Umoja wa mataifa unasema kuwa maelfu ya Wapalestina wanakimbia kutoka kwenye kambi moja ya wakimbizi iliyo karibu na mji wa bandari wa Latakia nchini Syria. Kambi hiyo imekuwa ikishambuliwa kwa makombora na jeshi la Syria kwa siku ya tatu mfululizo.
Watu wasiopungua 30 wameripotiwa kuuwawa tangu jumamosi ambapo vikosi vya serikali vilianza kutekeleza harakati hizo za kijeshi kutoka ardhini na baharini. Msemaji wa Umoja wa Mataifa Christopher Gunness, ameiambia BBC kwamba takriban nusu ya wakimbizi kwenye kambi hiyo yenye watu elfu kumi wanaukimbia mji huo.
Gunness amesema wafanyakazi wa umoja huo walio katika kambi hiyo wanahitaji msaada wa dharura kufuatia harakati hizo za kijeshi kwenye mji huo wa Latakia. Jumuiya ya kimataifa imelaani harakati hizo za kijeshi za serikali ya Syria dhidi ya wapinzani wa Rais Bashar Assad.
Akizungumza na waandishi wa habari, Waziri wa mashauri ya nchi za kigeni wa Uturuki Ahmet Davutoglu, amelaani hatua ya wanajeshi wa Syria kuwalenga raia wa miji ya Latakia na Deir al-Zor mashariki mwa taifa hilo. Davutoglu amesema hatua hizo za kijeshi zinakiuka haki za binadamu na kamwe hazitavumiliwa.
No comments:
Post a Comment