INTERNATIONAL NEWS

Mkuu wa polisi wa Congo asimamishwa kazi
Floribert Chebeya
Mkuu wa polisi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo amesimamishwa kazi kufuatia kifo cha mwanaharakati wa haki za kibinadamu.

Waziri wa mambo ya ndani wa Congo amesema maafisa wengine watatu wa jeshi la polisi wametiwa mbaroni, na rais wa nchi hiyo ameamua kushughulikia kesi hiyo.

Floribert Chebeya, mkuu wa kundi la kutetea haki za binadamu, alipatikana akiwa amekufa katika gari lake karibu na mji mkuu, Kinshasa siku ya Jumatano.

Iliarifiwa kuwa siku hiyo alitarajiwa kukutana na mkuu wa polisi.

Polisi pamoja na kundi aliloongoza Bw Chebeya wamesema mkutao huo haukufanyika.


Mwandishi wa BBC mjini Kinshasa amesema mkuu wa polisi, Bw John Numbi, anaonekana kama mshirika wa karibu wa Rais Joseph Kabila.

Wanaharakati wa haki za kibinadamu wanasema Bw Chebeya alikuwa akipokea vitisho katika miaka ishirini iliyopita.

Siku ya Ijumaa, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon alitoa wito wa kufanyika uchunguzi huru juu ya tukio hilo, huku serikali nayo ikiitisha uchunguzi wake.

Katika taarifa kupitia televisheni, Waziri wa Mambo ya Ndani Adolphe Lumanu alisema Rais Kabila "ananuia ukweli ujulikane" juu ya mauaji ya Bw Chebeya.

"ili kuruhusu uchunguzi ufanyike vizuri, baraza la usalama la taifa liliamua kama hatua ya tahadhari kumsimamisha kazi inspector generali John Numbi," taarifa hiyo ya serikali ilisema.


Wanaume wapendanao waachiwa Malawi

Wapenzi wa jinsia moja
Wanaume wawili wanaofanya mapenzi ya jinsia moja nchini Malawi waliofungwa baada ya kufanya sherehe ya uchumba wamesamehewa na Rais Bingu Wa Mutharika.

Bw Mutharika, akizungumza wakati katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa alipotembelea nchi yake, amesema ameamuru waachiliwe huru haraka iwezekanavyo.

Steven Monjeza na Tiwonge Chimbalanga walihukumiwa kifungo cha miaka 14 jela mapema mwezi huu kwa kufanya vitendo kinyume cha maumbile na vitendo vya aibu.

Kesi hiyo iliibua malalamiko kutoka nchi za kimataifa napia mjadala juu ya mapenzi ya jinsia moja ndani ya Malawi.

Bw Ban ameusifu uamuzi wa Rais kuwa ni wa "kijasiri."

Amesema, "Sheria hii iliyopitwa na wakati irekebishwe popote ilipo."



Waasi wajinufaisha na madini DRC

Makundi ya waasi yamejinufaisha na biashara haramu ya madini

Ripoti iliyotolewa na baraza la usalama la Umoja wa Mataifa imesema makundi ya waasi mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo yanaendelea kukusanya ushuru kinyume cha sheria kutoka kwa watu wanaohudumu katika kiwanda cha kuchimba madini ya dhahabu.

Ripoti hiyo pia imewasilisha ushahidi kuthibitisha kuwa waasi hao wanatumia stakabadhi gushi za Umoja huo ili kuyauza madini hayo katika mataifa jirani.

Waasi wa CNDP vile vile wametuhumiwa kuweka vituo vya ukaguzi na kuwatoza wenye magari na raia kodi kinyume cha sheria.

Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo ina mali asili za madini nyingi lakini makundi ya waasi wenye silaha wanadhibiti biashara hii.

Makundi haya yanaarifiwa kupata faida kutokana na biashara hii ya mamilioni ya dola kutokana na madini na kudhibiti migodi kwa nguvu na kuomba hongo au kodi.

Mchango wa biashara ya madini umetambulika kuwa moja ya sababu zinazochochea vita na kuchangia ukiukwaji wa haki za binadamu mashariki mwa nchi hii tangu kuanza kwa vita.

No comments:

GEITA DOCUMENTARY

Contributors