Waziri wa Nishati na Madini, Mhe. William Ngeleja
amesema uwekezaji unaoendelea hivi sasa katika mikoa ya kusini ni kiashiria kizuri juu ya kukua kwa uchumi wa mikoa hiyo na hasa katika bandari ya Mtwara.
Alikuwa akitoa ufafanuzi huo kuhusu uamuzi wa kampuni ya Petrobas ya Brazili kuweka meli yake katika bandari ya Mtwara wakati ikifanya kazi ya utafiti wa mafuta na gesi katika pwani ya Mtwara hadi Mafia.
Akizungumza mara baada ya kutembelea eneo la viwanda vya kujenga meli (ship building area) na kuikagua meli ya uchimbaji mafuta iitwayo Poisedon ambayo inajengwa katika bandari ya Geoje, iliyoko kusini mashariki mwa Seoul, Mji Mkuu wa Korea Kusini, Waziri Ngeleja alisema uwekezaji huo utatoa fursa nyingi zikiwemo ajira na biashara ya nchi za nje.
“Kitu kikubwa tunachotaraji ni kuona ajira zikiongezeka kwa watu wa mikoa ya Lindi na Mtwara… kutakuwa na ajira nchi kavu, majini na ajira kwa ajili ya watoa huduma kwenye mahoteli na makazi ya hawa wawekezaji,” alisema.
Alisema eneo jingine litakalonufaika na uwekezaji huo ni utalii na biashara ya mahoteli ambalo alisema linaenda sambamba na ukuaji wa miji ya Lindi na Mtwara na akatoa changamoto kwa viongozi wa mikoa kujipanga vizuri kwa kusimamia suala la mipangomiji ili uwekezaji huu usiwapite kando.
“Ni lazima wajipange vizuri kwa kutenga maeneo ya viwanda, maeneo ya makazi, maeneo ya starehe ili miaka ijayo kusiwe na msongamano kana kwamba hatukutarajia ukuaji huo. Ukuaji wa kasi wa miji ni dhahiri mahali popote penye uwekezaji mkubwa,” alisisitiza.
Alisema kukua kwa bandari ya Mtwara kutainuliwa pia na shughuli nyingine za uzalishaji ambazo alizitaja kuwa ni uzalisaji wa umeme kutokana na gesi, kujengwa kwa kiwanda cha mbolea, cha saruji, na uzalishaji wa bidhaa zinazotokana na gesi (petrochemicals) ambazo alisema zinatumika zaidi viwandani.
“Kuna fursa ya uuzaji wa bidhaa nje ya nchi (exportation) kutokana na uzalishaji wa gesi ya kupikia (Liquified Natural Gas – LNG), tukijipanga vizuri mikoa ya kusini itabadilika na kuonekana tofauti,” alisema.
Alisema fursa nyingine ni uwepo wa barabara ya Mtwara-Mangaka-Tunduru-Namtumbo-Songea ambazo zimepata fedha katika awamu tofauti na kwamba kazi ya ujenzi iko katika hatua za awali.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
ALHAMISI, JULAI 07, 2011.
1 comment:
Regards for this post, I am a big fan of this web site would like to keep
updated.
Post a Comment