 2012

TANESCO NA POLISI WAZUNGUMZA KUHUSU MADENI


 WAKATI Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) likiwa limetangaza opresheni ya kuwakatia umeme polisi nchi nzima, wahasibu wa jeshi hilo mkoani Kilimanjaro walikuwa katika mazungumzo mazito na shirika hilo ili kuangalia namna ya kuepusha dhahama hiyo.
Habari zilizopatikana jana mchana zilisema Mhasibu wa Polisi mkoani Kilimanjaro na mwenzake wa Chuo cha Polisi, walikuwa katika mazungumzo hayo.
Hadi saa 9:00 mchana wa juzi umeme ulikuwa ukiwaka katika vituo vyote vya polisi, kambi na makazi ya maofisa wa polisi, lakini Tanesco walitarajia kukata umeme wakati wowote kama wasingefikia muafaka.
Dharura ya umeme iliyotokea saa 4:00 juzi na kusababisha kukatika kwa umeme hadi saa 9:00 alasiri, kuliwatia kiwewe baadhi ya polisi hasa wale wa Idara ya mawasiliano.

Katika kipindi hicho, Idara ya mawasiliano ya simu za upepo ya polisi ,ilikuwa katika wakati mgumu zaidi kutokana na redio za masafa marefu kushindwa kufanya kazi kutokana na kukatika kwa umeme.
Hata hivyo redio hizo zilirudi kufanya kazi kawaida baada ya umeme kurejea saa 9:00 alasiri lakini polisi walionekana wakiandaa jenereta ili kukabiliana na ukataji wa umeme.

Meneja wa Tanesco wa Mkoa wa Kilimanjaro, Zakayo Temu, alilithibitishia gazeti hili juu ya kuwapo kwa mazungumzo kati yao na wahasibu wa Idara za polisi lakini maagizo aliyonayo ni kuwakatia umeme wasipolipa.

Baadhi ya polisi waliohojiwa walisema itakuwa ni fedheha na aibu kubwa kama watakatiwa umeme hasa ikizingatiwa kuwa fedha za kulipia huduma hiyo zinatengwa katika bajeti ya serikali kila mwaka.

Wakati Tanesco ikichukua hatua hiyo, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Moshi (Muwsa), inazidai idara zilizopo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani, madeni ya zaidi ya Sh264.7 milioni.
Februari mwaa huu, Mkurugenzi Mtendaji wa Muwsa,Anthony Kasonta alizitaja taasisi hizo ni ofisi ya RPC Kilimanjaro, MPA na Magereza.

No comments:

GEITA DOCUMENTARY