Mabadiliko katika mfumo wa dunia
tangu kuingia kwa karne mpya, ikiwa ni pamoja na utulivu mkubwa wa hali
ya kisiasa barani Afrika na kuongezeka kwa bidhaa muhimu, kama
vikitumiwa vizuri, vitatoa fursa kwa Afrika kuwa nguvu kubwa ya uchumi
duniani. Hayo yamo kwenye utangulizi wa Ripoti ya uchumi kuhusu Afrika
inayoitwa "Kutumia vizuri bidhaa za Afrika: mabadiliko ya viwanda kwa
ukuaji, ajira, na mageuzi ya kiuchumi" ulioandikwa na Carlos Lopes,
naibu katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa ambaye pia ni mkurugenzi mtendaji
wa Kamati ya Umoja wa Mataifa kuhusu uchumi wa Afrika akishirikiana na
mwenyekiti wa Kamati ya Umoja wa Afrika, Nkosazana Dlamini-Zuma.

Pia wamesema nchi za Afrika zina fursa kubwa ya kutumia vizuri
rasilimali zilizo nazo na bei kubwa ya bidhaa katika soko la kimataifa,
pia zinaweza kutumia fursa zinazotokana na mabadiliko ya uchumi wa dunia
kuinua zaidi uchumi wao kupitia mageuzi ya viwanda na kukabiliana na
umasikini, ukosefu wa usawa, na tatizo la ajira hasa kwa wasomi lukuki waliopo afrika na pia watu wenye elimu ya chini. Endapo fursa hizi
zitatumiwa ipasavyo, zitaisaidia Afrika kuongeza uwezo wake wa
ushindani, kupunguza kutegemea usafirishaji wa bidhaa ghafi na udhaifu
unaotokana na mambo hayo, hivyo kuibuka kuwa nguzo muhimu ya ukuaji wa
uchumi wa dunia.
